VIDEO: Kocha mpya Simba atua, atoa neno
Muktasari:
- Hemed Morocco aliiongoza Taifa Stars kufika hatua ya robo fainali ya Kombe la Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) 2024.
Dar es Salaam. Wakati Hemed Morocco akitarajiwa kuungana na Simba leo kwa ajili ya kuinoa kwa muda, Kocha huyo amesema kuwa yupo tayari kwa jukumu lililo mbele yake.
Morocco ambaye pia ni kocha wa timu ya taifa Taifa Stars,amesema, anakwenda kukutana na viongozi wa Simba, kisha baada ya hapo ataanza mara moja kazi hiyo.
"Nimefika salama namshukuru Mungu,ninachoweza kusema na kwenda kukabiliana na changamoto nzuri, lakini ina ugumu wake,"amesema Morocco ambaye amewahi kuzifundisha klabu za Namungo, Geita, Coastal Union.
"Haikuwa rahisi kukubalina na hili jukumu unajua Mimi bado ni kocha wa timu ya taifa, lakini baada ya kuzungumza na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) maana wao ndio waajiri wangu walikubali kunipa hiyo nafasi.
"Nimetanguliza weledi kwenye kuamua hili, na kwenda Simba ni timu kubwa, nahitajika kwenda kutuliza presha ya wafuasi wake wengi ambao wanatarajia kuona timu yao inatulia.
"Nakwenda kujiunga na timu ambayo sikufanya usajili na ipo kwenye mashindano, lakini pia haikuwa na utulivu mkubwa, nampongeza kocha aliyetangulia Fadlu (Davids) ni rafiki yangu amefanya kazi yake nzuri na ameondoka nadhani ni hatua ya kuanzia hapa alipoishia na kwenda mbele," amesema Morocco.
Morocco amesema kuwa, ametua Simba kwa ajili ya kuchukua nafasi ya muda mfupi, wakati klabu inasaka kocha mpya atakaekuja kukiongoza kikosi hicho msimu huu wa 2025/26.
"Nimetua Simba kuja kuchukua nafasi ya muda kuifundisha timu hiyo, baada ya aliyekuwa kocha wa wekundu hao Fadlu kusitisha ajira yake, hivyo nipo kwa ajili ya mechi chache zijazo hasa kimataifa," amesema Morocco.