Yanga kujadiliana Sh12 milioni za Morrison

Thursday November 25 2021
milionipic
By Charity James
By Imani Makongoro

Dar es Salaam. Wakati Bernard Morrison akivunja ukimya na kubainisha namna anavyoithamini klabu yake ya zamani ya Yanga, klabu hiyo imeitana ili kujadili namna itakavyomlipa Sh12 milioni nyota huyo wa Simba baada ya kuwashinda kesi ya CAS.

Katibu Mkuu wa Yanga, Haji Mfikirwa ameliambia Mwanaspoti kuwa; “Tumeipokea hukumu kama uongozi hatujakaa kuamua ni njia ipi itumike kumlipa mchezaji huyo kama ambavyo CAS (Mahakama ya Usuluhishi wa kesi za michezo duniani) imetuamuru,” alisema.

Awali Yanga ilitoa taarifa ya Mwenyekiti wa klabu, Mshindo Msolla akiwataka wanachama wao kusonga mbele na kuangalia masuala yaliyo mbele baada ya CAS kutupilia mbali rufaa yao. Yanga ilikata rufaa CAS kupinga uamuzi uliotolewa na Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji ya TFF kwamba Morrison hakuwa na mkataba na Yanga wakati akijiunga na Simba anakocheza hadi sasa.

Uamuzi wa Kamati uliotolewa Agosti 12, 2020 ambao ulikuwa ukieleza kwamba Morrison hakusaini mkataba mpya na timu hiyo, ingawa ilithibitika kwamba Yanga ilimpa Dola 30,000 na kamati kuamuru mchezaji kuzirudisha fedha hizo, kabla ya Yanga kukimbilia CAS. Pia iliitaka Yanga kumlipa mchezaji huyo Sh 12 Milioni kama gharama za uendeshaji wa kesi hiyo, pesa ambayo Mfikirwa alisema wataijadili ili kujua namna watakavyomlipa. Baada ya hukumu hiyo, Morrison alifurahia lakini akasema yameisha tugange yajayo.

Advertisement