UCSAF inavyofungua milango na fursa za maendeleo kupitia uboreshaji wa huduma za mawasiliano nchini
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk Samia Suluhu Hassan (kulia) akipokea tuzo kutoka kwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki wakati wa hafla ya uzinduzi wa minara 758 ya mawasiliano, kuunganishwa kwa mkongo wa mawasiliano katika wilaya 85 na makabidhiano ya mkongo wa mawasiliano serikalini iliyofanyika Aprili 10, 2026 katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre, jijini Dodoma.
Katika kile kinachotajwa kama kilele cha mapinduzi ya teknolojia ya habari na mawasiliano nchini, Serikali ya awamu ya sita imehitimisha hatua kubwa ya kihistoria kwa kuwafungulia ulimwengu mamilioni ya wananchi waishio maeneo ya vijijini.
Hafla ya uzinduzi wa minara 758 ya mawasiliano, kuunganishwa kwa mkongo wa mawasiliano katika wilaya 85 na makabidhiano ya mkongo wa mawasiliano serikalini iliyofanyika Aprili 10, 2026 katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre, jijini Dodoma imeweka alama isiyofutika katika safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kidijitali.
Hafla hiyo iliyopambwa na uwepo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Dk Samia Suluhu Hassan, imekuwa ni uthibitisho wa dhamira yake ya dhati ya kuhakikisha kuwa hakuna mtanzania anayeachwa nyuma katika upatikanaji wa huduma bora na za uhakika za mawasiliano, bila kujali umbali au eneo alilopo.
Akizungumza katika hafla hiyo Rais Dk Samia alisema katika dunia ya sasa inayobadilika kwa kasi, huduma za mawasiliano si tena jambo la anasa bali ni huduma ya lazima na uti wa mgongo wa uchumi wa kisasa.
Alilinganisha hali ya zamani ambapo mtaa mzima ulitegemea simu moja na hali ya sasa ambapo kila nyumba ina mawasiliano, akibainisha kuwa teknolojia ni daraja la fursa za uwekezaji na ajira kwa wananchi.
Viongozi na wananchi mbalimbali wakifuatilia hafla ya uzinduzi wa minara 758 ya mawasiliano, kuunganishwa kwa mkongo wa mawasiliano katika wilaya 85 na makabidhiano ya mkongo wa mawasiliano serikalini iliyofanyika Aprili 10, 2026 katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre, jijini Dodoma.
Rais alibainisha kuwa, kukamilika kwa ujenzi wa minara 758 ni hatua kubwa iliyoongeza upatikanaji wa huduma kwa wananchi zaidi ya milioni 8.5, hususani waishio vijijini na maeneo ya mipakani
“Hatua hii ni ukombozi kwa wananchi wa mipakani ambao awali walilazimika kutumia mitandao ya nchi jirani,” alisema Rais Dk Samia.
Aidha, alipongeza upanuzi wa Mkongo wa Taifa ambao sasa umefika katika wilaya 121 kati ya 139, ongezeko kubwa kutoka wilaya 36 pekee zilizokuwa zimeunganishwa mwaka 2021.
Rais Dk Samia pia alihimiza kuwa huduma za mawasiliano lazima zizingatie maadili, mila, na tamaduni za Mtanzani huku akionyesha kufurahishwa na mpango wa kampuni ya Huawei wa kutengeneza mfumo wa Akili Unde (AI) wa lugha ya Kiswahili ambao utasaidia kulinda maadili na kuchochea ubunifu kwa vijana.
“Serikali imetenga Sh 5 bilioni kwa ajili ya kutoa mitaji kwa kampuni changa za vijana (startups) ili kukuza ubunifu na ajira. Pia nimevutiwa hasa na bunifu za vijana nilizoziona, ikiwemo mfumo wa AI wa kuchunguza saratani (saratani AI) hivyo naihimiza wizara kuendelea kuwapatia mitaji ili kukua,” alieleza Rais Dk Samia.
Rais Dk Samia pia aliwashukuru wadau wa sekta binafsi (kama Vodacom, Airtel, Yas, Halotel, na TTCL), Benki ya Dunia na timu za majadiliano ya Serikali kwa ushirikiano wao uliowezesha Tanzania kuelekea kuwa kitovu cha mawasiliano katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohammed Khamis Abdulla akisaini Hati ya Makabidhiano kati ya Serikali na Umoja wa Watoa Huduma za Mawasiliano uliongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Yas Tanzania, Pierre Canton-Bacara (katikati), Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Charles Kamoto (wa kwanza kushoto) pamoja na Mkurugenzi wa Miundombinu ya Mtandao wa Kampuni ya Vodacom Tanzania, Andrew Lupembe. Makabidhiano hayo yalifanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma Aprili 10, 2026 na kushuhudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine wa juu wa Serikali. Kulia waliosimama ni Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki.
