Yanga yatinga kibabe robo fainali CAFCC
Muktasari:
- Yanga imeweka rekodi ya kutinga robo fainali kwa mara ya kwanza katika Ligi ya Mabingwa baada ya kuifunga Belouazidad mabao 4-0.
Dar es Salaam. Yanga imeweka rekodi ya kufuzu robo fainali ya mashindano ya klabu Afrika mara mbili mfululizo pasipo kusubiria mechi ya mwisho ya kundi huku ikiungana na timu nyingine tano ambazo zimeingia hatua hiyo baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya CR Belouizdad kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa leo.
Msimu uliopita, Yanga ilitinga robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kucheza mechi tano tu na mechi ya sita ya kundi ikawa ya kukamilisha ratiba na kuamua timu ipi ingeongoza kundi.
Hilo limejirudia msimu huu ambapo Yanga imetinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kucheza mechi tano huku ikibakiwa na mechi moja mkononi ambayo ni dhidi ya Al Ahly itakayochezwa Cairo, Misri, Machi Mosi.
Katika mchezo wa leo, mabao manne ya Yanga yaliyopachikwa na Mudathir Yahya, Stephane Aziz Ki, Kennedy Musonda na Joseph Guede yalitosha kuwavusha kwenda hatua inayofuata hata ikipoteza dhidi ya Al Ahly, itasonga mbele kwa vile itabebwa na kigezo cha kupata matokeo mazuri katika mechi mbili kati yake na Belouizdad.
Belouazidad inaweza kufikisha pointi nane, lakini kwa kuwa kanuni za CAF zinaangalia matokeo ya timu mbili zilipokutana yalikuwaje, basi Yanga itakuwa juu kwa wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Kwa kufuzu hatua ya robo fainali, Yanga imejihakikishia kiasi cha Dola 900,000 (Sh2.3 bilioni) ambacho Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrrika (CAF) linatoa kwa kila timu inayoishia hatua hiyo.
Yanga imekuwa timu ya sita kutinga hatua hiyo ambapo sasa zimebaki timu mbili tu ambazo zitapatikana katika raundi ya mwisho itakayochezwa mwishoni mwa wiki ijayo.
Timu sita ambazo zimefuzu robo fainali ni Yanga, Al Ahly, Mamelodi Sundowns, TP Mazembe, ASEC Mimosas na Petro Luanda.