Dk Baluch alieleza Bunge yanayofanyika Balochistan
Mwenyekiti wa wanaharakati wa jimbo la Balochistan nchini Pakistan (BNM), Dk Naseem Baluch ameliomba Bunge la Ulaya kutathmini upya biashara kati ya nchi hiyo na mataifa ya ulaya kwa madai kuwa yanayoendelea katika jimbo hilo ni ukiukwaji wa haki za binadamu.
Ameeleza hayo kando ya mkutano wa Bunge la Ulaya kuhusu makubaliano ya mataifa ya ulaya na Pakistan ulioandaliwa na mbunge kutoka nchini Romania, Georgiana Teodorescu.
‘’Ninawashukuru wabunge wa mataifa mengine kwa kupaza sauti kutokana na yanayoendelea Balochistan, eneo ambalo lina rasilimali nyingi lakini limenyimwa haki,’’
‘’Nazungumza hapa kama shahidi wa ukiukwaji wa haki za binadamu, kutengwa na unyanyasaji unaoendelea kwa miongo kadhaa tena kwa nguvu ya kutisha" alisema Dk Baluch.
Alidai vyombo vya usalama Pakistan vinawabana viongozi wa kisiasa, wanafunzi, watetezi wa haki za binadamu na wanaharakati.
Akizungumza mbele ya wajumbe mbalimbali, Dk Baluch alisema, ‘’kuna giza huko Balochistan. Kuna takwimu mpya za watu kutoweka. Katika miongo miwili iliyopita maelfu ya watu wametekwa, baadhi yao waliuawa na wengine kuteswa.’’
Alidai kuwa hivi karibuni yalibainika makaburi ya halaiki na kwamba taarifa hizo pia zimeripotiwa na mashirika mbalimbali ya kimataifa likiwemo Amnesty International.