Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Benki ya CRDB kukuza vipaji vya Ndondo Cup kupitia Imbeju Football Academy 

Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa (kushoto) akimkabidhi tuzo ya mchezaji bora wa mechi ya ufunguzi wa Imbeju Ndondo Cup Ardason Chawaka wa  Madenge FC katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa KMC jijini Dar es Salaam juzi. 

Dar es Salaam. Benki ya CRDB imetangaza mpango wa kuanzisha kituo maalum kitakacholenga kuibua, kukuza na kuendeleza vipaji vya wachezaji wa soka wanaong'ara katika mashindano ya Imbeju Ndondo Cup (Imbeju Football Academy), ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuwapa fursa ya kufikia soka la ushindani ndani na nje ya nchi.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa, baada ya mchezo wa ufunguzi wa msimu wa 13 wa Imbeju Ndondo Cup uliochezwa kwenye Uwanja wa KMC, Dar es Salaam, ambapo Madenge iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mzimuni.

Tully alisema benki hiyo imevutiwa na mwitikio mkubwa wa mashabiki waliojitokeza kushuhudia mchezo huo pamoja na kiwango kizuri kilichoonyeshwa na wachezaji.

Alisema uwekezaji wa Sh400 milioni uliofanywa na benki hiyo katika mashindano hayo unalenga kuwapa nafasi vijana wenye vipaji ambao mara nyingi hukosa fursa ya kuonekana na vilabu vikubwa.

"Nimefurahishwa na mwitikio mkubwa wa mashabiki waliofurika katika Uwanja wa KMC, lakini kikubwa zaidi ni kiwango cha wachezaji walichokionyesha katika mchezo wa ufunguzi," alisema Tully.

"Nitazungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dkt Abdulmajid Nsekela, kuhusu kuanzishwa kwa Imbeju Football Academy au CRDB Foundation Academy ili kuendeleza vipaji vya wachezaji hawa na kuwapa fursa ya kufikia viwango vya juu zaidi," aliongeza.

Alisema kupitia mashindano hayo, CRDB Bank Foundation inalenga kutumia michezo kama nyenzo ya kuwawezesha vijana kiuchumi na kuwafungulia milango ya ajira.

"Michezo ni ajira na afya. Kwetu sisi CRDB Bank Foundation, ndoto yetu ni kuchochea ubunifu na kuwawezesha vijana kujiajiri. Tunataka kuona wachezaji hawa wakicheza katika ligi kubwa hapa nchini na hata nje ya Tanzania," alisema.

Katika mchezo huo, bao pekee la Madenge, iliyokuwa chini ya kocha Idd Moshi, lilifungwa na Fadhil Nado dakika ya 39, huku Ardason Chawaka akichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mechi.
Katika mchezo huo, timu ya Mzimuni, iliyokuwa ikinolewa na  mchezaji wa zamani wa Yanga, Athumani Idd 'Chuji', ilishindwa kuhimili kasi ya wapinzani wake licha ya kumtumia kiungo mpya wa Yanga, Juma Issa Abushiri, aliyejiunga na timu hiyo akitokea Fountain Gate FC.

Mchezo wa ufunguzi ulihudhuriwa na wachezaji mbalimbali wa Ligi Kuu Tanzania Bara na ligi nyingine, akiwemo nyota wa zamani wa Yanga, Mkoko Tonombe. Pia, Afisa Mtendaji Mkuu wa Baraza la Michezo la Botswana, Olebile Sikwane, alihudhuria kushuhudia uzinduzi wa mashindano hayo.

Mbali na uwekezaji wa Sh400 milioni katika maandalizi na uendeshaji wa mashindano, CRDB pia imetenga zaidi ya Sh100 milioni  kwa ajili ya zawadi mbalimbali.

Bingwa wa msimu wa 13 wa Imbeju Ndondo Cup 2026 atajinyakulia Sh30 milioni, huku mshindi wa pili akiondoka na Sh20 milioni, katika hatua inayolenga kuongeza ushindani na motisha kwa timu zinazoshiriki.