CUF kufumua mfumo wa Mahakama, ajira za majaji
Muktasari:
- Katika ilani hiyo, CUF imeahidi kuubadili mfumo wa utoaji haki na ajira za watendaji wa Mahakama na kubadili kutoka majaji kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hadi kuajiriwa na Kamisheni ya Ajira za Mahakama.
Moshi. Ni kama hakuna eneo ambalo halijaiguswa, ilani ya uchaguzi ya Chama cha Wananchi (CUF) ya miaka mitano (2025-2030) imekuja na ahadi ya kuufumua mhimili wa Mahakama ikiwamo ajira za majaji wa Mahakama Kuu.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii, wamepongeza ilani hiyo ya CUF wakisema itasaidia mhimili wa Mahakama kuwa na uhuru ambao wananchi wanautamani na kuwa na chombo huru cha kushughulikia haki za binadamu.
Mchambuzi huru wa siasa safi, uongozi na usalama, Sam Temu anasema ilani ya CUF inalenga kupunguza uteuzi wa kisiasa na kuongeza uhuru wa Mahakama.
Hata hivyo, anasema kamisheni ya ajira inahitaji kuwa na uwazi.
Katika ilani hiyo, CUF imeahidi kuubadili mfumo wa utoaji haki na ajira za watendaji wa Mahakama na kubadili kutoka majaji kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hadi kuajiriwa na Kamisheni ya Ajira za Mahakama.
Kulingana na Ibara ya 109 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jaji Kiongozi na majaji wengine wa Mahakama Kuu watateuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kushauriana na Tume ya Kuajiri ya Mahakama.
Utaratibu huu unaopendekezwa na CUF hautofautiani na ule uliokuwemo katika Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji Joseph Warioba anayeteuliwa kuwa Jaji, lazima athibitishwe na Bunge.
Katika ilani hiyo, CUF imeahidi kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa kama ilivyo kwa Zanzibar kupitia katiba yao ya 2010, itakayohakikisha unaandaliwa mfumo wa Mahakama utakaompa haki kila mwananchi pasipo kutoa upendeleo wowote.
CUF inasema Idara ya Mahakama itakuwa na uhuru wa kutosha katika kuendesha na kutoa uamuzi wake ambao Katiba mpya itatamka wazi kuwa, Mahakama ndio taasisi yenye uamuzi na usemi wa mwisho juu ya suala lolote la kisheria.
CUF itaandaa Katiba itakayotamka wazi kuwa, ni ukiukwaji wa Katiba kwa Serikali kuvunja agizo, amri au hukumu yoyote ambayo imeshapitishwa na Mahakama.
Itaanzisha mfumo wa kuajiri majaji, wasajili wa Mahakama na mahakimu kupitia Kamisheni ya Aajira ya Watendaji wa Mahakama huku ajira za majaji na wasajili wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani zikihitaji kuthibitishwa na Bunge.
Chama hicho pia kimeahidi ndani ya miaka mitano, kitaboresha masilahi ya watendaji wa Idara ya Mahakama, kuongeza ajira ya watendaji zaidi wenye uwezo na kuanzisha mfumo wa kisasa wa matumizi ya teknolojia uendeshaji wa kesi.
Tume Huru ya Haki za Binadamu
Katika eneo hilo, CUF inasema Serikali yake itarejesha thamani ya utu na haki za kila Mtanzania nchini na inatunga Katiba itakayounda Tume Huru ya Haki za Binadamu yenye uwezo wa kusimamia haki za Watanzania.
Tume itakuwa na jukumu la kuchunguza ukiukwaji wa maadili na haki za binadamu na kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kurudisha haki kwa walionyimwa na kuwafikisha Mahakamani watakaoonekana na makosa ya uvunjaji wa haki hizo.
Mbali na hilo, lakini tume itakuwa na haki ya kuwaita na kuwahoji watuhumiwa wa uvunjifu wa haki za binadamu, bila kuomba ridhaa kwa mtu au taasisi yoyote, ikiwa ushahidi ulioko mbele yake utaonesha ni muhimu kufanya hivyo au baada ya kuombwa kufanya hivyo na mwathirika au mwakilishi wa mwathirika.
