Wikiendi ya burudani Robo fainali Euro 2024
Muktasari:
- Leo ndiyo siku ya kwanza ya hatua hiyo muhimu, ambapo mataifa makubwa nane yatakuwa uwanjani kila moja likitafuta nafasi ya kwenda hatua ya nusu fainali.
Munich, Ujerumani. Ndiyo hivyo. Mechi zote za hatua ya robo fainali kwenye Euro 2024 zimeshathibitishwa baada ya Uholanzi na Uturuki kuwa timu za mwisho kukata tiketi ya kucheza hatua hiyo.
Leo ndiyo siku ya kwanza ya hatua hiyo muhimu, ambapo mataifa makubwa nane yatakuwa uwanjani kila moja likitafuta nafasi ya kwenda hatua ya nusu fainali.
Hii ina maana kwamba, kwa leo mechi kati ya Hispania na Ujerumani, italirudisha taifa moja kubwa nyumbani, lakini mechi nyingine itashuhudia aidha Ureno ya Cristiano Ronaldo au Ufaransa na Klylian Mbappe mmoja akiaga mashindano hayo.
Hispania vs Ujerumani
Takwimu zinaibeba Ujerumani kwenye mchezo huu, kwani hakuna taifa lolote ambalo limewahi kuandaa mashindano hayo na kuondolewa hatua ya robo fainali hivi karibuni.
Mataifa manne ya nyuma yalivuka hatua hii na kwenda nusu fainali,England ilishinda kwa penalti dhidi ya Hispania mwaka 1996, Uholanzi ilifanikiwa kuichapa Yugoslavia 6-1 mwaka 2000, Ureno ikiipiga England kwa mikwaju ya penalti 2004, na Ufaransa ikaifumua Iceland 5-2 mwaka 2016.
Mbali na hilo, Ujerumani inaonekana kuwa kwenye wakati mzuri kila inapofika hatua ya robo fainali ikiwa ni robo yake ya 19 kwenye mashindano yote makubwa, Kombe la Dunia imefika mara (14) Euro mara 4 mwaka 1996, 2008, 2012, 2016 na hii ni mara yao ya tano.
Mechi hii itakuwa ni ya wababe wa mabao kwenye michuano ya Euro mwaka huu, Hispania hadi sasa imeshapachika mabao tisa, huku Ujerumani ikiwa imefunga kumi zikiwa ndiyo timu zilizofunga mabao mengi zaidi hadi sasa.
Hata hivyo, Hispania inakwenda kwenye mchezo huu ikiwategemea vijana wadogo wawili winga Nico Williams na Lamine Yamal, ambao wamefanya mambo makubwa kwenye michuano hii hadi sasa.
Yamal mwenye miaka 16, ameshatoa pasi mbili za mabao kwenye michuano hii akiwa ni mchezaji wa tatu mdogo kufanya hivyo kwenye Euro kuanzia mwaka 1980 huku Nico akiendelea kuwa bora kwenye kila mchezo.
Rekodi zinaonyesha kuwa hii itakuwa mara ya nne Ujerumani na Hispania zinakutana kwenye michuano hiyo ya Euro huku Hispania ikishinda mechi mbili mwaka 1984 na 2008 na Ujerumani mara moja 1988. Mara ya mwisho kukutana ilikuwa fainali ya mwaka 2008 ambapo Hispania ilishinda bao 1-0 likifungwa na Fernando Torres.
Pia timu hizo zimewahi kukutana kwenye Kombe la Dunia mwaka 2022 ambapo zilitoka sare ya bao 1-1 kwenye mchezo wa hatua ya makundi.
Ronaldo na Mbappe
Hii ni mechi ya mataifa mawili ambayo awali yalikuwa yanapewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa huu, lakini leo mmoja ataondoka.
Ureno inakwenda kwenye mechi hii ikiwa haijafunga bao kwenye michezo miwili mfululizo iliyopita, baada ya kupoteza 2-0 dhidi ya Georgia na kutoka suluhu ilipovaana na Slovenia kabla ya kuibuka na ushindi wa mikwaju ya penalti 3-0.
Hata hivyo, mambo pia ni magumu kwa Ufaransa ambao hawana bao lolote ambayo wamefunga kwenye mchezo wa wazi, mabao mawili wapinzani wao wamejifunga na bao moja ni la mkwaju wa penalti uliopigwa na Mbappé, hivyo ni mechi ya wababe wawili wenye ukame wa mabao.
Ronaldo ambaye alimwaga chozi baada ya kukosa penalti kwenye mchezo uliopita anakwenda kwenye mechi hii akiwa na rekodi kali zaidi akiwa amecheza michuano hiyo mara sita lakini msimu huu akiwa bado hajafunga kwenye dakika za kawaida, kama akifunga kwenye mechi hii ataweka rekodi ya mchezaji mkubwa zaidi kufunga kwenye Euro.
Hii ni mechi ambayo inakuja miaka 18 baada ya mataifa hayo kukutana mwaka 2006 kwenye fainali za Kombe la Dunia wakati ambapo staa Zinedine Zidane alifunga bao la ushindi kwa mkwaju wa penalti, ambapo mchezaji bora wa mechi hii alikuwa Lilian Thuram, ambaye mtoto wake Marcus, atakuwa uwanjani leo akivaa jezi ya Ufaransa.
Mbappé na Ronaldo wanatakiwa kuwa na tahadhari kubwa wasipewe kadi leo kwani kitendo hicho kitawafanya wakose mchezo wa nusu fainali kama timu zao zitafuzu.
Mtengo kwa England
England itatakiwa kufanya kazi ya ziada wakati itakapovaana na Uswisi kwenye robo fainali nyingine kesho.
Uholanzi ya kocha Ronald Koeman imekata tiketi ya robo fainali baada ya ushindi mnono kabisa wa mabao 3-0 dhidi ya Romania.
Cody Gakpo alifunga bao la kuongoza, kabla ya Donyell Malen kuja kufunga mara mbili kuifanya Oranje kusonga mbele.
Uturuki yenyewe iliichapa Austria 2-1. Merih Demiral aliifungia Uturuki bao la kuongoza kwenye dakika ya kwanza tu, kabla ya kuongeza lingine kwenye dakika 59, yakiwa mabao yake ya kwanza kwenye soka la kimataifa tangu 2022, huku Austria bao lao alifunga Michael Gregoritsch.
England ilitinga robo fainali kwa mbinde, ikihitaji bao la dakika za mwisho kabisa kupitia kwa Jude Bellingham kusawazisha mbele ya Slovakia, kabla ya kufunga la pili kwenye dakika 30 za nyongeza kwa kichwa cha Harry Kane.
England kama itafuzu basi itacheza na mshindi wa mechi ya Uholanzi na Uturuki kwenye nusu fainali siku nne baadaye ili kutinga fainali, itakayopigwa Berlin, Julai 14.
KIPUTE CHA ROBO
FAINALI EURO 2024
-Julai 5: Hispania vs Ujerumani - Stuttgart
Julai 5: Ufaransa vs Ureno - Hamburg
-Julai 6: Uholanzi vs Uturuki - Berlin
-Julai 6: England vs Uswisi - Dusseldorf