Yanga ubingwa, bado sana

Sunday March 07 2021
full time pic
By Khatimu Naheka

Yanga imezidi kujiwekea mazingira magumu ya kutwaa ubingwa msimu huu baada ya kuendelea kupata matokeo yasiyoridhisha  kwenye Ligi Kuu Bara.

Timu hiyo leo wametoa sare ya bao 1-1 dhidi ya Polisi Tanzania kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha na hivyo kufikisha sare nne kati ya mechi sita ilizocheza mpaka sasa kwenye mzunguko wa pili huku wakishinda mchezo mmoja na kupoteza mmoja.

Yanga inayonolewa na mrundi Cedrick Kaze ndiyo ilianza kupata bao dakika ya  42 lililofungwa na Fiston Abdulrazak kwa kisigino kabla ya Polisi Tanzania kusawazishiwa dakika ya 90 kupitia kwa Pius Buswita.

Fiston ambaye amefunga bao lake la kwanza msimu huu tangu ajiunge na timu hiyo, alifunga bao hilo kwa kisigino akimalizia krosi Tuisila Kisinda wakati bao la Piolisi lilifungwa kwa kichwa na Buswita aliyeunganisha mpira wa  adhabu uliopigwa na Deusdedit Cosmas

Tangu kuanza kwa mzunguko wa pili yanga imecheza ugenini dhidi ya Prisons na kutoka sare ya bao 1-1, Mbeya City 1-1, Kagera Sugar 3-3, ikashinda dhidi ya Mtibwa 1- 0 na kufungwa na Coastal Union mabao 2-1.

Yanga imefikisha alama 50 baada ya michezo 23 wakiwa kileleni huku wakifutiwa na watani zao wa jadi Simba wenye alama 45  lakini wakiwa na  michezo minne mkononi.

Advertisement

MPIRA ULIVYOKUWA

Dakika ya sita Yanga walitengeneza shambulizi zuri baada ya Tuisila Kisinda kugongeana vyema na beki wa kulia,Kibwana Shomari ambaye alipiga  krosu nzuri lakini Haruna Niyonzima alishindwa kufunga na  kupaisha.
Polisi walijibu mapigo dakika ya 11  kupitia kwa Seif Karihe ambaye alimtengenezea nafasi nzuri mshambuliaji Daruwesh Saliboko lakini shuti lake lilipaa juu kidogo ya lango.
Dakika ya 20 Kisinda alifanya kazi kubwa baada ya kuwatoka mabeki wa Polisi lakini krosi yake ikadhibitiwa na Kelvin Yondani na kuwa kona iloyokosa madhara.
Dakika ya 26 Yanga walitengeneza shambulizi kali Kisinda tena aliwatoka mabeki kabla ya kuachia krosi ambayo hata hivyo ilishindwa kumaliziwa vizuri na  Haruna Niyonzima. 

Kipindi cha pili Yanga walirudi na nguvu dakika  na  dakika ya 47 Ditram Nchimbi alifanya jaribio zuri lakini shuti lake kali lilitoka nje kidogo ya lango, Polisi waliendelea kushambulia mara kwa mara na dakika ya 90 walipata bao kupitia kwa Buswita.

Advertisement