Yanga yaendeleza umwamba Ligi Kuu Bara

Muktasari:

  • Yanga imepoteza mchezo mmoja tu wa Ligi Kuu msimu huu ikiwa imekusanya pointi 37 kwenye michezo 14, huku Mashujaa ikikusanya pointi tisa tu

Dar es Salaam. Yanga imeruhusu bao la saba msimu huu baada ya kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mashujaa kwenye Uwanja wa Chamazi.

Huu ni muendelezo bora wa Yanga kwenye Ligi Kuu Bara, ikiwa imepoteza mchezo mmoja baada ya kucheza michezo 14 kwenye ligi hiyo hadi sasa msimu huu.

Yanga imeendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa kukusanya pointi 37, ikiwa imejiweka kwenye mazingira mazuri ya kutetea ubingwa wa ligi hiyo.

Yanga ilianza kujipatia bao kupitia kwa Maxi Nzegeli katika dakika ya 45, ambaye alikuwa hajafunga kwenye michezo 10 mfululizo, tangu alipofanya hivyo kwenye mchezo wa Dabi dhidi ya Simba mwaka jana. Sasa amefikisha mabao nane sawa na Fei Toto.
Mashujaa ambayo ilionyesha kiwango cha juu kwenye mchezo huu ilisawazisha kupitia kwa Emmanuel Mtumbuka katika dakika ya 66, likiwa ni bao lao la nne msimu huu wanafunga ugenini, ikiwa imecheza michezo 14 na kukusanya pointi tisa tu.

Kiungo Mudathir Yahaya, ambaye amekuwa akitambulishwa kama mfalme wa Chamazi, aliendelea kuonyesha umwamba wake baada ya kuifungia Yanga bao la ushindi katika dakika ya 86, akimalizia krosi ya Kennedy Musonda, likiwa ni bao lake la pili la ushindi anafunga kwenye michezo miwili mfululizo baada ya kufanya hivyo dakika za mwisho pia kwenye mechi dhidi ya Dodoma Jiji.

Ushindi huu unaifanya Yanga isiwaze sana matokeo ya mchezo wa Simba dhidi ya Azam kwenye Uwanja wa CCM Kirumba kesho kwa kuwa hakuna atakayeitoa kileleni.