Yanga, Simba zafunika Dabi tano kali duniani

Muktasari:

  • Dabi ni mchezo unaohusisha timu zinazotoka eneo moja au zenye historia ya mafanikio au zenye upinzani kutokana na kumbukumbu fulani ya nyuma.

Uzito wa mechi ya watani wa jadi wa Kariakoo leo baina ya Yanga na Simba kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 11 jioni umefanya Dabi tano zinazochezwa mwishoni mwa wiki hii katika maeneo tofauti duniani zisiwe mjadala mkubwa hapa Tanzania.

Hali hiyo inaonekana ingekuwa tofauti iwapo miamba hiyo miwili ya soka nchini isingekutana leo katika mechi hiyo ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara.

Dabi ya kwanza ambayo imefunikwa na Yanga na Simba mwishoni mwa wiki hii ni ile ya Kenya maarufu kama Mashemeji inayozikutanisha Gor Mahia na AFC Leopards ambayo imepangwa kuchezwa kesho Jumapili kuanzia saa 9:00 alasiri katika Uwanja wa Nyayo jijini Nairobi.

Timu hizo hasimu zinakutana huku Gor Mahia ikiongoza msimamo wa Ligi Kuu Kenya ikiwa na pointi  54 wakati Leopards ipo nafasi ya nane ikiwa na pointi 38 na ikumbukwe katika mchezo wa kwanza baina yao, Gor Mahia ilipata ushindi wa mabao 2-0.

Ukiondoa hiyo, Hispania kuna Dabi ya kibabe inayokutanisha miamba miwili ya soka nchini humo, Real Madrid na Barcelona itakayochezwa kesho Jumapili kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu kuanzia saa 4 usiku.

Katika mchezo wa kwanza ambao Barcelona ilikuwa mwenyeji uliochezwa kwenye Uwanja wa Nou Camp, Oktoba 28 mwaka jana, Real Madrid iliibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Miamba hiyo miwili inakutana katika kipindi ambacho Real Madrid inaongoza ikiwa na pointi 78 na Barcelona inashika nafasi ya pili ikiwa imekusanya pointi 70.
Huko Rwanda leo kutakuwa na Dabi ya Jiji la Kigali baina ya vinara wa Ligi hiyo APR dhidi ya Kiyovu ambayo itachezwa kwenye Uwanja wa Pele jijini Kigali kuanzia saa 10 jioni.

APR yenye pointi 60 inahitaji ushindi au sare ya aina yoyote leo ili itwae ubingwa na kuiacha kwenye mataa Rayon inayoshika nafasi ya pili ikiwa na pointi 48.

Nchini Brazil leo kuna Dabi kali ya jiji la Rio de Janeiro ambayo itazikutanisha Fluminense na Vasco Da Gama katika Uwanja wa Maracana kuanzia saa 4 usiku.
Dabi hiyo inajulikana kwa jina maarufu la 'Classico dos Gigantes' ikimaanisha Dabi ya Wakubwa.

Huko Zambia nako kuna Dabi ya jiji la Kitwe leo hii kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa ambayo itazikutanisha Power Dynamos na Nkana FC.
Ukiondoa dabi hizo, kuna mechi nyingine kali ambazo zitachezwa leo na kesho katika maeneo tofauti duniani.

England leo kuna mechi ya nusu fainali ya Kombe la FA baina ya Man City na Chelsea itakayochezwa kwenye Uwanja wa Wembley kuanzia saa 1:15 usiku.

Kuna mechi mbili za hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo ya kwanza itakuwa jijini Lubumbashi, DR Congo kati ya TP Mazembe na Al Ahly itakayochezwa kuanzia saa 10 jioni na kuanzia saa 4 usiku, Esperance ya Tunisia itaikaribisha Mamelodi Sundowns.