Daraja la Matete Tarangire larahisisha utalii Tarangire
Mwonekano wa sehemu ya Daraja la Matete lililopo Hifadhi ya Taifa Tarangire ambapo lina urefu wa mita 85.
Muktasari:
- Ujenzi wa Daraja la Matete lenye urefu wa mita 85 katika Hifadhi ya Taifa Tarangire, mkoani Arusha, umetajwa kuwa suluhisho la changamoto za usafiri wakati wa msimu wa mvua na kusaidia kuimarisha shughuli za utalii.
Arusha. Ujenzi wa Daraja la Matete katika Hifadhi ya Taifa Tarangire umeelezwa kurahisisha kwa kiasi kikubwa shughuli za utalii, hasa wakati wa msimu wa mvua ambapo Mto Tarangire hufurika na kuzuia mawasiliano kati ya pande mbili za hifadhi hiyo.
Daraja hilo lenye urefu wa mita 85, lililogharimu Sh1.1 bilioni, limejengwa juu ya Mto Tarangire unaotenganisha upande wa mashariki na magharibi wa hifadhi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Jumamosi, Machi 14, 2026, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Tarangire, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Beatrice Kessy, amesema daraja hilo ni sehemu ya jitihada za Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) kuboresha miundombinu ya utalii nchini.
Amesema daraja hilo limeanza kutumika mwaka huu na tayari limeleta nafuu kubwa kwa watalii na waongoza watalii waliokuwa wakikumbana na changamoto za kuvuka mto huo wakati wa mvua.
“Tanapa imeendelea kuweka juhudi kubwa katika kuboresha miundombinu mbalimbali ya Hifadhi ya Tarangire. Daraja la Matete ni sehemu ya juhudi za Serikali kuboresha miundombinu ya taifa na limekuwa mkombozi mkubwa katika kukuza utalii katika hifadhi hii,” amesema Kessy.
Mwonekano wa sehemu ya Daraja la Matete lililopo Hifadhi ya Taifa Tarangire ambapo lina urefu wa mita 85, lililoanza kutumika mwaka huu na kuondoa adha ya usafiri kwa watalii wanaotembelea hifadhi hiyo, kutokana na daraja la awali kuwa linajaa maji msimu wa mvua.
Ameeleza kuwa wakati wa msimu wa mvua, Mto Tarangire unapofurika hukatiza kabisa mawasiliano kati ya pande mbili za hifadhi, hali iliyokuwa ikisababisha changamoto kwa watalii na waongoza watalii kufika katika maeneo ya malazi yaliyo upande wa pili wa mto.
“Sasa hivi ni msimu wa mvua. Kama isingekuwa daraja hili, magari mengi yasingeweza kupita kwenda upande wa pili wa hifadhi. Kwa muda mrefu tangu kuanzishwa kwa hifadhi hii mwaka 1970, watalii walikuwa wanapata changamoto kubwa kuvuka mto huo wakati wa mvua,” amesema.
Ameongeza kuwa upande wa mashariki wa hifadhi hiyo kuna hoteli nyingi zinazopokea watalii, hivyo uwepo wa daraja hilo umeimarisha upatikanaji wa huduma na kurahisisha safari za wageni.
Kessy pia amesema Tanapa inaendelea kuboresha miundombinu mingine ndani ya hifadhi hiyo ikiwemo barabara, mageti na maeneo ya huduma kwa wageni.
Kwa mujibu wa Kessy, kwa sasa hifadhi hiyo ina mageti matatu na lango jipya la Mamire linatarajiwa kuwa la nne, huku maboresho pia yakifanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kuro ambapo jengo jipya la kupokea wageni limejengwa pamoja na maeneo ya mapumziko na vyoo.
Mwonekano wa daraja lililokuwa likitumika awali katika Hifadhi ya Taifa Tarangire,likiwa limejaa maji ambapo kuanzia mwaka huu halitumiki kufuatia ujenzi wa daraja jipya la Matete,ambalo limesaidia kuondoa adha hiyo waliyokuwa wakikutana nayo watalii wanaotembelea hifadhi hiyo.
Amesema Hifadhi ya Tarangire ni ya pili kwa kupokea watalii wengi nchini baada ya Hifadhi ya Serengeti, ambapo wakati wa msimu wa utalii hupokea hadi wageni 2,500 kwa siku, sawa na magari takribani 600.
Baadhi ya waongoza watalii wamesema daraja hilo limepunguza kwa kiasi kikubwa changamoto walizokuwa wanakabiliana nazo hapo awali.
Mmoja wa waongoza watalii, Felix Christian, amesema zamani walikuwa wakipata shida kuvuka mto huo wakati wa mvua kutokana na maji kufunika daraja la zamani.
“Mmefanya kazi nzuri. Zamani tulikuwa tunateseka kupita daraja la chini, lakini sasa tunapita daraja la juu hata mvua ikinyesha hakuna shida,” amesema.
Naye Suleiman Saitabau amesema daraja la zamani lilikuwa likifunikwa na maji wakati wa mvua na kusababisha kuchelewa kwa safari za watalii.
“Kiukweli zamani tulikuwa tunateseka sana. Maji yalikuwa yanapita juu ya daraja la zamani na kutuchelewesha. Tangu hili jipya lijengwe, inasaidia sana kupeleka wageni upande wa pili wa hifadhi,” amesema.
Awali, Msimamizi wa Kitengo cha Miundombinu katika hifadhi hiyo, Ofisa Daraja la Pili Goodluck Busumbilo, amesema hifadhi inaendelea kuboresha miundombinu ili kurahisisha shughuli za utalii.
Amesema hifadhi hiyo ina mtandao wa barabara zenye urefu wa kilomita 796 pamoja na Uwanja wa Ndege wa Kuro ambao hupokea wastani wa ndege sita hadi 12 kwa siku.