“Tume itakuwa huru bila kuwa na mfungamano wowote wa kisiasa, na wajumbe wake watapatikana kwa kuteuliwa kutokana na mapendekezo yatakayotokana na mchakato utakaobainishwa na Katiba mpya na kuidhinishwa na Bunge,” inaeleza ilani hiyo.
“Tume itakuwa madarakani kwa muda wa miaka mitano na kila mwaka itapeleka taarifa ya kazi zake katika Bunge ambako zitawasilishwa na zitajadiliwa.
“Wajumbe wa Tume ya Haki za Binadamu watakaa madarakani kwa vipindi visivyozidi viwili au kama itakavyopitishwa na Bunge.”
Haki za raia
Serikali ya CUF itaanzisha sheria itakayoibana Serikali juu ya mwenendo wa kujitwalia kwa nguvu maeneo ya wananchi bila kuingia katika majadiliano ya kina na hatimaye kufikia makubaliano na wananchi wa eneo husika.
Pia, kupitia ilani hiyo, CUF itaanzisha sheria itayokataza vyombo vya dola kutumiwa na wanasiasa au maofisa wenyewe wa vyombo hivyo kushambulia wananchi wanaoandamana, kugoma au kukusanyika kwa njia za amani.
“Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoongozwa na CUF itaanzisha sheria itakayowataka waajiri wote kuwa na mikataba ya ajira na wafanyakazi wao.
“Tutahakikisha kuwa Katiba mpya inaeleza wazi kuwa vyombo vya habari baada ya kujisajili kama kampuni na kupata leseni ya biashara havitasajiliwa na taasisi nyingine yoyote ya Serikali wala kuwekewa mipaka ya kijiografia,” inaeleza.
Serikali hiyo ya CUF iltahakikisha kuwa, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inakuwa na kifungu kinachoruhusu raia yeyote mwenye sifa stahiki kuwa mgombea katika nafasi ya uchaguzi bila kipitia chama cha siasa
CUF kupitia ilani hiyo wameahidi kuhakikisha masuala ya haki za binadamu yanakuwa ni sehemu ya mitalaa ya somo la uraia shuleni katika ngazi za elimu ya msingi na sekondari kwa madhumuni ya kukuza uelewa juu ya haki za binadamu.
Walichokisema wachambuzi
Mchambuzi huru wa siasa safi, uongozi na usalama, Sam Temu anasema ilani ya CUF inalenga kupunguza uteuzi wa kisiasa na kuongeza uhuru wa Mahakama.
“Mahakama inaweza kuonekana huru zaidi, bila kuonekana kama inadaiwa fadhila kwa Rais. Ninachokiona itahitaji kamisheni yenye uwazi na uwajibikaji mkubwa, vinginevyo inaweza kubadilika kuwa tu mlango mpya wa upendeleo,” anasema.
Kuhusu vyombo vya habari, mchambuzi huyo anasema ilani hiyo, inalenga kurahisisha mazingira ya vyombo vya habari na kupunguza kero za udhibiti wa Serikali.
“Ni hatua muhimu kwa uhuru wa habari, maana mara nyingi taasisi tofauti hutumika kama kikwazo cha kisheria au kisiasa,” anasema mtaalamu huyo.
Mchambuzi mwingine wa masuala ya kisiasa, kijamii na kiuchumi, Edwin Soko ambaye pia ni mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA-TAN), anapongeza mipango hiyo ya CUF akisema ni mizuri.
“Kwa mtazamo wangu mimi, ni mipango mizuri kwa kuwa inafanya mhimili wa Mahakama kuwa huru kwa kuwa, majaji hawatawajibika tena kwa mteule ambaye ni Rais kwa mfumo wa sasa,” anasema.
“Jambo hilo hata wenzetu wa Kenya wanafanya hivyo, ndio maana unaona wana utofauti mkubwa kwa Mahakama zao kuwa huru.”
Kuhusu Tume Huru ya Haki za Binadamu, anasema hilo ni jambo jema na sio jipya sana kwa kuwa, hata tume ya sasa ni huru Kikatiba kwani haipaswi kuingiliwa na mhimili wowote ule.
“Sema kuna marekebisho kidogo yanaweza kuboreshwa hasa kwenye mamlaka ya uteuzi yatoke kwenye mamlaka ya Rais na yabaki kwenye chombo maalumu cha ajira,” anasema mchambuzi huyo.