Prime
Yanga yamkabidhi Zimbwe kwa Kibwana Shomari
Muktasari:
- Zimbwe amejiunga na Yanga kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Simba ambayo kaitumikia kwa miaka mitatu
Dar es Salaam. Ni wazi kwamba beki Mohamed Hussein ‘Zimbwe’ ataitumikia Yanga msimu ujao baada ya kujiunga nayo akitokea Simba.
Mwananchi Digital inafahamu kuwa Yanga imeshafunga hesabu kwa beki huyo na kilichobaki ni kumtambulisha rasmi jambo ambalo linaweza kufanyika siku yoyote kuanzia leo.
Hata hivyo wakati Yanga ikijiandaa kumtambulisha Zimbwe, timu hiyo imepanga kumkutanisha na beki wake mwingine Kibwana Shomari ili kuliweka sawa jambo moja.
Jambo hilo linahusu jezi namba 15 ambayo inavaliwa na Kibwana Shomari hivi sasa huku Zimbwe akitamani kuivaa katika msimu ujao akiwa ndani ya Yanga.
Zimbwe akiwa ndani ya Simba alikuwa anatumia jezi yenye namba 15 na baada ya kujiunga na Yanga, inaripotiwa anatamani kuendelea kuitumia lakini kwa sasa inavaliwa na Shomari.
Kutokana na hilo, Yanga imeliacha suala hilo kwa wachezaji wenyewe ikiamini watafikia muafaka jambo ambalo litafanyika hivi karibuni.
“Suala la namba ya jezi ni la wachezaji wenyewe hivyo wao watakutana na kuafikiana. Zimbwe ametamani kuendelea kutumia jezi namba 15 lakini kwa sasa inatumiwa na Kibwana hivyo kiungwana wanatakiwa wenyewe wakubaliane,” kilifichua chanzo ndani ya Yanga.
Kama hilo litafanyika, halitokuwa geni ndani ya Yanga kwani iliwahi kutokea pia kwa wachezaji Farid Muda na Clatous Chama.
Wakati Chama akijiunga na Yanga akitokea Simba mwaka jana, aliomba kuendelea kuitumia jezi namba 17 ambayo ndani ya Yanga ilikuwa inatumiwa na Farid Musa.
Wachezaji hao walikutanishwa na kufanya mazungumzo wenyewe ambapo Farid Musa alikubali kumuachia Chama jezi namba 17 ambayo alikuwa anaitumia kwa waajiri wake wa zamani.
Hata hivyo, Chama aliitumia jezi namba 17 kwa msimu mmoja tu ndani ya Yanga kwani tayari ameshaachana nayo baada ya kumalizika kwa msimu wa 2024/2025.