Utovu wa nidhamu waigharimu Simba, Yanga yawaponza marefa
Muktasari:
- Yanga inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa imekusanya idadi ya pointi 32 katika michezo 12 ikifuatiwa na JKT Tanzania na Azam.
Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), leo Machi 6, 2026 imetangaza adhabu mbalimbali kutokana na matukio ya utovu wa nidhamu yaliyojitokeza katika mechi za hivi karibuni za ligi huku Simba ikiongoza kwa kupata adhabu kubwa.
Katika adhabu hizo Simba imeongozwa kwa kutozwa faini kubwa zaidi ambapo italazimika kulipa kiasi cha Sh22 milioni kutokana na makosa yaliyofanywa na timu kiujumla na baadhi ya wachezaji wake.
Wakati huohuo, Refa mmoja ameshushushwa daraja na mwingine kufungiwa miezi sita kwa makosa waliyoyafanya ambayo yameonekana kuinufaisha Yanga.
Makosa matatu ambayo Simba imeyafanya katika mchezo dhidi ya Yanga ambao ulimalizika kwa sare ya bila kufungana, yameifanya itozwe Sh15 milioni na lingine moja dhidi ya Dodoma Jiji limeifanya itozwe Sh5 milioni.
Makosa dhidi ya Yanga ni kuingia kwa kutumia mlango usio rasmi, kukataa kutumia chumba kisicho rasmi na kosa la walinzi wake kugombana na wa Yanga na kutoleana lugha chafu.
Kosa dhidi ya Dodoma Jiji ni la mashabiki wake kumrushia makopo ya maji mshambuliaji Edgar William.
Selemani Mwalimu wa Simba amefungiwa mechi tatu na faini ya Sh1 milioni kwa kosa la kumpiga kiwiko Andy Bikoko wa Dodoma Jiji huku David Kameta akitozwa faini ya Sh1 milioni kwa kosa la kufanya vitendo vya kishirikina katika mchezo dhidi ya Yanga.
Yanga imetozwa Sh5 milioni kwa kosa la walinzi wake kupigana na kutoleana lugha chafu na wale wa Simba.
Timu inayoshika nafasi ya pili kwa kutozwa faini kubwa ya fedha ni Dodoma Jiji ambayo kiujumla imetozwa faini ya Sh10 milioni.
Kiujumla Bodi ya Ligi itavuna kiasi cha Sh51.8 milioni kutokana na adhabu za faini ambazo timu, wachezaji na maofisa tofauti wamepewal kwa sababu ya makosa ya uvunjifu wa kanuni waliyofanya.
Mbali na adhabu za faini na vifungo kwa wachezaji na maofisa wa timu, Kamati ya Uendeshaji pia imetembeza rungu kwa waamuzi walioshindwa kutafsiri vyema baadhi ya matukio katika mechi walizochezesha.
Refa Abdallah Mwinyimkuu wa Singida ameshushwa daraja kwa kushindwa kuipa Namungo adhabu ya penalti dhidi ya Yanga.
Refa Charles Simon wa Dodoma amefungiwa miezi mitatu kwa kosa la kuruhusu Dodoma Jiji kufanya mabadiliko ya wachezaji kwa mikupuo minne dhidi ya Simba.
Refa Msaidizi Kassim Mpanga amefungiwa miezi sita huku Hamdan Said akifungiwa miezi mitatu kwa kushindwa kutafsiri sheria ya kuotea katika mchezo baina ya Yanga na Simba.