Dk Msonde atoa wito mafundi ujenzi kuimarisha usalama wa majengo
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Dk Charles Msonde akitoa tuzo kwa mshindi wa ufundi bora wa kike kwa mwaka 2026, Vaileth Jackson
Muktasari:
- Naibu Katibu Mkuu Ujenzi Dk Msonde amewataka mafundi kuzingatia sheria za ujenzi, akidokeza kuwa tuzo za mafundi 2026 zimeongeza ushiriki na kuhamasisha ubora sekta ujenzi nchini
Dar es Salaam. Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dk Charles Msonde, amewataka mafundi ujenzi nchini kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya ujenzi ili wanapopewa kazi wazitekeleza kwa viwango vinavyostahili.
Dk Msonde amesema maisha ya wananchi yako mikononi mwa mafundi kutokana na jukumu lao katika ujenzi wa majengo, hivyo wanapaswa kuhakikisha wanajenga majengo bora na salama ili kuepusha madhara kwa jamii.
Kauli hiyo aliitoa jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na mafundi ujenzi kwenye hafla ya utoaji wa Tuzo za Mafundi Bora 2026 iliyoratibiwa na kampuni ya FENIC Investments Ltd, ambapo kada saba za ufundi zilitunukiwa tuzo.
“Niwaombe mafundi, mnapotekeleza kazi zenu, msingatie sheria, kanuni na miongozo ya ujenzi. Mkifanya hivyo mtasaidia taifa letu kuwa na majengo imara yenye kuleta thamani na maisha bora kwa wananchi,” amesema.
Amesema kuanzishwa kwa Tuzo za Fundi Awards ni matokeo ya ubunifu na maono yaliyolenga kuwapa mafundi nafasi ya kutambuliwa na kuthaminiwa kwa mchango wao katika maendeleo ya Taifa.
Dk Msonde amesema ongezeko la washiriki kutoka mafundi 16,500 mwaka jana hadi 25,000 mwaka huu linaonyesha jinsi tasnia hiyo inavyoendelea kukua na kuvutia watu wengi zaidi.
Ameeleza kuwa matumizi ya teknolojia na uwazi katika mchakato wa tuzo hizo vimechangia kuongeza ushiriki wa mafundi wengi zaidi.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Dk Charles Msonde akimpa tuzo mshindi bora wa ufundi 2026 upande wa kiume, Swedi Ramadhani katika hafla maalum iliyofanyika Dar es Salaam, wengine pichani ni wadhamini mbalimbali wa tuzo hizo.
“Jambo lolote linaloendeshwa kwa uwazi huvutia washiriki wengi na kusaidia kuifanya tasnia hii kutambulika zaidi katika jamii,” amesema.
Amesema mafundi wana mchango mkubwa katika maisha ya Watanzania kwa kuwa makazi na majengo mengi yanayotumiwa na wananchi zaidi ya milioni 60 nchini yamejengwa na wao.
Dk Msonde amesema utoaji wa tuzo hizo unaongeza chachu kwa mafundi kuboresha kazi zao na kuwapa hamasa ya kujiajiri.
“Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuthamini mchango wa mafundi kwa kufanya maboresho ya sheria na mifumo mbalimbali ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za ujenzi,” amesema.
Ameongeza kuwa maboresho ya Sheria ya Manunuzi yameongeza thamani ya miradi inayoweza kutekelezwa na wakandarasi wazawa kutoka Sh10 bilioni hadi Sh50 bilioni, hatua inayolenga kuongeza ushiriki wa wataalamu wa ndani na kuhakikisha fedha za Serikali zinaendelea kuzunguka nchini.
Pia amesema mfumo wa matumizi ya fedha za ndani (Force Account) ulianzishwa kuwapa nafasi zaidi wakandarasi na mafundi wa kawaida kushiriki katika ujenzi wa miradi ya maendeleo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo hizo, Nickson Masabo, amesema mwaka huu wameendesha muhula wa pili wa tuzo hizo baada ya mafanikio makubwa yaliyopatikana mwaka jana.
“Lengo letu ni kuendelea kutambua na kuthamini mchango wa mafundi katika sekta ya ujenzi pamoja na kuwahamasisha kufanya kazi kwa ubora zaidi katika maeneo yao,” amesema Masabo.
Amesema tuzo hizo zimeendelea kuleta chachu ya maendeleo katika sekta ya ujenzi kwa kuhamasisha utoaji wa huduma bora na kuongeza thamani kwa Watanzania.
Masabo amesema mwitikio wa mafundi umeongezeka mwaka huu ambapo mafundi 25,000 walifikiwa ikilinganishwa na 16,500 mwaka jana, huku zaidi ya mafundi 7,000 wakijisajili kupitia mfumo maalumu wa kidijitali.
Ameeleza baada ya mchakato wa usaili na uchambuzi, washiriki 76 waliingia katika hatua ya mwisho ya kupigiwa kura.
Vipengele vilivyogombewa katika tuzo hizo vilikuwa ni fundi bomba, fundi umeme, fundi mwashi, fundi wa tiles, fundi wa rangi, fundi wa urembo na fundi wa kupaua.
Katika vipengele hivyo, washindi watatu walipatikana kwa kila kada, huku washindi wa jumla wakiwa wawili: Vaileth Jackson aliyeshinda tuzo ya fundi bora wa kike 2026 na Swedi Ramadhan aliyeshinda tuzo ya fundi bora wa kiume 2026.
Washindi hao walikabidhiwa tuzo pamoja na fedha taslimu.
Baada ya kupokea tuzo hiyo, Swedi amesema siri ya mafanikio yake ni nidhamu katika kazi na kuaminiwa na wateja wake.
Naye Vaileth amesema kujituma na kuwashauri wateja kuhusu namna ya kuboresha kazi kabla ya utekelezaji ndiyo sababu iliyomfikisha kwenye mafanikio hayo.