Wakala wa Serikali wa Huduma za Matrekta na Zana za Kilimo: Nguvu mpya ya mageuzi ya kilimo Zanzibar
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Rashid Hadid Rashid (aliyevaa kofia) akikabidhi matrekta na zana zake kwa Wakala wa Serikali wa Huduma za Matrekta na Zana za Kilimo katika eneo la Machomanne Pemba. Matrekta hayo yalitolewa kupitia Mradi wa Kuimarisha Mifumo ya Chakula Tanzania (TFSRP) kwa kushirikiana na Mradi wa ODA.
Sekta ya kilimo imeendelea kuwa mhimili muhimu wa uchumi wa Zanzibar, ikitoa ajira kwa maelfu ya wananchi na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika usalama wa chakula pamoja na kipato cha kaya nyingi.
Katika juhudi za kuimarisha sekta hii, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanzisha na kuimarisha taasisi mbalimbali zenye jukumu la kusaidia wakulima kuongeza tija na uzalishaji.
Miongoni mwa taasisi hizo ni Wakala wa Serikali wa Huduma za Matrekta na Zana za Kilimo ulioanzishwa mwaka 2019, ambao umeendelea kuwa chachu ya mageuzi ya kilimo cha kisasa visiwani Zanzibar.
Kupitia utoaji wa huduma za mashine za kilimo, mafunzo kwa wakulima na ushirikiano na wadau mbalimbali, wakala huu umeleta mabadiliko makubwa katika namna kilimo kinavyofanyika Zanzibar.
Wataalamu wa Wakala wa Serikali wa Huduma za Matrekta na Zana za Kilimo wakitoa mafunzo ya uendeshaji wa mashine za kulimia kwa wakulima.
Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Ukulima, Mhandisi Said Jaffar Mussa wazo la kuanzisha wakala huo lilitokana na mahitaji ya kuongeza tija katika sekta ya kilimo kwa kutumia teknolojia na mashine za kisasa.
Hii ni kwa sababu, kwa muda mrefu wakulima wengi wa Zanzibar walikuwa wakitegemea mbinu za jadi, jambo lililosababisha uzalishaji mdogo na matumizi makubwa ya nguvu kazi ya binadamu.
“Serikali iliona umuhimu wa kuanzisha taasisi maalumu itakayoratibu na kusimamia matumizi ya matrekta pamoja na zana za kisasa za kilimo ili kusaidia wakulima kuongeza uzalishaji na kupunguza gharama za uzalishaji,” anaeleza Mhandisi Mussa.
Wakala huo ulianzishwa kama sehemu ya mkakati mpana wa kuimarisha kilimo cha kisasa, kwa lengo la kuwafikishia wakulima huduma za mashine za kilimo kwa urahisi na gharama nafuu.
Tangu kuanzishwa kwake, wakala umeendelea kupanua huduma zake kwa kuongeza idadi ya matrekta, zana za kilimo na wataalamu wa kilimo wanaotoa ushauri kwa wakulima.
Ikumbukwe kuwa, Zanzibar ina takribani ekari 22,000 ambazo zinatumika kulimwa kwa mazao mbalimbali ya chakula na biashara yakiwemo mashamba ya miwa na mboga mboga.
Hivyo wakala huwalimia wakulima wanaowasilisha maombi yao ya kulimiwa pamoja na taasisi za Serikali.
Majukumu ya wakala
Mhandisi Mussa anaeleza kuwa, jukukumu mama la wakala ni kurahisisha upatikaji na matumizi ya zana za kisasa za kilimo zitakazopelekea kuongeza ufanisi katika uzalishaji wa mazao ya kilimo kwa kuzingatia malengo na mikakati ya muda mrefu ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Majukumu mengine ya wakala ni kutoa huduma za matrekta na zana mbalimbali za kilimo kwa wakulima ili kurahisisha shughuli za kilimo kuanzia maandalizi ya shamba hadi kuvuna.
