Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

AAFP kujenga bwawa la mamba Ikulu kwa ajili ya mafisadi

Muktasari:

  • Kauli hiyo imetolewa leo, Jumatano Septemba 17, 2025, na mgombea urais wa AAFP Kunje Ngombare Mwiru, katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye viwanja vya Mwembeyanga, Wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam

Dar es Salaam. Chama cha Alliance for African Farmers Party (AAFP) kimesema endapo kitapata ridhaa ya kuongoza nchi, kitaanzisha hatua kali dhidi ya vitendo vya ufisadi, ikiwamo kujenga bwawa maalumu lenye mamba Ikulu kwa ajili ya kuwachukulia hatua mafisadi.

Kauli hiyo imetolewa leo, Jumatano Septemba 17, 2025 na mgombea urais wa chama hicho, Kunje Ngombare Mwiru, katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye viwanja vya Mwembeyanga, Wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam.

Mwiru amesema hatua hiyo ni ya ishara katika kupambana na rushwa, akisisitiza kuwa adhabu kali kwa watuhumiwa wa ufisadi ni jambo linalowezekana ikiwa kutakuwa na dhamira ya kweli ya kisiasa.

"Haiwezekani mtu kala hela za umma, anatembea na kitambi chake mtaani tunamwangalia tu huku hospitali watu wanakufa kwa kukosa dawa, hiyo sio kwa Serikali yangu.

"Pale Ikulu nitachimba bwawa la mamba na wale mafisadi wote watadumbukizwa, huko kuliwa hadi kuisha na nguo zake mtazikuta zimewekwa hapo kama ushahidi wa hilo kujua kuna mtu alidumbukizwa humo.

"Pia, hiki kirungu changu nilichoshika mkononi kitatumika kuwapiga kabla hawajaingia ndani ya bwawa hilo na kama nina ziara nje ya nchi siku hiyo nitaiahirisha hadi nihakikishe nimemshughulikia fisadi huyo," amesema mgombea huyo.


Afya, elimu

Akizungumzia sekta ya afya, mgombea urais wa AAFP, Mwiru amesema haiwezekani kituo cha afya kukosa dawa ilhali kina miundombinu ya kutolea huduma, akieleza kuwa hali hiyo inaonesha ukosefu wa mipango madhubuti katika mfumo wa afya.

Ameahidi iwapo chama chake kitapewa ridhaa ya kuongoza nchi, ndani ya mwaka mmoja, Serikali yake itawalipa fidia wananchi waliopo karibu na zahanati au hospitali ili kupisha ujenzi wa nyumba za watumishi wa afya, ambao watakaopangiwa nyumba hizo wataendelea kuishi humo hadi watakapostaafu.

"Haiwezekani mtu afike hospitali hamkuti muhudumu kisa tu anakaa mbali, nitahakikisha kunakuwa na nyumba za wahudumu za kutosha na wanapatika saa zote," amesema.

Elimu

Aidha, Mwiru amesema Serikali yake itashughulikia changamoto zinazowakabili walimu, akieleza kuwa ni watu waliowalea na kuwafundisha viongozi wote wa taifa, lakini leo hii wanaishi katika mazingira magumu.

“Walimu wamejenga misingi ya Taifa hili kwa elimu waliyoitoa, lakini bado maisha yao ni ya shida. Serikali yangu itahakikisha wanapata heshima na masilahi wanayostahili,” amesema.

Vilevile, hakusita kugusia hali ya askari wa Jeshi la Polisi, akieleza kuwa licha ya wao kuwa walinzi wa usalama wa wananchi na mali zao, mishahara yao haizingatii uzito wa majukumu waliyonayo.

“Askari wetu wanafanya kazi ngumu sana ya kulinda nchi, lakini mishahara yao ni midogo mno. Nitahakikisha wanapewa masilahi bora yanayowiana na kazi yao,” amesema Mwiru.


Katiba mpya

Pia, Mwiru amegusia suala la upatikanaji wa Katiba mpya, akieleza kuwa endapo atachaguliwa kuwa Rais, hatokimbilia mchakato wa Katiba mpya bila kuandaa wananchi ipasavyo.

Amesema hatua ya kwanza itakuwa ni kuanzisha madarasa ya elimu ya uraia ili kuwaelimisha wananchi kuhusu Katiba iliyopo sasa pamoja na ile iliyopendekezwa.

Kuhusu utawala bora alisema baraza lake la mawaziri halitazidi watu 15 ili kubana matumizi, lakini wakati huohuo watafanya kazi kama watu 200 kwa kuwa wanachohitaji ni kuwaletea maendeleo ya haraka wananchi.

Amesema kwa kuwa ana uhakika Oktoba mwaka huu anachukua nchi, waliopo chama tawala wasiogope kwa kuwa katika Serikali yake atafanya kazi na vyama vyote ilimradi tu mtu huyo alikuwa mzalendo.

"Nawaambia chama tawala wasiniogope, kwani nitashirikiana nao kwa wale waliokuwa wazalendo, nitawaingiza katika Serikali yangu ili tuwaletee wananchi maendeleo nikiamini maendeleo hayana chama," amesema.

Kwa upande wake mgombea mwenza, Chumu Abdallah amesema wametembelea Wilaya ya Temeke kuona changamoto zinazowakabili wananchi na kubaini mengi.

Chumu ameahidi endapo watachaguliwa watafanyia mambo mengi yatakayobadilisha nchi.

"Katika ziara yetu hiyo tumebaini kuna upungufu wa maji, kwenye masoko kina mama wametaka tuwainue kiuchumi. Kwa kweli muda ndio huu wananchi wa kuchagua chama kilicho bora kwani nikiwa makamu wa Rais nitamshauri na kumsimamia Rais kutekeleza yale yote mnayoyataka na tulioahidi wakati wa kampeni," amesema.