Ubunifu wa kidijitali unavyosaidia OSHA kulinda maisha, kuimarisha maeneo ya kazi
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano Kazini), Mheshimiwa Deus Sangu (kushoto) akimsaidia Mwenyekiti wa Kikundi cha Wanawake Wachimbaji Wadogo wa Madini Wilaya ya Bukombe, Regina Kabogo kuvaa fulana maalum ya kujikinga (reflective vest), ikiwa ni sehemu ya vifaa vya kujikinga vilivyotolewa na OSHA kwa kikundi hicho. Msaada huo uliambatana na mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi kwa kikundi hicho chenye zaidi ya wanachama 350.
Moja ya mafanikio makubwa zaidi ya OSHA hivi sasa ni utoaji wa huduma zake kwa njia ya kidijitali. Kupitia mfumo wa kielektroniki wa Usimamizi wa Taarifa za Sehemu za Kazi (Workplace Information Management System-WIMS), vyeti vya usajili wa maeneo ya kazi ambavyo awali vilichukua hadi siku 14 kutolewa, sasa vinapatikana ndani ya siku moja tu.
Leseni za kukidhi viwango vya usalama na afya (compliance license) ambazo hapo awali zilichukua hadi siku 28, sasa zinachakatwa ndani ya siku tatu. Mfumo mpya wa WIMS unaotegemea Tehama unawawezesha waajiri kusajili maeneo yao ya kazi, kuomba mafunzo, kuripoti ajali, kuwasilisha nyaraka na kufanya tathmini binafsi moja kwa moja kutoka ofisini kwao.
Kwa biashara ndogo katika maeneo ya vijijini na wawekezaji wakubwa katika miji mikubwa, mabadiliko haya yamepunguza gharama, kuondoa ucheleweshaji, na kurejesha imani katika huduma za umma. Lakini faida zake haziishii katika ufanisi pekee.
Mbinu ya ukaguzi inayozingatia sekta maalum imehamasisha kampuni/taasisi kujumuisha mifumo ya usimamizi wa usalama kama sehemu ya utamaduni wao, hali iliyoongeza mahitaji ya Maafisa Usalama Mahali pa Kazi na hivyo kuzalisha ajira mpya kwa Watanzania.
Wakati huo huo, kuongezeka kwa uelewa kuhusu afya kazini kumechochea uwekezaji katika utengenezaji na usambazaji wa vifaa vya kinga binafsi (PPE’s), sambamba na uanzishwaji wa viwanda vipya huku wafanyakazi walioko kazini wakilindwa.
Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda (kushoto) akimkabidhi Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano Kazini,) Rahma Kisuo (kulia) Vifaa vya Kujikinga (PPE) kwa ajili ya matumizi wakati wa ziara zake za ukaguzi wa usalama na afya mahali pa kazi.
Mafanikio haya ya Tanzania yamekuwa kivutio hata ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki. Wataalamu kutoka nchi jirani, ikiwemo Sudan Kusini, sasa wanakuja Tanzania kwa mafunzo ya OSHA, jambo linaloimarisha nafasi ya nchi kama kitovu kinachochipukia katika masuala ya usalama na afya kazini.
Utambuzi nje ya mipaka
Mafanikio ya Tanzania hivi karibuni yaliipatia OSHA uongozi wa Dawati la Usalama na Afya Kazini la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), baada ya kuwapiku wataalamu 48 kutoka nchi 16 wanachama.
Ingawa muhula wa awali umekamilika, Sekretarieti ya kikanda imeiomba rasmi Tanzania kuteua mtaalamu mwingine, ikiwa ni ishara ya kuendelea kuwa na imani katika uwezo wa kitaalamu wa nchi. Utambuzi huu unaimarisha sauti ya Tanzania katika kutengeneza viwango vya kazi vya kikanda, huku ukifungua fursa za ushirikiano wa kitaalam na kubadilishana maarifa. Ni ushindi wa kidiplomasia uliojengwa kwa mifumo inayo fanya kazi.
Kulinda maendeleo katika miradi ya kimkakati
Wakati Tanzania ikiendelea na miradi mikubwa ya miundombinu kama Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere, Reli ya Kisasa (SGR), Bomba la Mafuta Ghafi la Uganda–Tanga, upanuzi wa bandari, shughuli za madini na ujenzi wa barabara, OSHA imeendelea kushiriki kikamilifu katika maendeleo haya.