Mhandisi Mussa anafafanua kuwa wakala huo pia unasimamia matengenezo ya matrekta kupitia idara ndogo ya matengezo, kutoa mafunzo kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi ya zana za kilimo na kuhakikisha teknolojia mpya za kilimo zinawafikia wakulima kwa wakati.
“Tunajitahidi kuhakikisha kwamba wakulima wanapata huduma bora na kwa wakati. Lengo letu ni kuhakikisha kilimo kinakuwa rahisi, chenye tija na kinachovutia watu wengi zaidi kukifanya kama biashara,” anasema Mhandisi Mussa.
Mbali na hilo, wakala unashirikiana na wizara na taasisi nyingine za Serikali katika kuandaa mipango ya kuendeleza sekta ya kilimo, huku pia ukitoa ushauri wa kitaalamu kwa wakulima kuhusu mbinu bora za kilimo cha kisasa.
Ushirikiano na wakulima na wadau wa kilimoMoja ya nguzo muhimu katika mafanikio ya wakala ni ushirikiano wake na wakulima pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo. Kupitia ushirikiano huo, wakala umeweza kuwafikia wakulima wengi zaidi na kuwa-saidia kuboresha shughuli zao za kilimo.
Kwa mujibu wa Mhandisi Mussa, wakala hushirikiana na vyama vya wakulima, mashirika ya maendeleo, taasisi za utafiti na sekta binafsi ili kuhakikisha huduma za kilimo zinawafikia wakulima kwa ufanisi zaidi. “Tunafanya kazi kwa karibu na wadau mbalimbali ili kuhakikisha waku-lima wanapata huduma zote muhimu kwa wakati mmoja.
Kwa mfano, wakati tunatoa huduma za matrekta, tunahakikisha pia wakulima wanapata mbegu bora, ushauri wa kitaalamu na maso-ko ya mazao yao,” anasema Mhandisi Mussa.
Ushirikiano huu umechangia kuongeza uelewa wa wakulima kuhusu umuhimu wa kutumia teknolojia katika kilimo na kuwafanya wengi wao kuanza kuachana na mbinu za jadi.
Mafanikio katika kuongeza tija ya kilimo
Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, Wakala wa Serikali wa Huduma za Matrekta na Zana za Kilimo umefanikiwa kuongeza kiwango cha uzalishaji katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba.
Kupitia matumizi ya matrekta na zana za kisasa, wakulima wameweza kulima maeneo makubwa zaidi kwa muda mfupi, jambo ambalo limeongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali kama vile mpunga, mahindi na mboga mboga.
Mhandisi Mussa anasema kuwa wakala huo umefanikiwa pia kupunguza muda wa maandalizi ya mashamba na kuongeza ufanisi katika shughuli za kilimo.
“Zamani mkulima alitumia siku nyingi kuandaa shamba kwa kutumia jembe la mkono au wanyama kazi. Lakini sasa kwa kutumia trekta, shamba linaweza kuandaliwa kwa muda mfupi sana,” anaeleza. Matokeo yake ni kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao, kuimarika kwa usalama wa chakula na kuongezeka kwa kipato cha wakulima.
Juhudi za kuvutia vijana kuingia katika kilimo
Changamoto kubwa inayoikabili sekta ya kilimo katika maeneo mengi ni ushiriki mdogo wa vijana. Hata hivyo, wakala huu umechukua hatua mbalimbali kuhakikisha vijana wanaha-masika kuingia katika sekta hiyo.
Mhandisi Mussa anasema wakala umeanzisha programu maalum za mafunzo kwa vijana ili kuwafundisha kuhusu matumizi ya mashine za kilimo pamoja na mbinu za kilimo cha kisasa.
“Tunataka vijana waone kilimo kama fursa ya biashara na si kazi ya jadi pekee. Ndiyo maana tunatoa mafunzo na kuwasaidia kupata zana za kilimo ili waanzishe miradi yao. Kwa lugha nyingine tunasema tunaanzisha bodaboda wa kilimo,” anasema.
