Yanga yaendeleza ubabe kwa Simba, yatwaa Ngao ya Jamii
Muktasari:
- Simba imekubali kipigo kwa mara ya sita mfululizo katika michezo waliyokutana na mpinzani wake Yanga katika mashindano tofauti.
Dar es Salaam. Yanga imeendeleza ubabe wake dhidi ya Simba baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 katika fainali ya Ngao ya Jamii iliyochezwa leo Jumanne Septemba 16, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Shujaa wa mchezo huo alikuwa Pacome Zouzoua, aliyefumania nyavu dakika ya 54 akimalizia mpira uliotemwa na kipa Mousa Camara na kuipa Yanga ushindi wa sita mfululizo dhidi ya Simba katika michezo yote ya mashindano waliyokutana.
Katika dakika 45 za kwanza, timu zote zilishambuliana kwa zamu lakini zikashindwa kuzitumia nafasi walizopata. Prince Dube alikosa nafasi ya wazi kwa Yanga baada ya kuunganisha mpira kwa bega na kumrahisishia kazi kipa Mousa Camara kuokoa.
Simba nao walipata nafasi mbili kupitia Kibu Denis dakika ya 27 na Shomari Kapombe dakika ya 40, lakini kipa Djigui Diarra aliweka uhai kwa kuokoa mashuti hayo.
Dakika ya 25 Simba ilipata pigo baada ya beki wake Abdulrazack Hamza kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na Chamoue Karaboue.
Kipindi cha pili Yanga iliongeza kasi baada ya kumuingiza Mamadou Doumbia kwenye nafasi ya Mudathir Yahya, hali iliyozalisha bao la Zouzoua dakika tisa tu baada ya kuanza kwa kipindi hicho.
Simba walijaribu kupeleka mashambulizi katika lango la Yanga kupitia washambuliaji wake Steven Mukwala na Jean Ahoua, lakini walinzi wa mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara wakiongozwa na Dickson Job walikuwa imara kuzuia hatari.
Mabadiliko yaliyofanywa na makocha wa timu zote mbili hayakubadili matokeo, Yanga ikiendelea kulinda ushindi wake hadi mwisho wa mchezo huo.
Yanga ilianza na kikosi kilichoundwa na Djigui Diarra, Israel Mwenda, Chadrack Boka, Dickson Job, Ibrahim Bacca, Aziz Andabwile, Maxi Nzengeli, Duke Abuya, Prince Dube, Mudathir Yahya na Pacome Zouzoua.
Simba ilianza na Mousa Camara, Shomari Kapombe, Naby Camara, Rushine De Reuck, Abdulrazack Hamza, Allasane Kante, Kibu Denis, Yusuph Kagoma, Steven Mukwala, Jean Ahoua na Ellie Mpanzu.