WCB watakata tuzo za TMA, wakiondoka na tuzo saba

Dar es Salaam. Lebo ya muziki ya Wasafi (WCB) usiku wa kuamkia Aprili 30, 2023 katika hafla ya utoaji wa Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) imeng’ara kwa kupata tuzo saba katika vipengele tofauti ambavyo wasanii wake walishiriki.
Akizungumza baada ya kupokea baadhi ya tuzo kwa niaba ya wasanii wa lebo hiyo, Meneja wa wasanii hao ambaye pia ni Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Hamisi Taletale amesema amefurahi kuona wasanii wake wamefanya vizuri katika tuzo hizo huku akijinadi yote hiyo ni kutokana na uongozi bora ambao Wasafi wamekua nao.
“Nafurahi kuona wasanii wangu wanaendelea kufanya vizuri nah ii inasababishwa na uongozi mzuri ambao upo katika lebo,”amesema.
Baadhi ya tuzo zilizobebwa na wasanii wa lebo hiyo ni pamoja na; mwanamuziki bora ya wa mwaka kwa upande wa wanawake ambayo ameshinda Zuchu, video bora ya mwaka (Zuchu), nyimbo bora ya mwaka kwa wasanii wakike Bongo Fleva (Zuchu) huku Mbosso akiondoka na tuzo ya msanii bora wa Bongo Fleva kwa upande wa wanaume naye Diamond amechukua tuzo ya msanii bora wa kiume ambaye ni chaguo la watu katika jukwaa la kidigitali.
Katika washindi wa tuzo hizo hakuna lebo nyingine ya muziki ambayo ilibeba tuzo nyingi kuizidi Wasafi katika hafla hiyo iliyofanyika ukumbi wa Super Dome Masaki jijini Dar es Salaam.
Aidha, Kwa upande wa tuzo maalumu zimekwenda kwa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (Tasuba) ,Taasisi ya Sauti za Busara Zanzibar, Clouds media group na Chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).