Yanga yaipiga mkwara wa mwisho Belouizdad
Muktasari:
- Timu mbili zitakazomaliza katika nafasi mbili za juu katika kila kundi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika zitafuzu hatua ya robo fainali.
Dar es Salaam. Muda mfupi kabla ya Yanga kuikaribisha CR Belouizdad katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, Ofisa habari wa timu hiyo, Ally Kamwe amewahakikishia mashabiki wao kuwa watapa furaha kwa kubaki ushindi nyumbani leo.
Mchezo huo ni wa raundi ya tano ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambao Yanga inahitajika kupata ushindi ili iweke hai matumaini yake ya kutinga hatua ya robo fainali.
Ushindi katika mechi hiyo utaifanya Yanga ifikishe pointi nane na hivyo kuhitaji sare tu katika mechi ya mwisho dhidi ya Al Ahly ugenini iweze kusonga mbele na kuingia hatua inayofuata.
Kamwe amesema kuwa mashabiki wa Yanga wajiandae kupata furaha na timu imejiandaa vyema kuhakikisha hilo linatimia.
"Mara ya mwisho Yanga yetu kutupa raha mbele ya Waarabu, ilikuwa mbele ya macho palepale Algeria. Leo wamekuja kwetu Benjamin Mkapa, moto mkali sana utawawakia leo," amesema Ally Kamwe.
Yanga inashika nafasi ya tatu katika msimamo wa kundi D ikiwa na pointi tano huku vinara wakiwa ni Al Ahly ambayo ina pointi tisa wakati CR Belouizdad inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi tano.
Timu inayoshika mkia katika kundi hilo ni Medeama ambayo imekusanya pointi nne katika mechi tano ilizocheza hadi sasa.