Mwalimu: Jamii jirani na hifadhi zitafaidika na rasilimali
Muktasari:
- Mgombea urais wa Chaumma, Salum Mwalimu ameahidi kuruhusu wananchi kupata kitoweo kwa njia halali ili kupunguza ujangili. Pia amelalamikia ukali wa askari na mfumo unaochochea chuki kati ya wananchi na mamlaka.
Mara. Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu, ameahidi kuanzisha utaratibu maalumu wa kuzisaidia na kuzinufaisha jamii zinazozunguka hifadhi za Taifa endapo atachaguliwa kuunda Serikali baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Akizungumza leo Septemba 9, 2025 na wananchi wa Kijiji cha Ikoma, kilichopo mpakani mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Mwalimu amesema kuwa Serikali yake itaondoa mifumo kandamizi inayowanyima wananchi haki ya kunufaika na rasilimali asilia walizopewa na Mwenyezi Mungu.
Amesema moja ya mikakati yake ni kuruhusu wananchi wa maeneo hayo kupata kitoweo kama swala kwa njia halali na iliyodhibitiwa, jambo analoliona kama njia ya kupunguza ujangili unaozidi kuongezeka.
“Wananchi wakitaka kupata kitoweo wanaishia kupigwa risasi kwa neema ambayo Mwenyezi Mungu alikuwa amewaruzuku. Hivi niwaulize wale wanaoishi karibu na Ziwa Victoria wanazuiliwa kwenda kuvua sangara na sato? Yaani wao wakavue sangara na sato, nyie mpigwe risasi?” amedai Mwalimu.
Akiwa anatokea Karatu, mkoani Arusha ambako alifanya mikutano ya kampeni kuomba kura, Mwalimu amelalamikia mfumo wa sasa wa usimamizi wa maliasili, akidai kuwa unazua chuki kati ya wananchi na mamlaka badala ya kuhimiza ushirikiano na ushirikishwaji wa jamii katika kulinda rasilimali hizo.
“Utaratibu wa sasa ni kunyanyasa wananchi badala ya kuwapa fursa ya kushiriki ulinzi wa hifadhi na kunufaika na urithi wa Taifa. Hii siyo haki,” amesema.
Mkazi wa Ikoma, Meshack Mwita, ameunga mkono kauli hiyo akieleza kuwa kuishi jirani na hifadhi ni sawa na laana kutokana na ukali wa askari wa wanyamapori na migogoro ya ardhi isiyopatiwa ufumbuzi wa kudumu.
“Askari wamekuwa wakali kupita kiasi. Ukijichanganya kidogo, maisha yako yanakuwa hatarini. Jamii zetu zinakumbwa na shida kubwa hasa migogoro ya ardhi,” amesema Mwita.
Hata hivyo, Mwalimu ameahidi kuwa Serikali ya Chaumma itaweka utaratibu wazi na wa shirikishi ili kuhakikisha jamii zinazozunguka hifadhi zinajumuishwa kikamilifu katika mfumo wa ulinzi wa maliasili, huku zikifaidika moja kwa moja na rasilimali hizo.