Kupitia ukaguzi wa wakati muafaka na usimamizi wa kitaalam, Mamlaka inahakikisha kuwa kasi ya utekelezaji wa miradi haigharimu usalama wa wafanyakazi. Hatua hizi zinalinda maisha huku zikilinda uwekezaji, na kuwezesha miradi kuendelea kwa ufanisi na uendelevu.
Wafanyakazi wa Kampuni ya Geita Gold Mine Limited (GGML) wakionesha taratibu mbalimbali za uokoaji zinazotumika kukabiliana na ajali zinazoweza kutokea mahali pa kazi.
Katika mtazamo huu, usalama unakuwa nyenzo ya kuongeza tija, kupunguza usumbufu, kuzuia ajali na kujenga uaminifu kati ya wafanyakazi na waajiri.
Usalama kama haki ya msingi
Kimataifa, usalama na afya kazini ni jambo lililochukua sura mpya. Mwaka 2022, Shirika la Kazi Duniani (ILO) lilitambua rasmi usalama na afya kazini kama haki ya msingi mahali pa kazi. Tanzania imekumbatia mabadiliko haya. Katika hotuba yake ya Mei Mosi Mjini Dodoma, Rais Samia Suluhu Hassan alitangaza kuwa nchi iko katika mchakato wa kuridhia Mkataba wa ILO Na. 155, akisisitiza dhamira ya Serikali kuupa hadhi usalama wa wafanyakazi kutoka kuwa wajibu wa kisheria hadi kuwa kanuni ya msingi. Ni tamko linalosisitiza kuwa maendeleo hayapaswi kuletwa juu ya madhira yanayoweza kuzuilika.
Kujenga Kesho: Kituo cha umahiri cha OSHA
Kwa siku zijazo, Serikali, katika mipango yake mikubwa zaidi ya masuala ya usalama na afya kazini, inatazamia kuanzisha Kituo cha Umahiri cha Usalama na Afya Kazini chenye maabara za kisasa. Kwasasa, sampuli muhimu kama vumbi hatarishi mara nyingi hulazimika kuchunguzwa nje ya nchi, jambo linalogharimu mabilioni ya shilingi na kuchukua miezi kadhaa.
Kitakapokamilika, Kituo hicho kitapunguza muda wa majibu hadi siku 14 tu, kupunguza gharama kwa kiwango kikubwa, na kuongeza uwezo wa kuchakata sampuli kutoka takribani 200,000 hadi zaidi ya milioni moja kwa mwaka.
Mbali na huduma za maabara, Kituo hicho kitatoa mafunzo ya juu, utafiti, ubunifu na ushauri wa kitaalam kwa nchi nyingi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, na kuiweka Tanzania kama kitovu cha kikanda cha maarifa ya usalama na afya kazini. Mradi huu tayari umefikia hatua ya usanifu wa kina, ukiwa ni hatua nyingine muhimu iliyofikiwa ndani ya siku 100 za kwanza za Serikali ya Awamu ya Sita.
Mapinduzi katika maeneo ya kazi Tanzania
Akiwa hapo Kinondoni, Waziri Sangu aliwakumbusha wafanya kazi wa OSHA kwamba weledi, kujituma na uadilifu lazima viwe dira ya kazi zao za kila siku. Agizo lake la siku tisini sasa linasimama kama kikomo cha muda na pia mwaliko, likiwahimiza waajiri kujiunga katika juhudi za kitaifa za kulinda wafanyakazi na kuimarisha uzalishaji ili kujenga uchumi imara wa nchi.
Akina mama wakifuatilia mafunzo ya umuhimu wa usalama na afya mahala pa kazi yanayotolewa na OSHA.
Kupitia mageuzi ya teknolojia yanayoendelea kote Tanzania, kumekuwa matokeo chanya katika eneo hili la usalama na afya mahali pa kazi ambapo yanaonekana katika huduma za kidijitali zilizo haraka zaidi, katika ongezeko la takwimu za ukaguzi, katika maafisa wapya wa usalama wanaoingia maeneo ya kazi, na katika wafanyakazi wanaorejea nyumbani salama kila mwisho wa siku.
Aidha, mageuzi hayo, yanasikika katika sauti za uongozi zinazozungumza kwa uwazi na huruma. Na yanaakisiwa katika OSHA inayobadilisha namna uzalishaji unavyofanyika jambo ambalo limeleta tija kubwa katika uchumi wa Taifa pamoja na ustawi wa wafanyakazi.