Kwa upande wake Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki alisema kuwa mafanikio haya ni matokeo ya maelekezo madhubuti na usimamizi wa karibu wa Rais Dk Samia.
Moja ya maelekezo muhimu yaliyotolewa na Rais Dk Samia ni lile la Mei 13, 2023, ambapo aliagiza kukamilishwa kwa ufanisi na tija mradi wa ujenzi wa minara ya mawasiliano katika maeneo yaliyokuwa na changamoto kubwa.
Mafanikio ya sekta ya mawasiliano: Takwimu zinaongea
Mhe. Waziri Kairuki amesema tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya awamu ya sita, sekta ya mawasiliano imeshuhudia ukuaji wa kishindo ambao haujawahi kushuhudiwa tangu uhuru.
Alibainisha kuwa hadi kufikia Machi 2026, idadi ya watumiaji wa huduma za mawasiliano ya simu nchini imepaa hadi kufikia milioni 106.9. Hili ni ongezeko la asilimia 102 ikilinganishwa na watumiaji milioni 52.8 waliokuwepo mwaka 2021.
Kasi hii ya ukuaji haikuishia kwenye sauti tu bali pia upatikanaji wa mtandao wa kasi umeongezeka na kufikia asilimia 94 ya maeneo yenye makazi ya watu. Idadi ya watumiaji wa intaneti imeongezeka mara mbili, kutoka milioni 29 mwaka 2021 hadi kufikia milioni 58.1 machi 2026.
Vilevile, huduma za kifedha mtandaoni zimekuwa mkombozi kwa wananchi, ambapo watumiaji wamefikia milioni 76.5, ongezeko la asilimia 133.9 kutoka milioni 32.7 mwaka 2021.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mohammed Khamis Abdulla amesema sambamba na miundombinu ya minara, Serikali imepata mafanikio makubwa katika Operesheni Anuani za Makazi iliyozinduliwa Februari 2022.
Amesema hadi sasa, Anuani za Makazi milioni 12.9 zimesajiliwa, kiasi kinachowakilisha asilimia 95 ya lengo la awali. Hili ni uboreshaji mkubwa kwani kabla ya operesheni hiyo, utekelezaji ulikuwa umefikia asilimia 3 tu tangu mwaka 2010.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk Samia Suluhu Hassan (katikati, walioketi) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Serikali pamoja na watoa huduma za mawasiliano wakati wa hafla ya uzinduzi wa minara 758 ya mawasiliano, kuunganishwa kwa mkongo wa mawasiliano katika wilaya 85 na makabidhiano ya mkongo wa mawasiliano serikalini iliyofanyika Aprili 10, 2026 katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre, jijini Dodoma. Wa tatu kushoto walioketi ni Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki
Mhe. Abdulla amesema mfumo huu sasa unatumika kutoa barua za utambulisho wa mwananchi kidijitali, hatua inayomwondolea mwananchi adha ya kusafiri kufuata huduma Serikali za mitaa. Mifumo 29 ya taasisi 23 za Serikali na sekta binafsi tayari imeunganishwa na mfumo huu ili kuboresha utoaji wa huduma.
“Mfumo huu unaendelea kuboreshwa ili kutumika kwenye Sekta nyingine kama vile sekta ya utalii, elimu, afya, fedha na usafirishaji,” amesema Mhe. Abdulla.
UCSAF: Nguzo Muhimu katika mapinduzi ya huduma za mawasiliano nchini
Katika kitovu cha mafanikio haya upo Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ambao umetekeleza mradi kabambe wa ujenzi wa minara 758 katika kata 713 kwenye mikoa yote 26 ya Tanzania bara.
Katika kutekeleza lengo la Serikali la kufikisha huduma ya mawasiliano kwa wananchi waishio katika maeneo ya vijijini na mijini yenye changamoto za mawasiliano, Mei 13, 2023 UCSAF iliingia makubaliano na watoa huduma za mawasiliano wakiwemo Airtel, TTCL, Honora, Viettel na Vodacom ya kujenga minara 758 katika kata 713 kwenye mikoa yote 26 ya Tanzania Bara.
Mgawanyo wa minara hiyo kwa watoa huduma ulizingatia uwezo na ushirikiano wa sekta binafsi, ambapo Honora ilijenga minara 261, Vodacom 190, Airtel 169, TTCL 104, na Halotel 34.
Huu ni uwekezaji mkubwa uliogharimu jumla ya Sh 126 bilioni ikiwa na ruzuku ya Serikali, ambapo Sh 71 bilioni ni fedha za ndani kupitia UCSAF na Sh 55 bilioni ni mkopo kutoka Benki ya Dunia kupitia mradi wa Tanzania ya Kidigitali.
