Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ahadi ya Chaumma siku 100 za kwanza madarakani

Muktasari:

  • Chaumma imeahidi kufanya mageuzi mbalimbali ya kimfumo, kisheria na hata kimuundo ili kuhakikisha inasukuma mbele maendeleo ya Taifa na kuboresha hali ya maisha ya Watanzania nchini

Dar es Salaam. Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), kimejitofautisha na vyama vingine vinavyoshiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, kwa kuangazia mambo kitakayoyafanya ndani ya siku 100 za kwanza kikiingia madarakani.

Chama hicho kimeahidi kufanya mageuzi mbalimbali ya kimfumo, kisheria na hata kimuundo ili kuhakikisha kinasukuma mbele maendeleo ya Taifa na kuboresha hali ya maisha ya Watanzania wote nchini.

Ilani hiyo imezingatia maoni ya wadau mbalimbali kwenye jamii, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG), mikataba na matamko mbalimbali ya kimataifa ambayo Tanzania imeridhia.

Ilani hiyo pia, inalenga kuuhamasisha umma ili kuwa na mkakati wa pamoja wa kukabiliana na changamoto zilizopo mbele yao kama Taifa, kuwaangamiza maadui watatu wa zamani na wale wapya waliotengenezwa na tabaka la watawala.

“Ilani yetu inalenga kuiongoza Serikali kwenda kutumia rasilimali za Taifa zilizopo kwa manufaa ya kila mmoja wetu, kwa kuwa tunatambua kama Taifa tuna jamii inayotofautiana katika ziada lakini yenye usawa katika mahitaji ya msingi,” inaeleza ilani hiyo ya Chaumma.


Siku 100 madarakani

Endapo itapewa ridhaa na wananchi kuunda Serikali, Chaumma imeahidi kuwasilisha bungeni muswada wa sheria kwa ajili ya kukamilisha mchakato wa kuandika Katiba mpya.

Muswada utapendekeza kuundwa kwa tume kwa ajili ya kuratibu na kuandika rasimu ya Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Pia, tume hiyo itaundwa kwa kuvihusisha vyama vyote vya siasa, taasisi za dini, asasi za kiraia na makundi mengine ya kijamii ili kupata Katiba bora na hatimaye kupigiwa kura ya maoni na wananchi.

Chaumma inaahidi kuwasilisha bungeni muswada wa kuundwa Tume ya Ukweli na Upatanishi ikiwamo kufanya uchunguzi wa malalamiko mbalimbali ya wananchi kuhusu ulipwaji wa fidia wa ardhi na mali mbalimbali zilizotwaliwa na Serikali, mauaji, utekaji na kupotea kwa wananchi, kubambikiwa kodi au kesi za jinai hasa za uhujumu uchumi na malalamiko mbalimbali ya wafanyabiashara.

Chama hicho kinaahidi kuunda Tume ya Ardhi kuchunguza mgogoro wa wananchi na mamlaka za Uhifadhi za Taifa za Wanyamapori na mamlaka nyingine zinazohusika na masuala hayo ili kuondoa tatizo la mauaji ya wananchi wanaoishi au kupakana na mamlaka za wanyamapori au mamlaka za misitu.

Aidha, tume hiyo itachunguza migogoro ya wakulima na wafugaji ambayo kwa muda mrefu imelitafuna Taifa katika maeneo mbalimbali nchini bila kuwa na ufumbuzi wa kudumu.

Chaumma inakusudia kuanzisha na kuzindua mkakati wa mfumo bora wa lishe nchini kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wote wanapata lishe bora kuanzia kwa watoto wadogo katika ngazi ya elimu ya awali, wanafunzi shuleni na wagonjwa katika hospitali za umma.

“Mkakati huu utaitwa ‘ubwabwa kwa wote’ kuboresha mfumo wa lishe ni kuhakikisha kwamba, Taifa linaondokana na magonjwa yanayotokana na ukosefu wa lishe nchini,” inaeleza ilani hiyo ya Chaumma.

Vilevile, inakusudia kuwasilisha bungeni muswada wa kufuta tozo zote zinazoathiri sekta ya kilimo na ufugaji, tozo hizo zimeathiri mapato kwa wakulima na upatikanaji wa chakula bora na nyama nchini jambo litakalorudisha nyuma mkakati wa upatikanaji wa ubwabwa kwa wote.

