Dk Bashiru ampongeza Cherehani kutumia mfuko wa jimbo kuboresha Majosho Ushetu
Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Emmanuel Cherehani akiwa bungeni
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Bashiru Kakurwa, amempongeza Mbunge wa Jimbo la Ushetu wilayani Kahama mkoani Shinyanga, Emmanuel Cherehani, kwa kutumia kwa ufanisi Mfuko wa Jimbo (CDF) katika kutatua changamoto ya majosho ya mifugo katika jimbo lake.
Dk Bashiru ametoa pongezi hizo leo Juni 11, 2026 Bungeni jijini Dodoma, akieleza kuwa Mbunge Cherehani ni miongoni mwa wabunge wanaoonyesha mfano bora wa namna Mfuko wa Jimbo unavyoweza kutumika kuboresha huduma muhimu kwa wananchi, hususani katika sekta ya mifugo.
Akizungumza hayo Dk Bashiru amesema alipotembelea jimbo lake la Ushetu alikuta kulikuwa na ahadi ya waziri wa mifugo na uvuvi wa zamani, Luhaga Mpina ambayo ilikuwa haijatekelezwa ya kujenga josho.
Alisema alipoambiwa aliahidi kwamba atatekeleza kwa sababu ni ahadi ya waziri, lakini alisema anamshkuru Cherahani kwa kutumia mfuko wa jimbo kujenga josho na amemualika aende kulifungua.
“Hiki ni chanzo kingine kizuri cha kutatua changamoto ya majosho, na yeye kwa fedha za jimbo ameamua mwaka huu ni mwaka wa kurekebisha kwenye miradi ya mifugo,” amesema Dk Bashiru
Ameongeza; “Mwaka jana ilikuwa afya, Mwaka huu ni mwaka wa eneo la mifugo, na mimi naona sasa hivi huyu ndiye mbunge ambaye anaweza akaleta mfano wa namna ya kutumia vizuri mfuko wa jimbo katika kutatua changamoto tulizonazo”.