Zidane atambulishwa rasmi Ufaransa, kuanza na Uturuki
Muktasari:
- Zidane anarejea katika ukocha baada ya kuwa nje kwa miaka mitano tangu alipoachana na Real Madrid mwaka 2021.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Ufaransa (FFF) leo, Jumanne, Julai 28, 2026 limemtambulisha rasmi Zinedine Zidane kuwa Kocha Mkuu wa timu yao ya taifa.
Zidane mwenye umri wa miaka 54, amesaini mkataba wa miaka minne wa kuinoa Ufaransa akirithi mikoba ya mchezaji mwenzake wa zamani wa Juventus na Ufaransa, Didier Deschamps.
Deschamps aliachana na Ufaransa baada ya mechi ya kuwania mshindi wa tatu katika Kombe la Dunia 2026 dhidi ya England ambayo Ufaransa ilifungwa mabao 6-4.
Zidane anarejea uwanjani kwa mara ya kwanza baada ya kuwa nje ya ukocha kwa miaka mitano tangu alipoacha kuinoa Real Madrid mwaka 2021.
Rais wa FFF, Phillipe Diallo amesema kuwa walianza kufanya mazungumzo na Zidane tangu Februari 2025.
“Hii ni nyakati ya kipekee. Kwa sababu ya mtu aliyesimama baada yangu. Zinedine ni miongoni mwa magwiji wa soka la Ufaransa na kwa miaka mingi amesema miongoni mwa ndoto zake ni kuinoa timu ya taifa ya Ufaransa.
“Napenda kumshukuru Didier Deschamps na wasaidizi wake kwa kazi yao. Kwa miaka 14, ameiongoza timu ya Ufaransa kuwa juu,” amesema Diallo.
Katika miaka yake minne, Zidane anategemewa aiongoze Ufaransa katika mashindano ya UEFA Nations League mwakani, Kombe la Euro mwaka 2028 na Kombe la Dunia 2030.
Mchezo wa kwanza kwa Zidane akiwa Kocha wa Ufaransa, utakuwa dhidi ya Uturuki, Septemba 25, 2026 katika mashindano ya Nations League.