Ada-Tadea kuleta mageuzi sekta ya elimu, kutoa posho kwa walimu vijijini
Muktasari:
- Kutokana na changamoto hizo, chama cha Ada-Tadea kimeweka kipaumbele cha kipekee kwenye ilani yake ya uchaguzi ya 2025 – 2030, kikiahidi kuja na mageuzi yenye mwelekeo mpya wa kielimu.
Elimu imeendelea kuwa uti wa mgongo wa maendeleo ya Taifa lolote duniani. Kupitia elimu, jamii hujijengea uwezo wa kushughulikia changamoto za kijamii na kiuchumi, huku ikiboresha mustakabali wa vijana wake.
Hata hivyo, changamoto za walimu na mfumo wa elimu kwa ujumla zimekuwa zikisababisha matokeo yasiyoridhisha katika maeneo mengi ya nchi.
Walimu mara nyingi wamekuwa wakihusishwa na changamoto za kipato duni, mazingira magumu ya kazi na ukosefu wa makazi bora. Hali hiyo imeathiri ari yao ya kufundisha na mara nyingine imeathiri moja kwa moja kiwango cha elimu kinachotolewa kwa wanafunzi.
Kwa miaka mingi, sekta ya elimu imekuwa ikihitaji mageuzi ya kina yanayolenga kumthamini mwalimu kama mhimili wa elimu bora.
Ni kutokana na changamoto hizo ambapo chama cha Ada-Tadea kimeweka kipaumbele cha kipekee kwenye ilani yake ya uchaguzi ya 2025 – 2030, kikiahidi kuja na mageuzi yenye mwelekeo mpya wa kielimu.
Mageuzi hayo yanajikita katika kuboresha maslahi ya walimu, kuimarisha ukaguzi wa shule, kuhusisha wazazi katika maendeleo ya shule na kupanua wigo wa elimu ya ujuzi kwa vijana.
Kwa mujibu wa ilani hiyo, Ada-Tadea inalenga kuondoa dhana ya elimu kuwa ni nadharia pekee na badala yake kuibua mfumo utakaowajenga vijana katika ubunifu, michezo, sanaa na ujuzi wa kujitegemea. Hatua hii inalenga kutengeneza jamii shirikishi na bunifu, inayotumia elimu kama chachu ya maendeleo ya Taifa.
Maslahi ya walimu
Ada-Tadea inatambua kwamba bila kumthamini mwalimu, hakuna mageuzi ya kweli ya elimu yatakayofanikishwa, hivyo ilani yake imejikita katika kuangalia upya viwango vya kuajiri na kusajili walimu nchini, ili kuhakikisha mfumo wa ajira unakuwa wa haki na unaozingatia ubora.
Moja ya motisha kubwa iliyotolewa ni posho maalumu kwa walimu wanaopangiwa maeneo yenye changamoto kubwa. Walimu watakaohudumu vijijini au maeneo yenye mazingira magumu watahakikishiwa posho ya nyumba, na Serikali itaharakisha ujenzi wa makazi ya walimu.
“Walimu ambao wanapangiwa kwenye maeneo yenye changamoto nyingi watapewa posho maalumu, ikiwemo posho ya nyumba (accommodation allowance). Hivyo, Serikali itahakikisha nyumba za walimu zinajengwa haraka kwenye maeneo ambayo ni vigumu kufikika na yenye mazingira magumu,” inaeleza ilani hiyo.
Hatua hiyo inalenga kuondoa changamoto ya makazi na kuwapa walimu mazingira rafiki ya kuishi na kufundisha.
Mwalimu wa shule ya sekondari moja mkoani Morogoro, Grace Mnyang’anyi anasema iwapo chama hicho kitatekeleza ahadi ya kujenga nyumba na kutoa posho za makazi, hali hiyo itawapa walimu moyo na ari ya kufanya kazi kwa bidii, kwani watakuwa wameondokana na changamoto zinazowaondolea utulivu wa kiakili.
“Kukosa nyumba za walimu ni tatizo kubwa kwetu hasa vijijini. Wakati mwingine mwalimu analazimika kuishi mbali na shule na kutumia muda mwingi barabarani. Kama chama hicho kikipata dhamana ya kuongoza, isiwe maneno matupu bali ni utekelezaji,” anasema Grace.
Kuimarisha ukaguzi wa shule
Katika eneo la ukaguzi wa shule, ilani yao inaeleza kuwa ukaguzi wa shule umekuwa sehemu dhaifu kwa muda mrefu, ambapo mara nyingi umekuwa wa vitabu pekee bila kuangalia hali halisi ya walimu na wanafunzi.
