Mgombea urais Chaumma aahidi kuwalinda wafugaji, kukuza utalii
Muktasari:
- Mgombea huyo, Salum Mwalimu, ameahidi kulinda haki za wafugaji kwa kuhakikisha wanapata malisho na hawadhulumiwa. Pia ameahidi kuondoa vikwazo vinavyokwamisha Watanzania sekta ya utalii, ikiwemo masharti ya gari la kifahari kwa waombaji wa leseni.
Moshi. Mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu, ameahidi kulinda haki za wafugaji na kuondoa vikwazo vinavyowakwamisha Watanzania katika sekta ya utalii, endapo atachaguliwa kushika wadhifa huo.
Akizungumza katika mikutano miwili ya kampeni iliyofanyika Makuyuni na Soko la Jumapili, Monduli mkoani Arusha, leo Septemba 7, 2025, Mwalimu amesema Serikali yake itahakikisha mifugo inapata maeneo ya malisho na wafugaji hawabughudhiwi kama ilivyo sasa.
“Haiwezekani mifugo igeuke kuwa laana badala ya baraka. Nikiwa Rais, jambo hili halitakuwepo. Haiwezekani tembo anufaike, lakini Mtanzania mwenzangu ateseke kwa kukosa sehemu ya malisho,” amesema Mwalimu.
Katika sekta ya utalii, Mwalimu ameahidi kufanya mageuzi ya kisera na kisheria kwa kuondoa masharti kandamizi, ikiwemo lile linalowataka waombaji wa leseni za utalii kumiliki gari lenye thamani ya kuanzia Sh150 milioni.
“Utalii ni fursa yetu Watanzania. Haiwezekani wazungu na Wahindi wanakuja kunufaika, halafu sisi tunazuiwa kwa kuwa hatuna magari ya kifahari. Hili nitaliondoa. Kama una pikipiki, fanya kazi hiyo. Baada ya miaka mitatu, utapewa leseni kamili,” amesema.
Amesema urithi wa Taifa katika sekta hiyo haipaswi kuwanufaisha wageni pekee, huku wananchi wa kawaida wakiachwa nyuma kwa sababu ya vigezo visivyotekelezeka.
Mwalimu pia aligusia maono ya hayati Edward Lowassa, aliyekuwa Waziri Mkuu na Mbunge wa Monduli, akisema yuko tayari kuyaendeleza na kuyatetea akiwa Rais.
“Lowassa alikuwa na maono makubwa ya kuendeleza nchi hii. Alipohama CCM mwaka 2015, alikuwa akipigania mabadiliko. Wana-Monduli msikubali maono yake yapotee. Nipo tayari kuyaendeleza,” amesema.
Kwa upande wake, Leah Kweka, mgombea ubunge wa Chaumma jimboni Monduli, ameahidi kupigania huduma bora za maji, barabara na kuboresha miundombinu ya Soko la Jumapili.
“Wapo watu hawajaoga kwa siku tatu kwa sababu ya ukosefu wa maji. Nikichaguliwa nitapigania hili bungeni. Tutajenga vyoo bora na kuboresha mazingira ya wafanyabiashara,” amesema Kweka.
Uchaguzi Mkuu wa Tanzania umepangwa kufanyika Jumatano, Oktoba 29, 2025, ambapo vyama 17 vya siasa vimesimamisha wagombea wa nafasi mbalimbali, kuanzia udiwani hadi urais.