Yacouba aiokoa Yanga kwa KMC

Yacouba aiokoa Yanga kwa KMC

Muktasari:

  • KOCHA Juma Mwambusi ameanza kibarua chake kwa ugumu dhidi ya KMC, mchezo ambao ulikuwa wa kimbinu zaidi, zilizowanyima ujiko washambuliaji kujimwambafai mbele ya Makipa wa timu hizo.

KOCHA Juma Mwambusi ameanza kibarua chake kwa ugumu dhidi ya KMC, mchezo ambao ulikuwa wa kimbinu zaidi, zilizowanyima ujiko washambuliaji kujimwambafai mbele ya Makipa wa timu hizo.
Pamoja na ugumu huo, Yanga bado inaendelea kutawala kileleni ikifikisha pointi 51, ikiwa imecheza mechi 24, huku mchezo huo ukiwa wa kwanza kwa Mwambusi kama kaimu kocha mkuu.
Haikuwa rahisi KMC kupata bao la kuongoza dakika ya 28 kupitia beki wa kushoto David Bryson, ambaye alianza kuukokota mpira kuanzia katikati ya uwanja kisha akapiga shuti la chini chini lililomshinda kipa wa Yanga, Farouk Shikalo.
Mpira ulianza kwa ugumu, hazikuonekana pasi za ufundi zaidi ya mbinu zilizotumiwa na timu zote mpira kuzuia mianya ya mawinga na mastraika kwenda kufunga.
Mechi ilianza kwa kupooza, tofauti na kile kilichotarajiwa na mashabiki wa Yanga kuona timu yao inacheza kwa kasi na kuwa tishio kwa KMC, lakini mambo yakawa ndivyo sivyo dakika 45 za kipindi cha kwanza.
Dakika ya 36 KMC ilikosa bao la pili baada ya Charles Ilanfya kuwatoka mabeki na kipa Shikalo alipokuwa anamuwahi kumkabia kabla ya kufika eneo lake akauchopu mpira lakini vipimo vyake vikawa hovyo, unaenda pembeni mwa magoli.
Ugumu wa mchezo huo kipindi cha kwanza, ulifanya mabeki wa timu hizo wapate kadi za njano wakiwa katika harakati za kuzuia mashambulizi ambao ni Nahodha wa Yanga, Lamine Moro na Bryson beki wa KMC.
Dakika ya 46 Yanga ilisawazisha bao kupitia kwa Sogne Yacouba alifunga kwa kichwa akipokea pasi ya juu ya  Saido ambaye alipiga mpira wa adhabu.
Kusawazisha kwa bao hilo, wachezaji wa Yanga walichangamka na kuanza kucheza mpira wa kasi uliowaamsha mashabiki kushangalia tofauti na mwanzo ambapo walionekana kukata tamaa.
 Dakika ya 64 Abdallah Masoud alipewa kadi ya njano baada ya kumchezea rafu Faisal Salum 'Fei Toto' ambaye alionekana kumpita mchezaji huyo kwa kupeleka mashambulizi mbele.
Naye kocha wa KMC, Habibu Kondo alikumbwa na adhabu ya kadi ya njano kutoka kwa  mwamuzi Nassoro Mwinchui kutoka Pwani, baada ya kuonekana muda mwingi analalamika.
Huu ni mchezo wa kwanza wa Mwambusi akiwa kama kaimu kocha mkuu, akipokea mikoba ya aliyekuwa bosi Cedric Kaze.
Yanga ilimfuta kazi Kaze baada ya kuiongoza timu hiyo katika mechi 18, ilishinda 10, sare saba na ilifungwa mmoja dhidi ya Coastal Union ya Tanga na michezo mitano nyuma ilichezwa chini ya Zlatko Krimpotic.
VIKOSI
 Yanga: Farouk Shikhalo,Kibwana Shomary, Adeyun Salehe, Abdallah Shaibu 'Ninja', Lamine Moro, Mukoko Tonombe, Tuisila Kisinda, Sogne Yacouba, Fiston Abdoulrazak , Saido Ntibazonkiza.

KMC: Juma Kaseja, Israel Patrick, Raphael Bryson, Lusajo Mwaikenda, Andrew Vincent  'Dante', Masoud Cabaye, Abdul Hillary,Kenny Ally, Hassan Kabunda, Charles Ilanfiya, Emmanuel Mvuyekule.
Kocha Mwambusi alifanya mabadiliko alimtoa Fiston/Kaseke, Mukoko/Nchimbi

Mabadiliko ya KMC, kocha Kondo alimtoa Ilanfya/Mathao Anthony, Bryson/Kelvin Kajili