Yanga, Simba hii ni mechi muhimu kwao

Mechi za kwanza za hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu itachezwa mwishoni mwa wiki hii katika viwanja na miji tofauti barani Afrika.

Kwa hapa nyumbani Tanzania hapana shaka hisia zote zitaelekezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa ambao Ijumaa na Jumamosi utakuwa na mechi mbili za hatua hiyo ambazo zitahusisha Simba na Yanga zinazoiwakilisha nchi kwenye mashindano hayo.

Ijumaa, Machi 29, Simba itaikaribisha Al Ahly ya Misri na Jumamosi, Yanga itakuwa dimbani kucheza na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, mechi zote hizo zikichezwa kuanzia saa 3:00 usiku.

Ni mara ya nne kwa Simba kucheza hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika tangu muundo wa mashindano hayo ulipobadilika mwaka 2017.

Kwa Yanga, hii ni mara ya kwanza kwao kucheza hatua ya robo fainali ya mashindano hayo baada ya mabadiliko ya namna hiyo yaliyofanywa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf) miaka saba iliyopita.

Ushindi nyumbani lazima

Matokeo mazuri ambayo timu za Al Ahly zimekuwa zikiyapata katika viwanja vyao vya nyumbani kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, yanazilazimisha Simba na Yanga kuhakikisha zinapata ushindi ikibidi wa idadi kubwa ya mabao katika Uwanja wa Benjamin Mkapa ili zijiweke katika mazingira mazuri ya kutinga hatua ya nusu fainali.

Al Ahly hadi sasa ina rekodi ya kucheza mechi 11 mfululizo za Ligi ya Mabingwa Afrika nyumbani bila kupoteza ambapo mara ya mwisho kuangusha pointi tatu kwenye uwanja wa nyumbani ilikuwa ni Mei 30, 2022 ilipofungwa mabao 2-0 na Raja Casablanca.

Katika mechi hizo 16 mfululizo ambazo Ahly haijapoteza kwenye uwanja wa nyumbani, imeibuka na ushindi mara tisa na kutoka sare moja, ikifumania nyavu mara 24 na yenyewe imeruhusu mabao matatu tu.

Kwa upande wa Mamelodi Sundowns, wametimiza siku 1082 ambazo timu hiyo haijapoteza mechi yoyote ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo ilikuwa mwenyeji.

Tangu ilipofungwa mabao 2-0 nyumbani na CR Belouizdad, Aprili 9, 2021, Mamelodi haijapoteza tena mchezo wa mashindano hayo ikiwa Afrika Kusini ambapo katika mechi 16 zilizofuata, imeibuka na ushindi mara 12, ikitoka sare nne, imepachika mabao 34 na yenyewe nyavu zake zimetikiswa mara tisa.

Simba ukuta, Yanga ushambuliaji

Simba inaingia katika mechi dhidi ya Al Ahly ikijivunia safu bora ya ulinzi kwenye mashindano hayo msimu huu kuibeba ingawa itapaswa kufanya kazi ya ziada kuboresha safu yake ya ushambuliaji ili ipate mabao yanayoweza kuifanya isonge mbele.

Katika mechi sita za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, Simba imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili tu ikiwa ni wastani wa bao 0.3 huku safu yake ya ushambuliaji ikipachika mabao tisa sawa na wastani wa bao 1.5 kwa mechi ingawa mabao hayo tisa imeyapata katika mechi tatu huku michezo mitatu ikimaliza bila kufunga bao.

Yanga inaikabili Mamelodi ikitegemea zaidi makali ya safu yake ya ushambuliaji ambayo imeonekana kuwa tishio katika hatua ya makundi ingawa wasiwasi upo katika safu ya ulinzi iliyoonyesha kusuasua kwenye hatua iliyopita.

Katika mechi sita za hatua ya makundi ya mashindano hayo, Yanga imepachika mabao tisa ikiwa ni wastani wa bao 1.5 kwa mchezo na haikupata bao katika mechi mbili tu huku safu yake ya ulinzi ikiruhusu mabao sita sawa na wastani wa bao moja kwa kila mchezo.

