CCM ilivyokusanya Sh86.5 bilioni ndani ya saa 24
Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM), kimesema mbali na fedha za kampeni za uchaguzi mkuu 2025, harambee kiliyoianzisha inalenga pia kukusanya fedha za shughuli za ujenzi wa chama hicho.
Harambee hiyo ilitangazwa jana Jumatatu, Agosti 11, 2025 na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Emmanuel Nchimbi, akisema wanalenga kukusanya Sh100 bilioni kutoka kwa wadau, wafuasi, makada na washabiki wa CCM.
Kwa mujibu wa mtendaji mkuu huyo, fedha hiyo mbali na makundi ya makada, pia inalenga kupokelewa kutoka hata kwa wafuasi wa vyama vya upinzani.
Ufafanuzi kuhusu malengo ya harambee hiyo, umetolewa usiku wa leo Jumanne, Agosti 12, 2025 na Dk Nchimbi wakati wa harambee hiyo inayofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.
Amesema chimbuko la harambee hiyo ni ombi la wanachama wa CCM Mei 28, 2025 walipotaka wapewe nafasi ya kuchangia ujenzi wa Ofisini ya Makao Makuu ya chama hicho jijini Dodoma.
Ameeleza hilo lilifanyika siku ambayo Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan alikuwa anaweka jiwe la msingi la ujenzi wa ofisi hiyo, jijini humo.
Kutokana na maombi hayo ya wanachama, amesema alifikishiwa Rais Samia na akashauri kwa kuwa kuna suala la uchaguzi na ujenzi wa chama hicho, haitawezekana ziitishwe harambee mbili ndani ya muda mchache.
Amesema mwenyekiti huyo alishauri iandaliwe harambee moja itakayofanikisha michango ya fedha kwa ajili ya shughuli za kampeni za uchaguzi ndani ya chama hicho na ujenzi wa CCM.
"Kamati Kuu ikajadili na kuona wana-CCM wana haki ya kuchangia shughuli za chama chao. Ni michanuo ya kampeni na shughuli za chama. Kwa hiyo ni uamuzi wa Kamati kuu kuruhusu kufanyika kwa harambee hii," amesema.
Amesema uimara wa chama hicho utatokana na kuwa na nguvu ya kushiriki uchaguzi na kuunda dola na hatimaye.
Kwa upande wake, Rais Samia ameweka msisitizo kwa wadau kuchangia kwa maendeleo ya chama hicho, kadhalika kuiwezesha CCM izunguke kwenye kampeni za uchaguzi kwenda kuomba ridhaa ya kushika dola kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Amesema ni muhimu kuchangia, huku akiwashukuru viongozi, wasanii na wahudhuriaji mbalimbali wa shughuli hiyo.
Rais Samia aliongoza wachangiaji wa harambee kwa kuchangia Sh100 milioni.