Yanga yatenga bajeti ya Sh24.5 bilioni msimu ujao

Klabu ya Yanga imetangaza bajeti ya timu hiyo ya Sh 24.5 bilioni katika msimu ujao wa mashindano mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.

Akizungumza katika Mkutano Mkuu Wa Klabu hiyo, Mkurugenzi wa Fedha, Sabri Sadick, amesema ongezeko hilo ni kubwa zaidi ya msimu uliopita ila kukidhi mahitaji ya kikosi hicho.

"Yanga imetenga bajeti kubwa kwa sababu lengo ni kuona timu yetu inafanya vizuri zaidi katika mashindano mbalimbali ya ndani na nje ya nchi," amesema.

Aidha Sabri aliongeza, mapato ya timu hiyo msimu uliopita yalikuwa ni Sh21 bilioni huku matumizi yakiwa ni Sh22 bilioni ambayo ni sawa na klabu hiyo kuwa na upungufu wa Sh1 bilioni kwa msimu.

"Fedha hizo zimetokana na udhamini, kiingilio cha mlangoni, ada za wanachama, zawadi ya ushindi, mauzo ya wachezaji, faida ya jezi na mapato mengine," amesema Sabri.

Ongezeko hilo la bajeti kwa msimu ujao ni tofauti na ya msimu uliopita kwani klabu hiyo ilikuwa imetenga kiasi cha Sh20.8 bilioni katika Mkutano Mkuu uliofanyika Juni 24, mwaka jana.