Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Uwekezaji wa Carbon Tanzania katika misitu ya asili na safari  kuelekea kwenye utunzaji misitu endelevu

Tanzania kwa sasa iko katika safari ya mabadiliko kuelekea maendeleo endelevu ikiwa na mipango mipya ya soko la kaboni. Mdau muhimu katika safari hii ni Carbon Tanzania, Kampuni inayoongoza katika kutumia misitu asili tangu kuanzishwa kwake mwaka 2013.

Kampuni ikifanya kazi kwa mkataba wa miaka 30 na jamii za asilia kwa kushirikiana na Kituo cha Kitaifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC), dhamira ya Carbon Tanzania yanakwenda zaidi ya faida za kiuchumi yakilenga kutengeneza mustakabali ambapo uhifadhi wa mazingira na ustawi wa kiuchumi vinakuwa sambamba.

Moja ya mafanikio makubwa ya Carbon Tanzania ni miradi yake inayojumuisha eneo la ardhi la jamii lenye ukubwa wa kilomita za mraba 16,700 pamoja na lengo la kuanzisha miradi katika hifadhi sita za Taifa zinazojumuisha jumla ya hekta 1.8 milioni.

Hata hivyo, mafanikio ya Carbon Tanzania ndani ya Wilaya ya Kiteto, Mkoa wa Manyara ambapo mradi wa Makame Savannah unaoendeshwa na Jumuiya ya uhifadhi wanyamapori (WMA) umekuwa msingi wa mapato endelevu kwa zaidi ya wakazi 26,000.

Mapato haya yamesaidia kuboresha maisha, kuruhusu Wamasai kuendelea na mtindo wao wa maisha wa jadi kwa amani na kusaidia huduma muhimu za kijamii kama afya, upatikanaji wa maji na elimu. Hii inaonyesha dhamira ya kampuni hiyo katika kuleta uendelevu.

Mafanikio mengine makubwa ya Carbon Tanzania ni pamoja na uwezo wa kutumia mbinu zake katika maeneo tofauti yenye jamii mbalimbali na kuwapatia mapato ya fidia ya kaboni kwenye soko la hiari la kaboni kupitia juhudi za jamii husika katika kulinda na kuhifadhi misitu yao.

Hii inaleta chanzo kipya cha mapato na thabiti kwa wadau wa uhifadhi na jamii husika.  Ni muhimu kwa kuwa miradi hii inawezesha jamii kupata fedha moja kwa moja kutoka ulimwengu uliondelea kuja kwenye jamii za Kitanzania. Haya ni mafanikio makubwa ikizingatiwa kuwa watu wa asili hupata chini ya asilimia 1 ya fedha za mabadiliko ya tabianchi kama ilivyoripotiwa na taasisi ya Rainforest Foundation Norway.


Ushirikiano wa Carbon Tanzania umeweza kuonekana hivi karibuni kupitia kusaini Hati ya Makubaliano (MoU) ya mwaka mmoja kwa ajili ya upembuzi tyakinifu katika Hifadhi sita za Taifa za Tanzania kwa kushirikina na TANAPA, jamii, Serikali za vijiji na wilaya kwa lengo la kusisitiza umuhimu wa kufanya kazi pamoja kufikia malengo ya kimazingira na kiuchumi.

Nguvu hii ya ushirikiano inatilia mkazo wito wa Rais Samia Suluhu wa hivi karibuni aliyeagiza kuwepo na ushirikiano wa kutosha ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ili kukabiliana na  utawala wa wageni katika biashara ya kaboni.

Kampuni hiyo imeweka mikakati imara ya udhibiti katika mazingira kuhakikisha linafuata kanuni na viwango vya kitaifa na kimataifa. Hatua hii siyo tu inaongeza uaminifu wa miradi yake bali pia inajenga mazingira mazuri kwa wawekezaji wanaotafuta mazingira bora ya kuwekeza yanayofuata sheria na kanuni.

Kitu kinachowatofautisha zaidi Carbon Tanzania ni dhamira yao ya kutoa mapato ya fidia ya kaboni yenye ubora wa hali ya juu. Kuzingatia viwango vya uthibitishaji kama vile Verra na Plan Vivo kunahakikisha kuwa miradi yao inakidhi vigezo vya kimataifa na hivyo kuchangia kufikia malengo ya kimataifa ya mazingira.