Gamondi, Benchikha wabeba matumaini

Ubora na uwezo wa kimbinu na upangaji wa timu wa makocha Miguel Gamondi wa Yanga na Abdelhak Benchikha wa Simba vinategemewa kwa kiasi kikubwa kuwa chachu kwa timu hizo kupata ushindi na kusonga mbele dhidi ya Mamelodi Sundowns na Al Ahly.

Mfumo ambao Miguel Gamondi amekuwa akipendelea kuutumia mara kwa mara ni ule wa 4-2-3-1, huku akiwategemea zaidi viungo wake katika kuzalisha na kufunga mabao.

Chini ya Gamondi, Yanga imekuwa ikitegemea soka la kasi linaloambatana na pasi za haraka haraka katika ujenzi wa mashambulizi, ambalo limekuwa mwiba kwa timu pinzani.

Katika aina hiyo ya mfumo, Gamondi ametoa uhuru mkubwa kwa kiungo mmoja anayecheza mbele ya mstari wa mabeki, kusogea mbele mara kwa mara na kusaidia mashambulizi na jukumu hili mara kwa mara limekuwa likifanywa na Mudathir Yahya, huku kiungo mmoja wa ulinzi akibaki ili kutengeneza balansi ambaye mara nyingi huwa Khalid Aucho ambaye bado hajafahamika kama atakuwepo kwenye mchezo huu.

Kwa upande wa Simba, kocha Benchikha amekuwa akipendelea kutumia mfumo wa 4-3-3 akiwategemea zaidi mshambuliaji wake mmoja wa pembeni na kiungo wa ushambuliaji katika kutengeneza na kufunga mabao.

Benchikha ni muumini wa soka la kasi na pasi chache katika ujenzi wa mashambulizi kwa lengo la kuwanyima fursa wapinzani kujipanga pindi Simba inapokuwa na mpira.

Viungo wake wawili wa chini ambao mara nyingi huwa Babacar Sarr na Fabrice Ngoma wamekuwa wakitegemewa zaidi katika kuipa nguvu aina hiyo ya kiuchezaji kutokana na uwezo wao wa kupiga pasi ndefu kwenda ama kwa Clatous Chama na Saido Ntibazonkiza wanaocheza kwa kubadilisha katika nafasi ya kiungo mshambuliaji na mshambuliaji wa Pembeni.

Fedha ndio kila kitu

Ni mechi ambazo zinaweza kuwa fursa muhimu kwa wachezaji wa Simba na Yanga kupata kiasi kikubwa cha fedha ikiwa watawezesha timu zao kuibuka na ushindi lakini pia hata klabu zenyewe kuoga noti kwa namna tofauti.

Kwa wachezaji, wanaweza kupata fedha zitokazo kwa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ambaye anatoa kiasi cha Shilingi 10 milioni kwa kila bao ambalo linafungwa ama na Yanga au Simba kwenye hatua hiyo na iwapo zitasonga mbele zaidi ya hapo.

Kwa upande mwingine, kama timu hizo zitafanikiwa kuvuka robo fainali na kutinga nusu fainali, kila moja itajihakikishia kiasi cha Dola 1.2 milioni (Sh 3 bilioni) ambazo ni fedha zitolewazo na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf) kwa kila timu ambayo itakomea katika hatua hiyo.

Ikumbukwe kwa kutinga tu hatua ya robo fainali, Simba na Yanga kila moja tayari ina uhakika wa kuvuna kiasi cha Dola 900,000 (Sh 2.3 bilioni) kutoka Caf.

Lakini pia kwa kusonga mbele, timu zinajihakikishia kuvuna fedha kupitia mapato ya mlangoni kutoka kwa mashabiki ambao watakwenda uwanjani kutazama mechi ya hatua ya nusu fainali au zaidi ya hapo