Yanga yawawekea kikao Kaze, Simba

Thursday September 23 2021
kikaopicc

Cedric Kaze

By Imani Makongoro

Dar es Salaam. Homa ya Kariakoo Derby imeanza kupanda, kwani leo mabosi wa Yanga watafanya kikao maalumu chenye ajenda mbili tu, kuhusu Simba na hatma ya kocha Cedric Kaze anayerejeshwa Jangwani.

Wikiendi hii Yanga itavaana na Simba katika mechi ya Ngao ya Jamii ya kuzindua msimu mpya wa Ligi Kuu Bara, mchezo utakaopigwa kuanzia saa 11:00 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku ikiwa inajiandaa kumpokea Kaze ili kuja kumsaidizi Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi kikosini.

Mabosi wa Jangwani wamegawanyika juu ya ujio wa Kaze ambaye baadhi ya viongozi wanataka arejee Yanga, lakini safari hii akiwa kocha msaidizi na wengine wanapinga wakihoji sababu za kumrejesha wakati walishaachana naye alipowahi kuwa kocha mkuu.

Baada ya kikao hicho, Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo itakutana na mdhamini wao GSM ambaye pia itakuwa na kikao  kisha muda huo wote wataelekea kambini kuzungumza na wachezaji ili kuwaweka sawa kabla ya mechi ya Jumamosi.

“Kitakuwa ni kikao ambacho kitamjadili kwa mara nyingine kocha Kaze ambaye ujio wake ni kama umeugawa uongozi, wapo wanaotaka arudi na wengine hawamtaki, lakini kikubwa ni kuweka mikakati ya kuelekea kwenye mechi ya Jumamosi, ambayo Simba watake wasitake tutawafunga,” alisema mmoja wa viongozi wa juu wa Yanga ambaye aliomba hifadhi ya jina.

Alisema uongozi wote na mdhamini wao watafanya kikao maalumu na wachezaji wakati wa chakula cha mchana hii leo na baadaye jioni watashuhudia mazoezi ya timu hiyo ambayo ni ya mwisho mwisho kabla ya mechi na Simba Jumamosi ya Ngao ya Jamii.

Advertisement

“Tunachokiamini ni kwamba Simba tunawapiga na hawatusumbui kwa lolote,” alisema kiongozi huyo ambaye alibainisha kwamba kikao cha leo pia kitakuwa cha kuwaeleza wachezaji motisha gani uongozi utawapa wakiifunga Simba,” alisema.

Naye Rais wa Simba, Murtaza Mangungu alisema katika mechi ambayo haiwapi presha ni ya Jumamosi dhidi ya Yanga.

“Hawawezi kutufunga kwa vyovyote vile, mechi ni yetu na tunawachapa kwa mara nyingine,” alisema Mangungu jana kwa kujiamini akisisitiza, mechi hiyo ni ya kawaida kwao kama ambavyo wanacheza na timu nyingine.

“Huwezi kumdharau mpinzani wako, ila tunaamini Yanga haitufungi,” alisisitiza Mangungu.

Advertisement