Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

DCEA yakamata zaidi ya kilo 7,900 za dawa za kulevya Kanda ya Magharibi

Mkuu wa wilaya ya Urambo Hamisi Mkanachi akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Tabora katika maadhimisho ya siku ya kupiga vita dawa za Kulevya yaliyofanyika katika uwanja wa shule ya Sekondari Uyui manispaa ya Tabora.

Muktasari:

  • Dawa hizo zimekamatwa wakati wa operesheni ya mwaka mmoja katika kanda hiyo.

Tabora. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Kanda ya Magharibi imekamata zaidi ya kilo 7,900 za dawa za kulevya katika operesheni zilizofanyika ndani ya mwaka mmoja, huku ikifungua kesi 49 dhidi ya watuhumiwa wa biashara hiyo haramu.

Akizungumza leo Julai 5, 2026 katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupiga Vita Matumizi na Biashara ya Dawa za Kulevya yaliyofanyika Kanda ya Magharibi, Kamishna wa DCEA Kanda hiyo, Christina Rweshabura alisema dawa zilizokamatwa ni kilo 7,735 za bangi, kilo 177.036 za mirungi na gramu 29.99 za heroin.

Alisema kati ya kesi 49 zilizofunguliwa, kesi 11 tayari zimetolewa hukumu, ambapo Jamhuri imeshinda kesi nane na kushindwa tatu.

Mbali na operesheni hizo, alisema mamlaka imeendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu madhara ya dawa za kulevya na tayari imewafikia watu zaidi ya 11,377 katika maeneo mbalimbali ya Kanda ya Magharibi.

"Tunaendelea kutoa elimu ili jamii ifahamu madhara ya dawa za kulevya na kushiriki katika mapambano dhidi ya biashara hiyo. Tunasisitiza pia ushirikiano wa taasisi za Serikali, asasi za kiraia, jumuiya za kimataifa na wananchi kwa ujumla katika kubuni mbinu za kudhibiti matumizi na biashara ya dawa za kulevya," alisema Rweshabura.

Wananchi wakisikiliza hotuba wakati wa maadhimisho ya siku ya kupiga Vita dawa za kulevya kanda ya Magharibi yaliyofanyika katika uwanja wa shule ya sekondari Uyui manispaa ya Tabora.

Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tabora katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Wilaya ya Urambo, Hamisi Mkanachi aliagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuongeza ushirikiano katika kukabiliana na wahalifu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Alisema wahalifu hao wanaendelea kubuni mbinu mpya za kulima, kuhifadhi na kusafirisha dawa za kulevya, hivyo vyombo vya dola vinapaswa kuwa wabunifu zaidi katika kuwabaini na kuwakamata.

Mkanachi alisema Mkoa wa Tabora unakabiliwa na changamoto ya uwepo wa maeneo makubwa ya hifadhi na misitu ambayo hutumiwa na baadhi ya wahalifu kulima bangi kwa siri.

"Wilaya ya Sikonge, kwa mfano, asilimia 95 ya eneo lake ni hifadhi, hivyo nguvu kubwa inahitajika kubaini na kudhibiti shughuli haramu zinazofanyika katika maeneo hayo," alisema.

Katika maadhimisho hayo, mmoja wa waathirika wa matumizi ya dawa za kulevya aliyepata nafuu baada ya matibabu na ushauri kutoka DCEA, Jimmy Batistuta, aliwataka vijana kujiepusha na matumizi ya dawa hizo akisema yalimgharimu afya yake.

Alisema aliwahi kusafirisha heroin kwa kuificha tumboni baada ya kufanyiwa upasuaji, hali iliyomsababishia matatizo makubwa ya kiafya.

"Nawashauri vijana waache kabisa matumizi na biashara ya dawa za kulevya kwa sababu ni adui wa afya na maendeleo ya maisha yao," alisema.

Naye mkazi wa Tabora, Junior Rikado, aliwataka vijana kutumia muda wao katika shughuli za maendeleo badala ya kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya, huku Hamida Hamidi akisema Serikali imeendelea kupanua fursa za kiuchumi kwa vijana, hivyo hawana sababu ya kujiingiza katika vitendo vinavyoharibu maisha yao.

Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupiga Vita Matumizi na Biashara ya Dawa za Kulevya huadhimishwa duniani kila mwaka Juni 26. Kwa Kanda ya Magharibi, maadhimisho ya mwaka huu yamefanyika Julai 5 kutokana na sababu mbalimbali.

Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni, "Ubunifu wa kimkakati, suluhisho la changamoto za dawa za kulevya," ikisisitiza umuhimu wa kutumia mbinu mpya katika kukabiliana na biashara na matumizi ya dawa hizo.