WPL inarejea leo kibabe zaidi
Muktasari:
- Msimamo wa ligi unaonyesha hadi sasa Simba Queens iko kileleni ikiwa timu pekee ambayo haijapoteza mchezo wowote ikikusanya pointi tisa.
Dar es Salaam. Raundi ya nne ya Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) inarejea leo zikichezwa mechi nne ikiwemo dabi ya wanajeshi kati ya JKT Queens na Mashujaa Queens itakaopigwa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo.
Msimamo wa ligi unaonyesha hadi sasa Simba Queens iko kileleni ikiwa timu pekee ambayo haijapoteza mchezo wowote ikikusanya pointi tisa.
JKT Queens imeshinda mechi mbili dhidi ya Alliance Girls na Mlandizi, huku ikitoka sare na Bunda Queens ilhali Mashujaa ikisalia nafasi ya tatu baada ya sare mbili na kushinda mechi moja.
Mechi nyingine leo Fountain Gate Princess itaikaribisha Bunda Queens katika Uwanja Tanzanite Kwaraa, Get Program dhidi ya Alliance Uwanja wa TFF Kigamboni, ilhali Ceasiaa ikiialika Mlandizi ambapo zote zinapigwa saa 10 jioni.
Akizungumzia mchezo dhidi ya Mashujaa Queens, Kocha wa JKT Queens, Esta Chabruma alisema timu zote mbili zinajuana kuanzia wachezaji na viongozi hivyo upande wao hautakuwa rahisi. “Tunakwenda kupambania pointi tatu hata ukiangalia msimamo wa ligi wenzetu Mashujaa tunafuatana tukiwa na tofauti ya pointi mbili tu.”
Wakati hizo zikikipiga leo, kesho katika Uwanja wa KMC Complex, Yanga Princess itakuwa nyumbani kuikaribisha Simba Queens ukiwa mchezo wa kwanza wa ligi msimu huu kati ya watani hao wa jadi.
Awali timu hizo zilikutana kwenye Ngao ya Jamii ambapo dakika tisini za mchezo huo zilimalizika kwa sare ya bao 1-1 na Simba kuchapwa kwa penalti 4-3
Kama Simba itapoteza na JKT ikishinda itaipa nafasi kupanda nafasi ya kwanza ikiwa na pointi 10, lakini Yanga ikipoteza itasalia nafasi ya sita ikitegemeana na matokeo ya timu nyingine na ikishinda itasogea hadi tatu bora.