Aidha, mradi huu haukuishia kujenga minara mipya pekee bali pia kuiongezea nguvu minara 304 kutoka teknolojia 2G kwenda 3G na 4G, jambo ambalo limewanufaisha wananchi zaidi ya milioni 4.2 kupata huduma bora za data.
Jambo jingine la kihistoria lililoshuhudiwa ni kufikishwa kwa huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika ngazi ya wilaya.
Agizo la Rais Dk Samia la kufikisha mkongo huu wilayani limetekelezwa kwa kishindo, ambapo jumla ya wilaya 85 mpya zimeunganishwa na kufanya jumla ya wilaya 121 kati ya 139 nchini kuwa na huduma ya mkongo.
Hali hii inaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa miundombinu bora ya mawasiliano barani Afrika, ikiimarisha usalama wa nishati ya habari na kuwezesha taasisi za umma na binafsi kutoa huduma kwa ufanisi zaidi.
Lengo ni upatikanaji wa huduma zote kidijitali mahali popote, kwa bei nafuu na kwa ubora ili kila Mtanzania aweze kunufaika.
Hadi kufikia Disemba 31, 2025 mradi wa minara 758 ulikuwa umekamilika kwa asilimia 100 ambapo kukamilika kwake kumewezesha wananchi zaidi ya 8,500,000 kupata huduma za uhakika za mawasiliano ya sauti na data. Aidha, kwa mradi wa kuongeza nguvu minara 304 ulikamilika Machi 2025.
Uwekezaji unaogusa maisha ya wananchi
Faida za uwekezaji huu wa Serikali kupitia UCSAF zimeanza kugusa maisha ya kawaida ya Watanzania. Wananchi wameonyesha shukrani zao wakibain-isha kuwa mawasiliano sasa yamekuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku, si tu kwa simu bali hata katika elimu.
“Sisi Wamasai zamani mawasiliano yetu yalikuwa ni ya mdomo, yaani nikikutana na mtu lazima nimuulize mahali alikotoka na anakokwenda na huyo akienda anamuuliza mwengine. Hivi sasa tunaweza kutumia simu hata kama mfugaji yupo machungani ukimpigia simu anakupa taarifa ya kinachoendelea. Kwa kweli tunaishukuru sana Serikali,” amesema Mzee Simon Zephania Mkazi wa Ngorongoro.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk Samia Suluhu Hassan akizindua minara 758, maunganisho ya Mkongo wa Mawasiliano katika Wilaya 85 na kukabidhi Mkongo wa Mawasiliano Serikalini kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma Aprili 10, 2026.
Kwa upande wake Mwalimu wa Shule ya Msingi Msolokelo iliyopo Mvomero mkoani Morogoro, Shaban Shelukindo amesema wanafunzi sasa wanaweza kutumia mtandao kupata mafunzo na kupakua video za kujifunzia mtandaoni.
Shelukindo amesisitiza kuwa, kauli ya Serikali ya kufanya mawasiliano yawe kila mahali sasa inatekelezwa kwa vitendo.
Hali kadhalika, maendeleo yameanza kuonekana katika sekta za kilimo na biashara vijijini, ambapo wananchi wanapata taarifa za masoko na mbinu mpya za uzalishaji kupitia simu zao za mkononi, jambo linalopunguza gharama za maisha na kuongeza tija.
Mikakati ya baadaye: Kuelekea 2030
Licha ya mafanikio haya makubwa, Serikali bado inaendelea na mikakati imara ya kuboresha huduma za mawasiliano. Safari ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha teknolojia inaendelea. UCSAF imetangaza kuwa tayari mikataba imesainiwa kwa ajili ya ujenzi wa minara mingine 201 katika kata 201, mradi unaotarajiwa kukamilika ifikapo Machi 2027 na kuwanufaisha wananchi zaidi ya milioni 2.8.
Aidha, mkakati wa mawasiliano wa kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2030 wananchi wote nchini wanapata huduma za mawasiliano tayari umeshaan-daliwa.
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ipo katika hatua za mwisho za ukamilishaji wa Sera ya Anga la Juu na mapendekezo ya kutunga Sheria ya TEHAMA, hatua ambazo zitaiweka Tanzania katika ramani ya dunia kama nchi inayozingatia weledi na utawala bora katika sekta ya teknolojia.
Mapinduzi haya ya mawasiliano nchini si tu kuhusu ujenzi wa minara na nyaya za mkongo ni kuhusu kumpa mwananchi uwezo wa kuwasiliana na mtu yoyote duniani.
Pia yanahusu kukuza uchumi wa kidijitali, kuzalisha ajira kwa vijana na kuongeza tija katika kila sekta ya uzalishaji. Chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan na utekelezaji makini wa UCSAF, Tanzania inasonga mbele kuelekea mapinduzi ya nne ya viwanda kwa kishindo.