Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Siku 100 za Rais Samia: OSHA yaacha alama ukuzaji uwekezaji, kuimarisha usalama wa wafanyakazi

Mtendaji Mkuu wa OSHA,  Khadija Mwenda (kushoto) akikabidhi vifaa vya kujikinga kwa ajili ya shughuli za ukaguzi wa mifumo ya usalama na afya mahali pa kazi kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Kazini, Deus Sangu (kulia).

Wakati tathmini za utendaji wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan ndani ya siku 100 za uongozi wake zikiendelea kutolewa na taasisi, wadau na mashirika mbalimbali, mchango wa Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) katika kufanikisha malengo ya Serikali umefahamika.

Ndani ya siku 100 za Rais, Dkt. Samia, Wakala huo ulitembelewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu–Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu aliyefika katika ofisi hizo zilizopo Kinondoni, Dar es Salaam, kujionea utendaji wa taasisi hiyo.

Akiwa katika ziara hiyo, Waziri Sangu aliikumbusha OSHA juu ya wajibu ilionao katika kusimamia masuala ya usalama na afya mahali pa kazi, akiwasisitiza kusajili maeneo yote ya kazi ikiwamo viwanda, mashamba, ofisi, maeneo ya ujenzi na karakana ambazo hazijasajiliwa ndani ya siku 90 kuanzia Januari 2026.

Mkaguzi wa Mitambo wa OSHA, Sam Sichone (kulia) akifanya tathmini ya usalama katika mtambo wa uchimbaji madini wakati wa ukaguzi katika eneo la mgodi. Pembeni yake ni mtaalamu wa mitambo wa taasisi hiyo.

Maelekezo hayo yanalenga kusimamia uwajibikaji wa kitaifa katika nyakati hizi muhimu, ambapo Tanzania inaingia katika hatua za ukuzaji uchumi kupitia utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050 unaotakiwa kwenda sambamba na uzingatiaji wa utu. “Taasisi hii ina jukumu kubwa,” Waziri Sangu aliwaambia wafanyakazi wa OSHA.

“Mmekabidhiwa jukumu la kulinda nguvu kazi yetu dhidi ya ajali, magonjwa na vifo vinavyotokana na mazingira yasiyo salama ya kazi. Ili OSHA iweze kusimamia usalama kwa ufanisi, maeneo ya kazi lazima kwanza yatambuliwe na kusajiliwa.”

Ziara yake hiyo, ya kwanza tangu kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, ilikuwa ya kimkakati, iliyoakisi dhamira ya Serikali ya kuimarisha mifumo ya kazi huku ikiweka maslahi ya wafanyakazi katikati ya maendeleo ya Taifa.


Hata hivyo, agizo la siku tisini linakuja wakati ambao tayari OSHA imepata mafanikio makubwa katika siku 100 za kwanza za Serikali ya Awamu ya Sita, mafanikio yanayoonesha jinsi shughuli za OSHA zinavyobadilisha mitazamo ya watanzania kuhusiana na masuala ya usalama na afya, tija na kazi zenye staha.

Kwa miaka mingi, utekelezaji wa sera ya usimamizi wa afya na usalama mahali pa kazi umekuwa jambo la kusukumana miongoni mwa waajiri na wafanyakazi wengi ambao walikuwa wakiona kama adhabu, lakini hivi sasa mambo yamebadilika.

Nyuma ya mabadiliko haya yupo Mkurugenzi Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, ambaye uongozi wake umeisaidia mamlaka kubadilika kutoka kuwa msimamizi tu wa sheria na kuwa mshirika wa maendeleo.

“Kwa niaba ya wafanyakazi wenzangu, nakuhakikishia kwamba hatutakuwa sababu ya kukwamisha utendaji wako. Badala yake, tutajitahidi kutekeleza majukumu yetu ipasavyo, ili viongozi wetu wasonge mbele kwa sababu ya matokeo yetu,” amesema Khadija.

Maneno yake yanaakisi falsafa ya ndani ya taasisi kwamba usalama na afya kazini huongeza tija na kinga ni bora kuliko tiba.

Chini ya uongozi wake, OSHA imeongeza ukaguzi, imeboresha utoaji wa huduma kwa kutumia mifumo ya kisasa, imepanua programu za mafunzo, na kuimarisha ushirikiano na waajiri, ikiweka msingi wa maeneo salama ya kazi katika sekta zote.

Mkurugenzi Mtendaji wa Omega Fish Limited, Hamad Alsalman (katikati), akimpa maelezo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano Kazini), Deus Sangu (kulia), sambamba na Mtendaji Mkuu wa OSHA,  Khadija Mwenda (kushoto)  wakati wa ziara rasmi yake katika kiwanda cha kuchakata samaki. Ziara hiyo ililenga kukagua utekelezaji wa Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Na. 5 ya mwaka 2003 pamoja na sheria nyingine zinazohusu kazi.

Katika kipindi cha Novemba 2025 hadi Januari 2026 pekee, OSHA ilifanya kaguzi 98,771, ikilinganishwa na kaguzi 80,396 katika kipindi kama hicho mwaka mmoja uliopita.

Kaguzi hizi zilijumuisha masuala ya usalama wa umeme, usalama wa mitambo na zana za kazi, maeneo ya ujenzi, mifumo na taratibu za igonomia, vifaa vya kunyanyulia mizigo mizito, ubora wa hewa na afya ya mazingira.

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda.

Wakati huo huo, uchunguzi wa afya kwa wafanyakazi ulifikia 196,682, huku idadi ya waliopata mafunzo ya usalama na afya kazini ikiongezeka kutoka 4,317 hadi 5,097.

Nyuma ya takwimu hizi, kuna maelfu ya maisha yaliyolindwa vyema na hatari nyingi zilizobainika kabla ya majanga kutokea.

Kwa mujibu wa vifungu vya 16 na 17 vya Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003, maeneo yote ya kazi nchini yanapaswa kutambuliwa na OSHA kupitia usajili maalum ili kuwezesha maeneo husika kufikiwa kwa ajili ya ukaguzi wa mifumo ya usalama na afya pamoja na kupatiwa ushauri wa maboresho yanayohitajika.

Kufuatia kampeni ya kitaifa ya usajili iliyoanzishwa chini ya Serikali ya Awamu ya Sita, idadi ya maeneo ya kazi yaliyosajiliwa imeongezeka kutoka 2,084 hadi 3,427 ndani ya miezi mitatu tu.

Kila usajili ni zaidi ya kutii sheria; ni ufunguzi wa mlango wa ushauri wa kitaalam, tathmini za vihatarishi na maboresho endelevu.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano Kazini), Mheshimiwa Deus Sangu (kushoto) na Naibu wake, Rahma Kisuo (kulia) wakiwa wamebeba maua wakati wa ziara yao iliyolenga kukagua utekelezaji wa Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Na. 5 ya mwaka 2003 pamoja na sheria nyingine zinazohusu kazi.

Waziri aliwahimiza wafanyakazi wa OSHA kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi pamoja na kujituma, huku akiwataka waajiri kuzingatia kwa umakini mkubwa ushauri unaotolewa na wataalam wa OSHA ambapo alisisitiza kuwa ulinzi wa nguvukazi ya Taifa ni jukumu la kila mtu.