Vigogo Simba wavamia Ghana, kuibuka na mashine mbili, mmoja akacha timu ya Taifa

Muktasari:

  • Mbali na hilo pia wamepania kucheza soka la kiwango cha juu na kupata wadhamini wa fedha nyingi zaidi ya walionao kwa sasa.

SIMBA wameanza ziara ya anga kwa anga kusaka mashine mpya za kurejesha heshima msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa inayoanza Septemba wao wakianzia hatua ya awali badala ya mtoano.

Zamoto kabisa kutoka ndani ni vigogo wake wawili wako nchini Ghana kufuatilia wachezaji wanne ambao mwishowe watachagua wawili ingawa kuna fowadi mmoja anaweza kutambulishwa wikiendi. Agustine Okrah anayekiwasha Backem United.

Huyu mchezaji analalamikiwa na wadau wa michezo wa Ghana kwa kukataa wito wa timu ya Taifa ambayo ipo Japan kwenye mechi kadhaa za kirafiki. Wanadai amepiga chini wito huo ili amalizane na Simba, ingawa amefafanua alipiga chini kwa vile hayuko fiti.

Okrah mwenye miaka 28 ametupia mabao 14 kwenye mechi 31 za msimu huu wa Ligi ya Ghana akiwa na Backem United. Kwa Okrah Simba inaelezwa kuwa kwenye hatua nzuri ya kumsainisha mkataba wa miaka miwili na inaelezwa ni miongoni mwa wachezaji machachari zaidi kwa sasa.

Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti inazo ni viongozi hao wamepewa baraka na bodi ya Simba na miongoni mwa mastaa walioko kwenye rada yao ni fowadi Mcameroon anayecheza Asante Kotoko ya Ghana, Franck Mbella Etouga.

Habari zinasema Simba wamepania ama kupata fowadi ya maana, beki mbadala wa Serge Wawa pamoja na kiungo mkabaji. Habari zinasema Bilionea wa Simba, Mohamed Dewji Mo yuko nchini Dubai kwa ishu zake za kibiashara lakini amekunjua roho na kuwaambia viongozi Simba watafute mafundi pesa ipo.

Ingawa Simba wanafanya mambo kimyakimya na kwa siri kubwa, lakini Mwanaspoti linajua wamepania kumaliza mambo kwa haraka ili kupata muda wa kupumzika na kujiandaa na msimu mpya.

Kati ya malengo ambayo Simba wamepania msimu ujao wakiwa chini ya kocha mpya ni kufuzu nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na kutetea makombe yao yote ya ndani waliyopoteza msimu huu.

Mbali na hilo pia wamepania kucheza soka la kiwango cha juu na kupata wadhamini wa fedha nyingi zaidi ya walionao kwa sasa.