Ilani ya Chaumma inakusudia kutunga sheria ya kuhuisha mfumo mzima wa Serikali za mitaa, kimuundo na kimapato.

Hatua hiyo italenga kufanya marekebisho ya utaratibu wa tozo na mapato ya halmashauri na Serikali kuu ili kuziwezesha halmashauri kukusanya mapato na kujiendesha bila kutegemea ruzuku kutoka Serikali Kuu.

Aidha, Chaumma kupitia muswada huo wa sheria, inakusudia kuhuisha mfumo mzima wa Serikali za mitaa na halmashauri ikiwamo kuziunganisha halmashauri za wilaya au manispaa ambazo hazina uwezo wa kujiendesha.

“Serikali ya Chaumma itatunga sheria ya matumizi ya akili mnemba katika shule na vyuo bila kuathiri masuala ya ubunifu na uwezo wa kufikiri upya wanafunzi ili kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknojia yanayokua kwa kasi ulimwenguni.

“Sheria hiyo itakuwa kwa ajili ya maendeleo ya watu wote na sio kutumika kuwaadhibu watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini,” inasomeka sehemu ya ilani hiyo inayolenga kukuza uchumi, maisha endelevu na kupunguza umaskini wa kipato.


Waichambua ilani

Akizungumzia ahadi ya Chaumma katika siku 100, mchambuzi wa siasa, Gilbert Msoma amesema ni jambo zuri kwa chama hicho kuangazia mipango yake katika siku 100 za kwanza, hata hivyo hadhani kama mambo makubwa ya kubadilisha mfumo yanaweza kufanyika ndani ya siku hizo 100.

Anasema Tanzania inahitaji mabadiliko makubwa ya kimuundo na kimfumo, jambo linalohitaji muda wa kutosha ili kufanikisha hilo na kuyafanya maisha ya Watanzania kuwa yenye furaha na maendeleo.

“Ilani zote za vyama, zina mambo mazuri kwani zimeakisi mahitaji halisi ya wananchi, kinachohitajika sasa ni watakaopewa dhamana kuhakikisha wanabeba masilahi ya wananchi na siyo kupigania masilahi yao binafsi,” anasisitiza.

Msoma anasema chama kitakachoshinda uchaguzi kisipate kigugumizi kuchukua mambo mazuri kutoka kwenye ilani za vyama vingine kwa kuwa, kufanya hivyo ni kwa lengo la kuboresha na kujenga mustakabali mwema wa Taifa.

“Maendeleo ni nguzo muhimu katika Taifa lolote, hata hivyo wananchi wanahitaji kuwa na furaha. Vipimo vya furaha vinaonesha kiwango chetu kiko chini, hivyo ni jukumu la viongozi wetu kuhakikisha tunakuwa jamii yenye furaha,” anasema mchambuzi huyo.

Buberwa Kaiza, anasema ilani ya Chaumma imebainisha kufanya mabadiliko ya sheria na kuunda tume zitakazosimamia mambo ya msingi kama ardhi, jambo linalofaa kuigwa na vyama vingine.

“Chaumma ni chama kichanga, kwa maana ya kuanzishwa kwake, hata hivyo mwaka huu kimekuja kivingine kwa kuandaa ilani inayoeleza namna itakavyoongoza Serikali yake kwa misingi ya utawala bora na kwa nguvu ya umma,” anasema Kaiza.

Pia, anasisitiza kwamba Watanzania wanapenda kuona mambo yao yanasikika na kufanyiwa kazi na wale waliopewa dhamana, lakini kwa bahati mbaya watawala wamekuwa mwiba mkali kwa wananchi wanaowaongoza, jambo linalojenga uhasama na matabaka baina yao.

“Tukubali kwamba, mambo hayako sawa hapa nchini, hata ilani ikiwa nzuri vipi, kama hakuna utashi wa kisiasa wa kubadilisha hali hii, tutaendelea kuwa vilevile. Tunahitaji viongozi wenye uchungu na maisha ya wananchi wanaowaongoza,” anasema Kaiza.