Ada-Tadea inasema mfumo huo utaangaliwa upya na kuboreshwa, ili kuhakikisha unaleta tija. Ukaguzi utajikita si tu kwenye mwenendo wa kitaaluma, bali pia maisha ya walimu, mazingira ya shule na uwajibikaji wa wanafunzi. Lengo ni kuweka mfumo utakaosaidia kubaini changamoto mapema na kuzitatua kabla hazijawa kikwazo kikubwa.
Ushirikishwaji wa wazazi
Ili elimu iwe ya matokeo, wazazi hawawezi kuepushwa na jukumu. Ada-Tadea inasisitiza katika ilani yake kuwa wazazi watahusishwa moja kwa moja katika kamati za maendeleo ya shule na kamati ndogo ndogo zinazojenga mazingira bora ya elimu.
Kupitia ushirikishwaji huo, wazazi watatoa utaalamu na weledi wao katika kuboresha shule, huku pia wakifuatilia maendeleo ya watoto wao kwa karibu. Hatua hii inalenga kuongeza kiwango cha nidhamu, ari ya kujifunza na ushirikiano wa kijamii.
“Ukaguzi wa shule utaangaliwa upya na kuboreshwa ili kujua hali ya walimu na wanafunzi ikoje na kama wanawajibika. Tutahakikisha wazazi wanajihusisha na wanafunzi, ikiwemo kushiriki kwenye kamati za maendeleo ya shule na kamati zake ndogo. Hii itasaidia kuleta utaalamu na weledi mbalimbali walionao wazazi. Hali hiyo itaongeza kiwango cha elimu kwa shule.”
Godfrey Mkwizu, mwalimu wa shule ya msingi mkoani Shinyanga anasema: “Kukosekana kwa vifaa vya kufundishia ni tatizo linalotuathiri. Kuna wakati tunalazimika kufundisha somo bila vitendea kazi vya kutosha. Hali hii inawafanya wanafunzi washindwe kuelewa kwa vitendo na matokeo yake kushuka.”
Anasema mageuzi yaliyopendekezwa na Ada-Tadea ya kuimarisha ukaguzi wa shule na kushirikisha wazazi yanaweza kusaidia kupunguza changamoto hizo.
“Tukishirikiana na wazazi, vifaa vya shule na mazingira vinaweza kuboreshwa. Wazazi wakiwa sehemu ya suluhisho, mwalimu atabaki kufundisha kwa utulivu na wanafunzi watanufaika,” anasema Mkwizu.
Elimu ya ujuzi kwa vijana
Moja ya mageuzi makubwa yanayoahidiwa ni kuondoa dhana ya elimu kuwa ya nadharia pekee. Ada-Tadea inalenga kuimarisha elimu ya ujuzi kwa vijana kwa kuwapa nafasi ya kujifunza utafiti, ubunifu, utengenezaji na uuzaji wa bidhaa.
“Chama kitarekebisha na kuboresha mfumo wa elimu kutoka kwenye dhana hadi kwenye utendaji, kiasi ambacho elimu ya ujuzi itapewa umuhimu wa hali ya juu, ambapo vijana wengi zaidi watapelekwa kujifunza elimu ya ujuzi wa utafiti, ubunifu, utengenezaji na uuzaji wa bidhaa.”
Ilani hiyo inaeleza kwamba fedha zitatengwa kwa malengo maalumu na ujuzi maalumu kwa kufanikisha kitu maalumu kwa manufaa ya maendeleo ya uchumi wa Taifa.
Mafunzo hayo yataelekezwa kwenye miradi yenye kuchochea ukuaji wa mapato ya vijana na jamii husika, kufanikisha suala la ajira kwa vijana wa Kitanzania.
Naye, Mwalimu Paulo Mhando wa shule ya msingi mkoani Mtwara, anasema mageuzi ya elimu yanayolenga kuongeza ujuzi na kuimarisha mfumo wa elimu ni mwanga mpya.
“Kama Serikali kupitia Ada-Tadea itatupunguzia mzigo huu kwa kuongeza walimu na kuimarisha elimu ya vitendo, basi tutajenga kizazi chenye uelewa mpana na uwezo wa kujitegemea. Hii ndiyo elimu tunayohitaji kwa Tanzania ya leo,” anasema Mhando.
Kuthamini vipaji
Elimu ya Tanzania imekuwa ikijikita zaidi kwenye masomo ya kawaida, huku vipaji vya michezo, muziki, sanaa na uigizaji vikipewa nafasi ndogo. Ada-Tadea inalenga kubadili mtazamo huo kwa kuingiza vipaji hivi katika mfumo rasmi wa elimu.
Walimu wabobezi katika nyanja mbalimbali wataandaliwa na vifaa stahiki vitatolewa ili wanafunzi wenye vipaji waendelezwe. Hii italeta mageuzi ya kijamii, kwani Taifa litazalisha wanamichezo, wasanii na wabunifu watakaotambulika kitaifa na kimataifa.