Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vilio vya wagombea TFF ni dalili kwamba hawakujiandaa

Muktasari:

  • Mmoja wa wagombea waliotia huruma katika mchakato huu ni ndugu Mustafa Salum Himba, ambaye pia ni mjumbe wa kamati moja wapo za klabu ya Yanga.

Kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi TFF, Ijumaa ya Juni 20, 2025, ndio ilikuwa siku ya mwisho ya kuchukua na kurudisha fomu 

Hatua inayofuata ni kikao cha mchujo wa awali wa wagombea na kuandika barua za kuwajulisha wagombea juu ya mchujo wa awali .

Kazi hii itafanywa na Kamati ya Utendaji na wagombea wa awali watatangazwa Juni, kesho Jumanne ya Juni 24, 2025.

Lakini hadi kufikia hatua hiyo, kumekuwa na vilio vingi sana kutoka kwa watia nia wakilalamikia hujuma.

Mmoja wa wagombea waliotia huruma katika mchakato huu ni ndugu Mustafa Salum Himba, ambaye pia ni mjumbe wa kamati moja wapo za klabu ya Yanga.

Ndugu huyu na mwanasheria wake wakili Aloyce Komba, waliibuka na kutoa malalamiko mengi kuhusu mchakato wa uchaguzi. 

Himba alichukua fomu ya kugombea,  akaijaza na kutaka kuirudisha.

Lakini bahati mbaya akakosa vigezo kwa kuwa hakupata wadhamini (angalau 5) wanaohitajika kikanuni.

Akaita waandishi wa habari na kuanza kumtupia lawama mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi.

Kupitia mkasa wa ndugu huyu tu inatosha kuamini kwamba watu hawakujipanga kugombea, ila wameshtuka tu ghafla mchakato umefika na wao wakaingia.

Katika hali ya kawaida huwezi kwenda kuchukua fomu ya kugombea hata nafasi ndogo kiasi gani bila kujua wadhamini wako.

Hii sio sifa ya mtu anayestahili kuwa kiongozi wa taasisi kubwa kama TFF.

Nimeshangaa zaidi kuona hata mkongwe wa soka, Ally Mayay, naye pia amekosa wadhamini...maana yake na yeye hakujiandaa.

Mayay, mchezaji wa zamani wa CDA ya Dodoma na Yanga, ana uzoefu mkubwa wa kugombea kwa sababu hii ni mara yake ya tatu.

Alianza 2017 na kushindwa na Wallace Karia katika uchaguzi uliofanyika kwenye ukumbi wa St. Gasper Dodoma.

Akarudi kwa kishindo mwaka 2021 akiambatana na Mtemi Ramadhan, nyota wa zamani wa Simba na Taifa Stars, aliyewania nafasi ya makamu wa Rais.

Wakafanya maandamano maalumu siku ya kurudisha fomu, hadi makao makuu ya TFF, Karume, wakiwa na kaulimbiu ya Bring Back Our Football au Turudishie Mpira Wetu.

Kaulimbiu hii ilimaanisha kwamba mpira ulivamiwa na watu wasio wa mpira, hivyo yeye na Mtemi ambao ni watu wa mpira, wanataka wavamizi wawarudishie mpira wao.

Kaulimbiu hii aliikopa kutoka Nigeria ilipotumika katika harakati za kuwakomboa mabinti waliotekwa na kundi la Boko Haramu, Bring Back Our Girls.

Hata hivyo, akashindwa!

Ilitarajiwa kumuona safari hii akija kwa kishindo zaidi ya kile cha 2021...lakini wapi, kakosa hata wadhamini. 

Uchaguzi wa mpira ni sawa na uchaguzi mwingine wowote, hutawaliwa na faulo ndogo ndogo.

Mtu aliyejipanga kugombea hufanya utafiti na kujua kila kitu kuhusu siasa za uchaguzi na anapoingia anaingia miguu miwili.

Mgombea anapokwama kupata wadhamini, anatoa ujumbe mmoja tu kwamba hakuwa amehipanga sawasawa.

Wadhamini hupatikana kwa kujenga ushawishi, na hiyo ndio itakuwa kazi yako katika kipindi chote cha uongozi wako kama utashinda.

Unaposhindwa kupata wadhamini angalau watano, maana yake umeshindwa kushawishi watu watano tu...utaweza kushawishi wadau mbalimbali katika uongozi wako?

Mojawapo ya kauli za medani za kivita inasema wakati wa amani ndio wakati wa kujiandaa na vita.

Wagombea hawa waliokosa wadhamini sasa hawakuijua kauli hii mapema, matokeo yake wakaanza kujiandaa na vita wakati wa vita...huwezi kushinda vita hiyo.

Wanachotakiwa kufanya kwa sasa ni kuanza maandalizi ya uchaguzi ujao mwaka 2029.

Uchaguzi pekee ambao unaweza kujiandaa nao pale unapokuwa umefika ni wa baba ntakatifu, Papa...kwa sababu huwa hakuna kampeni wala vipindi maalumu. 

Lakini hizi chaguzi ambazo hujirudia kwa vipindi maalumu, lazima ujipange mapema.

Kwa hiyo wanatakiwa kujipanga sasa...na hasa waweke nguvu zaidi utakapofika wakati wa chaguzi za vyama vya mikoa.