Hii inaifanya Carbon Tanzania kuwa kampuni ya kutegemewa na wa kuaminika kwa wawekezaji wanaoipa kipaumbele miradi yenye matokeo chanya na endelevu.

Eneo la kimkakati la Carbon Tanzania ndani ya soko la hiari la kaboni nchini Tanzania linalingana na mahitaji yanayoongezeka kimataifa ya mapato ya fidia ya kaboni.

Historia yake iliyojaa mafanikio, miradi inayoongozwa na jamii na dhamira ya viwango vya ubora inaifanya kuwa chaguo la kuvutia kwa wawekezaji wanaotafuta faida za kifedha pamoja na athari chanya kwa mazingira na jamii.

Kulingana na Ripoti ya Uwekezaji wa Biashara ya Kaboni ya Kimataifa kwa mwaka 2023 iliyofanywa na Trove Research, uwekezaji katika miradi kati ya 2012 na 2022 ulifikia dola bilioni 36 na nusu ya uwekezaji huo ulifanywa katika miaka mitatu iliyopita. Carbon Tanzania inachangia katika taswira hii, kuwavuta wawekezaji wanaotambua uwezekano wa kupata faida za kifedha na utunzaji wa mazingira na misitu ya asili.

Mbali na mikopo ya kaboni, soko la kimataifa la bioanuwai linaloinukia linatoa fursa mbalimbali kwa Tanzania ndani ya wigo wa suluhisho za msingi za asili kuelekeza fedha kwa jamii zilizoko mstari wa mbele katika kulinda bioanuwai.

Zaidi ya mapato ya fidia ya kaboni, uwekezaji katika bioanuwai unachangia katika uthabiti wa mfumo wa ikolojia, jambo muhimu katika kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mapato ya fidia ya bioanuwai, ikiwa ni msingi wa taswira inayobadilika ya suluhisho za msingi za asili Tanzania, inawakilisha mabadiliko muhimu katika uhifadhi wa mazingira na misitu ya asili, na maendeleo endelevu. Mapato ya fidia hizi yanaenda mbali zaidi ya miradi ya asili inayojikita katika kaboni, ikitambua thamani halisi ya mifumo mbalimbali ya ikolojia.

Mapato ya fidia ya bioanuwai, mfumo ulioundwa kujumuisha thamani ya kiuchumi ya bioanuwai katika masoko ya kimataifa, hufanya kazi kama kitengo kinachopimika na kilichothibitishwa. Uwasilishaji huu wa kidijitali unalenga kuepuka upotezaji au ongezeko katika eneo la bioanuwai.

Viwango vingi vinajitokeza kuelezea na kuweka itifaki za usanifishaji na upimaji wa bioanuwai ulimwenguni, kuongeza uaminifu na ufanisi wa jitihada kama hizo.

Katika Mkutano wa COP28, Azaria Kilimba, Meneja wa Operesheni wa Carbon Tanzania, alisisitiza thamani ya bioanuwai na asili. Huku akikiri umuhimu wa mapato ya fidia ya kaboni, alitoa mtazamo mpana kuhusu mapato ya fidia ya bioanuwai, akisisitiza, “Mapato ya fidia hizi yanapaswa kujumuisha uelewa zaidi wa hali ilivyo katika jamii, kujumuisha jukumu muhimu la jamii za wazawa katika kujenga thamani halisi ya asili. Katika taswira hii, tofauti kati ya mapato ya fidia ya kaboni na ya bioanuwai inafuata baada ya lengo mama la kuzalisha fedha kwa jamii, hivyo kusaidia katika kulinda na kuelewa thamani halisi ya mazingira yaliyolindwa.”

Wakati Tanzania ikijipambanua kama mdau muhimu katika soko la kaboni duniani, Carbon Tanzania inasimama kama ushahidi wa fursa zinavyojitokeza huku ushirikiano na uwekezaji vikikutana kwa maslahi ya pamoja. Kwa kushughulikia changamoto za kisheria na kutumia fursa za masoko yanayochipuka, Tanzania inatengeneza njia kuelekea mustakabali ambao utajiri wa asili unakuwa chanzo cha ustawi endelevu kwa wote.

Huku dunia ikielekea katika mustakabali chanya wa asili, hatua za Tanzania katika masoko ya kaboni na bioanuwai zinaiweka katika nafasi muhimu katika jitihada za kimataifa za kuleta pamoja maendeleo ya kiuchumi na utunzaji wa mazingira na misitu ya asili.