Yanga yalipa kisasi, Mayele bado moja

Muktasari:

  • Yanga imelipa kisasi baada ya kuifunga Ihefu bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu NBC uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Dar es Salaam. Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu NBC Yanga, wameendeleza moto wake baada ya kupata ushindi kwenye mchezo wa saba mfululizo tangu ilivyopoteza mara ya mwisho dhidi Ihefu.

Yanga imepata ushindi wa bao 1-0 kwenye mechi ya leo iliyochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa na bao pekee lilifungwa na Fiston Mayele na kuendelea kujiwekea vizuri kwenye mbio za ufungaji bora msimu huu.

Baada ya ushindi huo Yanga inasalia kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa imecheza mechi 20 na kufikisha pointi 53, wakati Ihefu ikisalia nafasi ya 13, ikiwa imecheza mechi sawia na kufikisha pointi 20.

Mechi ya leo hadi kipindi cha kwanza kinamalizika Yanga ilikuwa inamiliki mpira kwa asilia 54, wakati Ihefu asilimia 46.

Mechi ya mzunguko wa kwanza ilichezwa Mbeya Uwanja wa Mbalari Estate Ihefu ikiwa nyumbani ilipata ushindi wa mabao 2-1, dhidi ya mabingwa watetezi Yanga.

Ihefu mabao yao kwenye mechi hii yalifungwa na Lenny Kisu na Never Tigere wakati lile la Yanga lilifungwa na Yanick Bangala aliyekosekana kwenye mechi ya leo.

Mechi hiyo ilichezwa Novemba 29, 2022 Ihefu ilitibua rekodi ya Yanga kutokucheza mechi 49 pasina kufungwa mchezo wowote.

Yanga baada ya mchezo huo kupoteza ilicheza mechi sita za ligi na kushinda zote hadi unakutana tena na Ihefu leo (Jumatatu), Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Ihefu wao baada ya kucheza na Yanga na kupata ushindi uliyokwenda kutibua rekodi hiyo ilicheza mechezo mingine mitano kabla ya kukutana na Yanga tena imeshinda mitatu na kufungwa miwili.

Kumbukumbu zinaonyesha msimu wa kwanza Ihefu kucheza Ligi Kuu Bara ilikuwa 2020-21, mechi ya kwanza dhidi ya Yanga ilipoteza kwa kufungwa mabao 3-0.

Mabao kwenye mchezo huo ilichezwa Desemba 23, 2020 yalifungwa na Deus Kaseke, Yacouba Sogne na Feisal Salum ambao wote hawapo kwenye kikosi cha Yanga kwa sasa.

Mechi ya mzunguko wa pili Yanga ilishinda mabao 2-0, mabao yote yalifungwa na Feisal Salum wakati msimu huu mchezo wa kwanza uliisha kwa Ihefu kuwa wababe.

Kwenye kikosi cha kwanza Ihefu kulikuwa na wachezaji wawili wapya waliosajili kwenye dirisha dogo la usajili lililofungwa jana beki wa kushoto, Yahya Mbegu na mshambuliji Adam Adam.

Dakika 62, straika mpya wa Yanga Kennedy Musonda aliingia kuchukua nafasi ya Farid Muda na aliichezea timu hiyo kwenye mechi ya kwanza ya kimashindano akitokea Power Dynamos ya Zambia.

Dakika 64, Fiston Mayele alifunga bao la kwanza kwenye mchezo huo baada ya uzembe wa kipa wa Ihefu, Fikirini Bakari kushindwa kuhokoa mpira kwa usahihi.

Bao hilo linakuwa la 15, kwa Mayele msimu huu na kujiweka vizuri kwenye mbio za ufungaji bora wa ligi akiwa kinara.

Msimu uliopita Mayele alimaliza nafasi ya pili kwenye mbio za ufungaji bora akiwa na mabao 16, kutokana na kufunga bao la kwanza anakuwa amebakisha bao moja ili kufikia rekodi yake ya msimu uliopita.

Msimu uliopita Mayele alishindwa kutwaa tuzo ya mfungaji bora kutokana na kinara kuibuka, George Mpole aliyekuwa anacheza Geita Gold na sasa ametimkia FC Lupopo ya DR Congo kumaliza msimu na mabao 17.