Yanga mzuka mwingi, historia yao mh!

Sunday September 12 2021
makambo pic
By Charles Abel

YANGA imesisitiza ina kikosi kipana na Mnigeria hatoki leo jioni. Straika Heritier Makambo ambaye ameonyesha mzuka wa aina yake mazoezini wiki hii amemhakikishia Kocha Nabi Mohammed na matajiri wa Yanga kwamba leo Rivers United lazima wapigwe.

Mazoezi ya juzi vigogo wa Yanga walijazana kuwapa mzuka wachezaji kuhakikisha wanafanya mambo na kumaliza mechi mapema. Viongozi wamepania kama kukipatikana matokeo mazuri kwenye mechi ya kesho watakodi ndege maalumu kwenda na kurudi nchini Nigeria ili kuepuka figisu za wenyeji.


YANGA HESABU KALI

Hisia za wengi zimeelekezwa katika mchezo baina ya Yanga na Rivers United utakaochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa leo kuanzia saa 11 jioni.

Yanga inarudi katika mashindano hayo baada ya kuyakosa msimu uliomalizika ikiwa na kiu ya kurejea au kufanya vizuri zaidi ya 1998 ilipotinga hatua ya makundi.

Advertisement

Mwaka 2016 na 2018, Yanga ilitinga makundi ya klabu Afrika lakini ilikuwa kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

Wenyeji wanajivunia usajili wa nyota wenye uzoefu ambao wamewahi kushiriki hatua za juu za mashindano hayo kama Yannick Bangala, Heritier Makambo na Ducapel Moloko ambao wamekuwa wakifanya kazi ya ziada kukazia mzuka kambini ili waingie uwanjani kibabe.

Lakini pia wanaye kocha mjanja na fundi wa mbinu, Nasreddine Nabi ambaye ana historia nzuri ya mashindano ya kimataifa, akiwahi kutwaa taji la Shirikisho Afrika 2012 alipoiongoza AC Leopards ya Kongo. Pia amewahi kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2015 na hatua kama hiyo Kombe la Shirikisho Afrika 2011.

Pamoja na kuwakosa Djuma, Fiston Mayele na Khalid Aucho, Yanga itaingia ikiwa na wigo mpana wa kikosi kutokana na uwepo wa nyota akiwemo Makambo, Mukoko Tonombe na Shomary Kibwana wanaoweza kuziba mianya na amepania kwelikweli. Kocha Nabi kwa nyakati tofauti amekuwa akisisitiza wapo tayari kwa mchezo huo utakaochezeshwa na Hassan Mohamed Hagi kutoka Somalia atakayesaidiwa na Suleiman Bashir na Ali Mohamud Mahad huku refa wa akiba ni Ahmed Hassan Ahmed

“Wachezaji waliorudi kutoka timu za taifa wapo vizuri na nitawatumia, ambao watakosekana kwa sababu mbalimbali kuna mbadala wao watacheza nafasi hizo,” alisema.

Heritier Makambo anayetarajiwa kuachiwa msala wa mabao katika mchezo huo na wenzake wanaelezwa kujaa mzuka wa kutaka mechi ipigwe ili wamalize kazi mapema.

Kikosi cha Yanga katika mechi hiyo kinaweza kuundwa na Djigui Diarra, Shomary Kibwana, Adeyum Saleh, Bakari Mwamnyeto, Dickson Job, Mukoko Tonombe, Ducapel Moloko, Yannick Bangala, Heritier Makambo, Feisal Salum na Yacouba Songne.

Kwenye benchi wanaweza kuwepo Erick Johora, Paul Godfrey, Yusuph Athuman, Abdallah Shaibu, Deus Kaseke, Zawadi Mauya na Ditram Nchimbi.

Historia inaonyesha Yanga haijawahi kutamba mbele ya timu kutoka Nigeria ambapo mara mbili imekutana nazo, huku Yanga ikisonga hatua inayofuata. Yanga imecheza mechi nne dhidi ya timu za Nigeria kwenye klabu za Afrika ambapo kati ya hizo, imetoka sare mara mbili na kupoteza mechi mbili.

Advertisement