Yanga SC yapeleka mabadiliko yao serikalini

Aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu waYanga, Senzo Mazingisa.
Muktasari:
- Mchakato wa mabadiliko ya mfumo ndani ya klabu Yanga bado unaendelea na sasa hatua mpya ni kuwafuata viongozi wa serikali katika kutambulisha rasmi mabadiliko hayo.
Dar es Salaam. Mchakato wa mabadiliko ya mfumo ndani ya klabu Yanga bado unaendelea na sasa hatua mpya ni kuwafuata viongozi wa serikali katika kutambulisha rasmi mabadiliko hayo.
Mshauri wa mambo ya uongozi wa Yanga, Senzo Mazingisa alisema juzi kuwa kwasasa ripoti ya kutoka Hispania kwa wadau wao La Liga wanaowashauri katika mabadiliko hayo imeshatafsiriwa kutoka lugha ya kiingereza kuja kiswahili.
Senzo alisema baada ya kubadiliaha ripoti hiyo hatua inayofuata ni kuiwasilisha kwa kamati ya utendaji ya klabu hiyo ili nao waipitie vizuri maudhui ya ripoti hiyo.
Alisema baada ya hatua hiyo watakutana na viongozi wa serikali hususan wizara ya michezo ambapo watakutana nao kwa hatua ya awali kutambulisha dhamira yao ya kubadilisha muundo huo.
“Tukitoka kwa kamati ya utendaji sasa tutakwenda kwa viongozi wa serikali, Yanga tunaheshimu mamlaka ya nchi na huko tutakwenda kwa nia ya awali ya kujitambulisha lakini pia kutambulisha dhamira yetu ya mabadiliko,” alisema Senzo.
“Tutawaeleza kila kitu na tunakusudia kufanya kipi,tubadilishe mambo yapi naamini nao watatupa maangalizo yapi ya kuhakikisha tunayazingatia katika mchakato huu.
“Nasema hii itakuwa hatua ya awali kukutana na serikali kwasababu tutarudi tena baadaye kwao kuwapelekea na kuwashirikisha kwa kuwapa ripotio mbalimbali katika kila hatua ambayo tutakuwa tunafikia katika mchakato huu,ili tusije kukwama baadaye na kurudishwa nyuma,” aliongeza.
Senzo alieleza zaidi kwamba baada ya kutoka serikalini watakutana na viongozi wa matawi ya Yanga ikiwemo hatua ya kuzunguka nchi nzima kuhakikisha elimu husika inawafikia wanachama na mashabiki wao.