Yanga kuwakosa watatu dhidi ya Mazembe, yumo Diarra
Muktasari:
- Hata hivyo kitendo cha wachezaji hao watatu kupata kadi za njano kwenye mechi ya juzi dhidi ya Monastir kina faida kubwa kwa Yanga kuliko hasara ya kukosa mchezo dhidi ya TP Mazembe ambao ni wa kukamilisha ratiba tu kwa vile wameshafuzu robo fainali.
Dar es Salaam. Yanga itawakosa Djigui Diarra, Khalid Aucho na Djuma Shaban katika mechi ya mwisho dhidi ya TP Mazembe ambayo wanahitajika kupata ushindi ili wajihakikishie kumaliza kileleni mwa msimamo wa ligi na sababu ya kukosekana kwao ikiwa ni kutumikia adhabu ya kukosa mechi moja baada ya kukusanya kadi mbili za njano kwa kila mmoja.
Hata hivyo kitendo cha wachezaji hao watatu kupata kadi za njano kwenye mechi ya juzi dhidi ya Monastir kina faida kubwa kwa Yanga kuliko hasara ya kukosa mchezo dhidi ya TP Mazembe ambao ni wa kukamilisha ratiba tu kwa vile wameshafuzu robo fainali.
Faida hiyo kwa Yanga ni kuwa na uhakika wa kuwatumia nyota hao wawili kwenye mechi ya hatua ya kwanza ya hatua ya robo fainali ambao pengine wangeweza kuukosa ikiwa wangecheza dhidi ya TP Mazembe na kuonyeshwa kadi ya pili ya njano kwa kila mmoja.
Kwa mujibu wa kanuni za mashindano ya Klabu Afrika, mchezaji anayetimiza kadi mbili za njano anapaswa kukosa mchezo unaofuata baada ya ule alioonyeshwa kadi ya pili.
Kabla ya mchezo wa juzi dhidi ya Monastir, Diarra alikuwa ameonyeshwa kadi ya njano mara moja ambayo ilikuwa ni katika mchezo wa mwisho wa hatua ya mtoano kabla ya makundi dhidi ya Club Africain ya Tunisia ambao Yanga waliibuka na ushindi wa bao 1-0 kama ilivyokuwa kwa Khalidi Aucho.
Kwa upande wa Djuma Shaban yeye alikuwa ameonyeshwa kadi ya njano katika mchezo ambao Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Baada ya kuonyeshwa kadi juzi, maana yake wachezaji hao watakosa mchezo dhidi ya TP Mazembe ambao hata wakipoteza hakutakuwa na athari yoyote kubwa kwani tayari wapo robo fainali ambayo ni uhakika wataicheza.
Lakini wakati Djuma na Diarra wakijihakikishia kucheza robo fainali, presha kubwa ipo kwa Kennedy Musonda, Stephane Aziz Ki, Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Bacca na Mudathir Yahya ambao kila mmoja ana kadi ya njano moja hivyo yeyote atakayeonyeshwa kadi ya njano dhidi ya TP Mazembe kwenye mechi inayofuata atakosa mchezo wa kwanza wa hatua ya robo fainali dhidi ya timu watakayopangwa nayo.
Kilichotokea kwa Djuma Shaban, Aucho na Diarra ndicho kipo kwa nyota wawili wa Simba, Mohammed Hussein 'Zimbwe' na Kibu Denis ambao nao watakosa mechi ya mwisho ya Simba ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Raja Casablanca ugenini baada ya kutimiza kadi ya pili ya njano kwa kila mmoja kwenye mechi ya Jumamosi waliyoibuka na ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya Horoya.
Zimbwe alipata kadi ya kwanza ya njano katika mechi ya kwanza ugenini ya hatua ya makundi dhidi ya Horoya ambay walipoteza kwa bao wakati Kibu Denis alionyeshwa kadi ya njano katika mechi ya ugenini dhidi ya Vipers.
Wachezaji ambao Simba ipo katika hatari ya kuwakosa kwenye robo fainali ikiwa wataonyeshwa kadi za njano kwenye mechi inayofuata dhidi ya Raja Casablanca ni Joash Onyango, Saido Ntibazonkiza, Henock Inonga, Sadio Kanoute na Moses Phiri ambao kila mmoja ana kadi moja ya njano.
Nyota wa zamani wa Simba, Uhuru Seleman alisema kadi ambazo wachezaji hao wamezipata zina faida kwa timu zao.
"Mechi za robo fainali ni muhimu kuliko hizo za mwisho za hatua ya makundi ambazo hata wakipoteza bado Simba na Yanga zimeshasonga mbele. Ukiangalia hao wachezaji waliotimiza kadi tatu karibia wote ni wazoefu hivyo wanajua wanavyohitajika kwenye timu zao katika hatua muhimu kama robo fainali," alisema Uhuru.