Utambulisho wa Drogba wateka Bunge
Mshambuliaji wa zamani wa timu ya Taifa ya Ivory Coast na Klabu ya Chelsea, Didier Drogba akiwa amesimama wakati wa kutambulishwa leo Mei 4, 2026, bungeni jijini Dodoma.
Muktasari:
- Drogba ametambulishwa Bungeni kama mgeni wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Paul Makonda akiwa miongoni mwa wageni katika siku ambayo hotuba ya Wizara hiyo inasomwa leo.
Dodoma. Nyota wa zamani wa Timu ya Chelsea na Timu ya Taifa ya Ivory Coast Didier Drogba ameteka ukumbi wa Bunge baada ya kutangaza jina lake na Spika.
Drogba (48) amekuwa nyota katika kikosi cha Chelsea ambako alicheza kwa mafanikio makubwa.
Drogba ametambulishwa bungeni kama mgeni wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Paul Makonda akiwa miongoni mwa wageni katika siku ambayo hotuba ya wizara hiyo inasomwa leo.
Mapema asubuhi Drogba ameingia tofauti na wageni wengine ambao hutumia lango C lakini aliingia kwa kutumia lango A ambalo ni maarufu kama lango la Waziri Mkuu.
Ameingia na kupokewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Gerson Msigwa.
Mara baada ya Spika kumtambulisha, wabunge walipiga makofi kwa sauti za juu na kuchukua muda mrefu kuliko mgeni mwingine yeyote aliyetambulishwa kwa siku ya leo.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda akiwa pamojana mshambuliaji wa zamani wa timu ya Taifa ya Ivory Coast na Klabu ya Chelsea, Didier Drogba katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma leo Mei 4, 2026.
Hata hivyo, utambulisho wa Drogba na kocha Mkuu wa Timu ya Taifa Miguel Gamondi ulikuwa tofauti kwani wageni wengine walitambulishwa na Mwenyekiti wa Bunge Najma Giga lakini hawa wengine walitambulishwa na Spika.
Hii si mara ya kwanza kwa Drogba kuja Tanzania kwani alishawahi kuja na timu yake ya Taifa ya Ivory Coast.