Benki Kuu ya Tanzania ilivyoanzishwa

Benki Kuu ya Tanzania ilivyoanzishwa

Muktasari:

  • Mwalimu Julius Nyerere kamwe hakuficha hisia zake kwa kile alichokutana nacho kuhusu uanzishwaji wa benki hii kwani, aliwaza kiwe kitu kikubwa zaidi.

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesimamia fedha na uchumi kwa nchi kwa miaka 55 sasa. Tangu ilipoanza shughuli zake Juni 14, 1966 BoT imeisaidia nchi kuweka sawa mipango yake kuelekea uchumi unaoongozwa na sekta binafsi, kwa kuanzia usimamizi wa benki kadhaa na taasisi za kifedha kisha kusimamia mashirika mengi zaidi.

Kwa mujibu wachambuzi, licha ya mabadiliko makubwa nchini BoT ilikusudiwa kuwa mbadala wa muda tu kwa matarajio kwamba baada ya kuundwa kwa Serikali ya Shirikisho la Afrika Mashariki ingeundwa na benki kuu ya shirikisho hilo.

Kuanzia Tanganyika ilipopata Uhuru Desemba 1961 hadi Juni 1966 mahitaji ya fedha na sarafu ya Tanganyika yalikuwa yakitolewa na Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki (EACB).

Tanganyika, na baadaye Tanzania ilibaki katika bodi ya sarafu kwa matarajio kwamba Kenya na Uganda zingekubaliana na pendekezo la Mwalimu Julius Nyerere la kuanzisha Shirikisho la Afrika Mashariki na mwishowe kuunda Serikali ya shirikisho hilo.

Lakini, wakati nchi hizo mbili ziliposhindwa kujibu pendekezo la Mwalimu, Tanzania iliamua kuunda benki kuu yake. Kenya na Uganda zilifuata mfano huo na kuunda benki kuu zao mwaka huo huo.

Alipokuwa akiizindua benki hiyo Mwalimu Nyerere alisema kuanzishwa kwa benki hiyo haimaanishi kuwa Tanzania ilikuwa inafunga mlango wa Umoja wa Afrika Mashariki.

Alisema: “Ikiwa wakati wowote katika siku za usoni washirika wetu katika mpangilio wa zamani wa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki wako tayari kuungana kisiasa katika shirikisho nasi, Benki Kuu na sarafu tunayoizindua leo itaundwa upya kuzingatia mahitaji ya shirikisho kama hilo. Yote yatafanywa na benki kuu ya shirikisho, hitaji la benki kuu na sarafu litakuwapo siku zote.”

Mapema katika hotuba yake Mwalimu Nyerere alisema hakufurahia kabisa Benki iliyozinduliwa siku hiyo haikuwa benki kuu ya shirikisho. Alisema: “Nina hisia za majuto na kukata tamaa kwamba benki kuu si ya shirikisho. Tungekuwa na furaha kubwa katika mioyo yetu kama tungeona Rais wa shirikisho ndiye aliyesimama kuzindua benki kuu ya shirikisho na lazima niseme wazi kabisa kwamba ningekuwa tayari, na kwa kweli nilikuwa na furaha kuwa katika hadhira kumtazama anafanya hivyo.

Kwa upande mwingine, ninafurahi kwamba mwishowe, kwa kadiri Tanzania inavyohusika, sasa tumebuni nyenzo kwa upande wa hazina ya Serikali na fedha, ambayo inaweza kuchangia maendeleo yetu bila vikwazo visivyokuwa vya lazima vinavyotokana na sera za kisiasa na kiuchumi za ulimwengu wa tatu ambazo hazina uratibu.”

Kuanzishwa kwa benki hiyo kulifanyika haraka na shughuli zake zikafanyika katika majengo ya muda. Ujenzi wa jengo maarufu la BoT ambalo liko katikati ya minara miwili ya BoT jijini Dar es Salaam lilianza ulianza Desemba 1966.

Hata hivyo, Shirikisho la Afrika Mashariki halikuanza kwa sababu Kenya na Uganda walikuwa na hofu ya kufanya jambo hilo. Hatimaye nchi hizo tatu zilianzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka uliofuata, yaani mwaka 1967.

Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ilianzishwa na kupewa dhamana ya kusimamia ‘huduma za pamoja’ ambazo zilijumuisha makao, huduma za posta, reli na usafiri wa anga.

Sera za fedha na hazina ya Serikali, sarafu na huduma za kibenki hazikuwa sehemu ya mpango huo, labda kwa sababu nchi hizo tatu zilitumia falsafa tofauti za kiuchumi.

EAC ilivunjika mwaka 1977, lakini ikaja kufufuliwa miaka 22 baadaye, mwaka 1999. Lengo kuu la EAC iliyofufuliwa ni shirikisho la kisiasa wa hatua kwa hatua. Baada ya kupitia Umoja wa Forodha na Soko la Pamoja, hatua inayofuata ni Umoja wa Fedha (Monetary Union) ambao ungeziunganisha Serikali wanachama wa EAC katika masuala ya kifedha.

Gavana wa kwanza wa BoT alikuwa Edwin Mtei (1966-1974). Charles Nyirabu alimrithi Mtei na alidumu kwenye wadhifa huo hadi mwaka 1989 aliporithiwa na Gilman Rutihinda.

Kuanzia mwaka 1993 hadi 1998 Idris Rashid alikuwa gavana. Rashidi alisimamia mageuzi makubwa katika BoT ambayo iliiwezesha taasisi hiyo kusimamia utitiri wa benki na taasisi za kifedha baada ya uchumi huria ulioruhusu kuanzishwa benki binafsi.

Baadhi ya benki, hususan zinazomilikiwa na wageni zilikuja na utaalamu wa hali ya juu wa kifedha na teknolojia ambao ulihitaji benki kuu yenye uwezo wa kusimamia.

Daudi Balali, aliyeteuliwa mwaka 1998 alidumu kwa miaka kumi. Vivyo hivyo Profesa Benno Ndulu ambaye aliteuliwa mwaka 2008.

Gavana wa sasa Profesa Florens Luoga aliteuliwa mwaka 2018. Baadhi ya naibu magavana walioteuliwa BoT tangu kuanzishwa kwake ni pamoja na Bob Makani (1974-1986), Ndewirwa Kitomari (1987-1995), Mohammed Mbaye (1997-2002) na Juma Reli (2005-2016).

Wengine ni Profesa Benno Ndulu (kuanzia Julai 2007 Januari 2008), Lila Mkila (kuanzia Julai 2007 hadi Juni 2017) Dk Enos Bukuku (Januari 2008 hadi Mei 2011), Dk. Natu Mwamba (Juni 2011 - Juni 2017), Julian Banzi Raphael (Jan 2016 –hadi leo), Dk Bernard Kibesse (Mei 2017 hadi leo) na Dk Yamungu Kayandabila (Mei 2017 hadi leo).