Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chaumma yaahidi neema ya viwanda vya viuatilifu, mbolea

Muktasari:

  • Asema chama hicho kikishika madaraka na kuunda Serikali, wakulima watanunua mbolea kwa Sh20,000, wakati kwa sasa mbolea yenye ruzuku ya Serikali ni wastani wa Sh70,000 na isiyo na ruzuku ni takribani Sh130,000.

Igalula. Mgombea mwenza wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Devotha Minja, ameahidi ujenzi wa viwanda vingi vya viuatilifu na mbolea, endapo chama hicho kitapatiwa ridhaa ya wananchi ya kuunda Serikali.

Minja amesema chama hicho kimedhamiria kujenga viwanda ili kilo 50 ya mbolea iuzwe kwa Sh20,000 au pungufu zaidi.

Mgombea mwenza huyo amesema hayo leo Jumanne, Septemba 9, 2025, alipozungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Mswaki, Jimbo la Igalula, mkoani Tabora.

Minja anaendelea kuzisaka kura za Chaumma akiomba uungwaji mkono, wananchi wapige kura za ndiyo kwa wagombea wa Chaumma kwa nafasi ya urais, ubunge  na udiwani, Oktoba 29, 2025.

Amesema hali si nzuri nchini, kwani Tanzania inategemea kilimo, Chaumma kina ilani inayotilia mkazo kilimo kwa kuwa kinaweza kubadili maisha ya wananchi wengi, kwani gharama za kuendesha kilimo zitapungua iwapo chama hicho kitaruhusiwa kuunda Serikali.

"Gharama inakuwa juu kutokana na kodi kwenye viwanda vya mbolea na viuatilifu. Chaumma, tukiingia madarakani, tutakuja na mkakati wa kujenga viwanda vingi vya mbolea, kuondoa kodi ili watu waingie kwenye kilimo," amesema Minja.

Amesema mbolea yenye ruzuku ya Serikali ni zaidi ya Sh100,000, lakini chini ya Chaumma bidhaa hiyo muhimu kwa wakulima itauzwa kwa Sh20,000 au pungufu. Kwa wale ambao hawatakuwa na uwezo kununua mbolea, Minja amesema Serikali itabeba mzigo wa kuhakikisha wanapata huduma hiyo.

Kuhusu viuatilifu, mgombea mwenza amesema Serikali yao itawekeza katika ujenzi wa viwanda vya ndani ili kudhibiti upotevu wa mazao unaosababishwa na wadudu.

Akizungumzia sekta ya ardhi, Minja ameahidi kuwa kila mwananchi atamilikishwa ardhi bure.

Amesema hatua hiyo itarahisisha ukusanyaji wa kodi na pia kuwawezesha wakulima kupata mikopo. Amesema hivi sasa wakulima wengi hawawezi kukopesheka kutokana na kutegemea kilimo cha mvua kisicho na uhakika. “Tutawezesha kilimo chenye tija ili wakulima wakopesheke,” amesema.

Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Jimbo la Igalula kupitia Chaumma, Omary Juma, ameahidi kushughulikia kero ya ubinafsishaji wa hifadhi unaoendelea mkoani humo bila wananchi kushirikishwa.

Aidha, amesema endapo atapatiwa ridhaa ya wananchi, atahakikisha kunajengwa soko, kituo cha kisasa cha daladala na barabara kwa kiwango cha lami, akisisitiza kuwa chama chake ndicho pekee kitakachowaletea wananchi hao mabadiliko ya kweli.