Kupitia mafunzo hayo pamoja na kuwajengea fursa za kupata mikopo ya zana za kilimo, vijana wengi wameanza kujihusisha na kilimo cha kisasa, hasa katika uzalishaji wa mazao ya biashara na bustani.
Mbali na kutoa zana za kilimo, wakala huu umeweka mkazo katika kuwahamasi-sha wakulima kuachana na mbinu za jadi na badala yake kutumia mbinu za kisasa zinazoongeza tija.
Mhandisi Mussa anasema kuwa wakala hutoa elimu kwa wakulima kuhusu matu-mizi sahihi ya mashine za kilimo, mbinu bora za kuandaa mashamba, matumizi ya mbegu bora na usimamizi wa mazao.
“Tunafanya kampeni mbalimbali za elimu kwa wakulima ili kuwafanya waelewe faida za kilimo cha kisasa. Lengo ni kuongeza uzalishaji na kuhakikisha kilimo kinakuwa endelevu,” anasema. Kwa mujibu wake, mabadiliko hayo tayari yanaonekana katika maeneo mengi ambapo wakulima wameanza kutumia teknolojia katika shughuli zao za kilimo.
Licha ya mafanikio makubwa yaliyopatikana, wakala huu bado unakabiliwa na changamoto mbalimbali. Miongoni mwa changamoto hizo ni uhaba wa matrekta na zana za kilimo ukilinganisha na mahitaji ya wakulima.
Aidha, baadhi ya wakulima bado wanaendelea kutumia mbinu za jadi kutokana na ukosefu wa uelewa au uwezo wa kifedha wa kumudu huduma za kilimo cha kisasa.
Mhandisi Mussa pia anataja changamoto ya miundombinu ya barabara katika baadhi ya maeneo ya kilimo, jambo linalosababisha ugumu katika kufikisha huduma za matrekta kwa wakulima.
Mkulima wa zao la mpunga Zanzibar akiendelea na kilimo kwa kutumiza trekta.
Ili kukabiliana na changamoto hizo, wakala umeweka mikakati mbalimbali ikiwemo kuongeza idadi ya matrekta na zana za kilimo, kuimarisha mafunzo kwa wakulima na kuimarisha ushirikiano na wadau wa sekta ya kilimo.
“Tunafanya kazi kwa karibu na Serikali pamoja na wadau wa maendeleo ili kuongeza rasilimali zitakazosaidia kupanua huduma zetu. Katika kulitekeleza hilo, Serikali kupitia wakala ilipata ufadhili wa matrekta ya kisasa kutoka Shirika la Maendeleo la Korea (KOICA),” anasema Mhandisi Mussa.
Pia wakala unapanga kuanzisha vituo zaidi vya huduma za mashine za kilimo katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wakulima.
Mustakabali wa kilimo Zanzibar
Kwa kuzingatia juhudi zinazoendelea kufanywa na Wakala wa Serikali wa Huduma za Matrekta na Zana za Kilimo, matarajio ya sekta ya kilimo Zanzibar yanaonekana kuwa mazuri.
Kupitia matumizi ya teknolojia na mashine za kisasa, wakulima wanaweza kuongeza uzalishaji na kuifanya sekta ya kilimo kuwa chanzo kikubwa zaidi cha ajira na maendeleo ya kiuchumi.
Mhandisi Mussa anaamini kuwa ikiwa juhudi hizi zitaendelea kuungwa mkono na wadau wote, Zanzibar inaweza kufikia kiwango kikubwa cha uzalishaji wa mazao na hata kuwa kitovu cha kilimo cha kisasa katika ukanda wa Afrika Mashariki.
“Kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wetu. Tukikiwekea mazingira bora na kutumia teknolojia sahihi, kinaweza kubadilisha maisha ya wananchi wengi,” anahitimisha.