Tanzania miaka 60: Serikali yaalika nchi 65 kushuhudia sherehe za uhuru wa Tanganyika

Tanzania miaka 60: Serikali yaalika nchi 65 kushuhudia sherehe za uhuru wa Tanganyika

Muktasari:

  • Maandalizi ya sherehe za uhuru yalikuwa kemkem na katika mialiko yake Tanganyika haikusahau msimamo wake kuhusu ‘marafiki’ na ‘maadui’ wa kisiasa.

“Nchi zote za Jumuiya ya Madola isipokuwa nchi za Nyasaland (Malawi), Southern Rhodesia ( Zimbabwe) na Northern Rhodesia (Zambia) zimealikwa kuhudhuria sherehe za za uhuru wa Tanganyika Desemba 9, 1961,” alisema Waziri wa Mambo ya Ndani, George Kahama.

Kahama alisema Serikali imetuma mwaliko katika jumla ya nchi 65, lakini si kwa Afrika Kusini. Vyama vya kitaifa vya Afrika Kusini na mashirikisho ya ukanda huo yaliombwa kutuma wawakilishi wake kwenye tukio hilo kubwa na la kihistoria na hakutakuwa na zuio kwa waandishi wa habari kutoka katika mataifa yasiyopewa mwaliko.

“Mtu yoyote anayefahamu siasa atatambua kwa nini nchi hizo hazikualikwa kwenye uhuru. Sera na mitazamo ya Serikali yetu kuhusu nchi hizi inafahamika vyema lakini kuna waandishi wengi wa Afrika Kusini ambao hawafungamani na Serikali yao, wanaruhusiwa kuhudhuria,” alisema Kahama.

Kahama alisema mbali na viongozi wa juu wa mataifa yaliyoalikwa, kutakuwa na wageni wengine 130 kutoka nje ya Tanganyika.

Chanzo: Gazeti la Tanganyika Standard


Tanu yawapa wanafunzi laki moja nembo za uhuru

Wanafunzi laki moja kwenye shule mbalimbali za Tanu Tanganyika walipewa nembo maalumu za kilele cha siku ya uhuru Desemba 9, 1961.

Hayo yalielezwa jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa sherehe za uhuru wa chama cha Tanu, Chande Ali. Nembo hizo zilikuwa na picha ya Waziri Mkuu, Julius Nyerere pamoja na bendera ya chama hicho zilizotengenezwa Uingereza. Tanu iliagiza nembo 500,000.

Mbali na nembo zilizotolewa kwa wanafunzi, zilizobaki ziliuzwa ili kuchangia mfuko wa chama kwa ajili ya maandalizi ya uhuru ambazo zitaingiza kiasi cha Paundi 15, 000.

Ali alisema mbali na nembo hizo, kamati hiyo ilikuwa na mpango wa kuuza vipeperushi 50,000 vya rangi kwa ajili ya uhuru.

Chanzo: Gazeti la Tanganyika Standard


Serikali yatoa utaratibu mpya wa elimu baada ya uhuru

Hati ya kisheria inayotoa utaratibu wa aina moja ya elimu kuhusu mataifa yote yaliyopo Tanganyika ilitangazwa na Serikali.

Kwa kufuata mipango ya hati ya sheria ya elimu ya mwaka 1961 ambayo ilijadiliwa katika Baraza la Taifa, Waziri wa Elimu atashika madaraka kamili ya kukuza elimu na kuendeleza shule Tanganyika.

Kamati ilianzishwa ili kumshauri waziri huyo utaratibu wa elimu nchini Tanganyika. Kila Serikali ya mtaa yaani manispaa, halmashauri za miji na wilaya pia zitakuwa na mamlaka juu ya elimu ya msingi katika maeneo yake.

Aidha, mpango unafanywa wa kuanzisha halmashauri za wasimamizi au kamati za shule na zile zinazosaidiwa na Serikali kabla shule yoyote haijaanzishwa.

Chanzo: Gazeti la Busara


Duncan Sandy’s ateuliwa kuongoza wajumbe kutoka Uingereza katika sherehe za uhuru

Waziri wa uhusiano wa Jumuiya ya Madola, Duncan Sandy’s aliteuliwa kuongoza wajumbe wa watu kutoka Uingereza watakaohudhuria sherehe za uhuru Desemba 9, 1961.

Pia Sandy’s atafuatana na Katibu wa Idara ya Ufundi, Dewnis Vosper, Waziri wa Makaloni wa Jumuiya ya Madola, Sir Hilton Pyntoni na balozi wa Uingereza ambaye atakuwa Tanganyika, Neil Pritchard.

Wajumbe wengine watakaohudhuria sherehe hizo ni Eric Harrison, balozi wa Australia nchini Uingereza, Waziri Mkuu wa Guinea, Abdulaya Diallo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Yasumi Kurogane, Waziri Mkuu wa New Zealand, J.S Reid, Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Ghana, Huang Hua na Rais wa Togo, Sylvanus Olympio. Chanzo: Gazeti la Busara