Yanga yavunja mwiko Majaliwa...Yazikataa Azam, Simba

Mshambuliaji wa Yanga akiwatoka mabeki wa Namungo katika mchezo ligi uliochezwa uwanja wa Majaliwa, Lindi. Picha| Loveness Bernard.

Muktasari:

  • YANGA imemaliza mzunguko wa kwanza kibabe ikisalia kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu NBC ikifikisha pointi 38 baada kuifunga Namungo mabao 2-0.

USHINDI wa 2-0 uliopata Yanga dhidi ya Namungo unaifanya timu hiyo ivunje mwiko wa kutopata ushindi katika uwanja wa Majaliwa.

Mabao ya Yanick Bangala dakika ya 40 na Tuisila Kisinda dakika ya 82 yametosha kuipa Yanga ipate ushindi wa kwanza kwenye Ligi Kuu katika uwanja huo.

Namungo na Yanga kwenye mechi sita za mwisho za Ligi Kuu zimecheza mechi tatu kwenye uwanja huo na zote zilimalizika kwa sare.

Wakati huo kwenye mechi tatu walizocheza katika uwanja wa Mkapa, walitoka sare mbili na Yanga kushinda mchezo mmoja.

Mshambuliaji wa Yanga, Tuisila Kisinda amefunga bao lake la kwanza katika mchezo wa Ligi Kuu tangu arejee katika kikosi hicho akitoka kwa mkopo RS Berkane ya Morocco.

Matokeo hayo yanaifanya Yanga iendelee kukaa kileleni ikiwa na pointi 38, Azam FC 35, Simba 34 , Singida Big Stars 27 na Geita Gold ikifunga tano bora kwa pointi 22 baada ya timu zote kucheza mechi 15.