Dk Nchimbi aahidi kujengwa kongani ya vyakula, maziwa Sumbawanga
Muktasari:
- Jumatano ya Oktoba 29, 2025 ni siku ambayo Watanzania watapiga kura kuwachagua madiwani, wabunge na Rais. Kuanzia Agosti 28 hadi Oktoba 28, 2025 kampeni zinaendelea kwa vyama kunadi Ilani zao na ahadi mbalimbali watakazozifanya watakapoingia madarakani
Sumbawanga. Mgombea mwenza wa urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi ameahidi kujengwa kwa kongani ya viwanda vya kusindika vyakula na maziwa, Wilaya ya Sumbawanga, mkoani Rukwa.
Pia, Serikali ya CCM chini ya Samia Suluhu Hassan itahakikisha inakomesha mbolea na mbegu za ruzuku zinawafikia wakulima kwa wakati na wanaosababisha kuchelewesha wanachukulia hatua.
Dk Nchimbi amesema hayo leo Jumatatu, Septemba 8, 2025 katika mkutano wa kampeni za urais, ubunge na madiwani uliofanyikia Uwanja wa Shule ya Msingi Laela A, Jimbo la Kwela, Wilaya ya Sumbawanga.
Ni mkutano wa kwanza wa kusaka kura za CCM mkoani Rukwa, baada ya kuwasili kwa ndege akitokea Bukoba, Mkoa wa Kagera alihotimisha mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Baada ya uzinduzi wa kampeni kitaifa uliofanywa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Agosti 28, 2025 Uwanja wa Tanganyika Packers, Dar es Salaam, Dk Nchimbi na Samia waligawana maeneo.
Wakati Rais Samia akipiga mikutano Morogoro, Dodoma, Songwe, Njombe, Mbeya na Iringa, Dk Nchimbi alishambulia kanda ya ziwa akianza na Mwanza, Mara, Simiyu, Shinyanga, Geita na Kagera.
Katika mkutano wa Laela, Halmashauri ya Sumbawanga Vijijini, Dk Nchimbi ameeleza mambo mbalimbali yaliyofanywa miaka mitano iliyopita na yanayotarajiwa kufanywa mitano mingine iwapo watapewa dhamana na wananchi.
Ameanza kwa kuwapongeza kwa jitihada za kilimo akisema Samia anatambua mpango wao.
"Na ndiyo maana, miaka mitano ijayo tutajenga kongani ya kusindika vyakula na maziwa na itajengwa hapahapa Laela ili mazao ya wakulima yasiishie sokoni tu bali yaongeze thamani na kutoa ajira kwa vijana wetu,"amesema.
Katibu mkuu huyo wa zamani wa CCM amesema wanakusudia kujenga soko la mazao na Halmashauri ya Sumbawanga Vijijini imechagua lijengwe Laela.
Kongani hujengwa kwa miundombinu bora kama vile barabara, umeme, maji, mitandao ya mawasiliano na huduma nyingine muhimu ili kuvutia wawekezaji na kurahisisha uzalishaji wa bidhaa.
Malengo ya kongani za viwanda huwa ni kukuza uwekezaji wa viwanda, kutoa ajira kwa wananchi, kuongeza thamani ya mazao ya ndani, kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii na kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje.
Kuhusu kilimo, Dk Nchimbi amesema jitihada mbalimbali zimefanywa miaka mitano iliyopita ya kuwawezesha wakulima ikiwamo kuweka ruzuku kwenye mbolea na mbegu.
Amesema miaka mitano ijayo iwapo Samia atachaguliwa Oktoba 29, 2025 anakwenda kukomesha ucheleweshaji wa mbolea na mbegu hizo za ruzuku ili wananchi ziwafikie haraka wakulima.
Katika hilo, Winfreda Sokoni, mkazi wa Laela akizungumza na Mwananchi viwanja hapo amesema, hilo litakuwa jambo jema kama litasimamiwa ipasavyo.
"Unakuta msimu umefika, tukiuliza tunaambiwa mbolea na mbegu zipo lakini zinachelewa kutufikia, sasa kama anasema wanakwenda kusimamia iwe inawahi, wafanye kweli," amesema Winfreda.
Eneo la afya, Dk Nchimbi amesema miaka mitano iliyopita kwa kushirikiana na Kanisa Katoliki, wameboresha Kituo cha Afya Laela na miaka mitano ijayo watajenga vituo vitatu na kimoja kitajengwa Laela.
Amesema zahanati zilikuwa 55 na sasa ziko 67, "Hospital ya Wilaya hapakuwa na huduma ya upasuaji sasa wananchi wanaipata hapohapo na miaka mitano ijayo tutaboresha zaidi huduma katika hospitali hii."
Dk Nchimbi amesema shule za msingi zilikuwa 104 sasa 118, za sekondari zilikuwa 16 sasa 25 na walimu walikuwa 1485 sasa 1660.
Amesema miradi ya majisafi na salama imetekelezwa ikiwamo miradi mipya 15 ambayo imewezesha upatikanaji wa huduma hiyo kutoka asilimia 77 hadi 82.
Miaka mitano ijayo ameahidi itafikia zaidi ya asilimia 90 kwa kujengwa mabwawa ya maji na kuongeza visima vya maji.
Pia, ameahidi kujengwa stendi mpya Laela inayohusisha maduka: "Sasa angalieni msianze kunyang'anyana hapahapa maduka wakati bado hayajajengwa."
Kero ya barabara ambayo ilitolewa na Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Rukwa, Silafu Maufi amesema inakwenda kufanyiwa kazi akisema:"
Changamoto za barabara zenu zipo zinahitaji changalawe na lami, tunakwenda kuzifanyia kazi ili jina lenu la Kwela liendane na maendeleo.
Awali, akimkaribisha Dk Nchimbi kuzungumza, Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Rukwa, Silafu Maufi ameanza kwa kufikisha ombi kwa Dk Nchimbi akisema :"Tunaomba barabara inayoshuka Bonde la Rukwa kufanyiwa kazi. Ninajua ilani itatekelezeka mara dufu yake, lakini hili liangaliwe."
Silafu amesema: "Mama Samia hana deni na sisi, sisi ndiyo tuna deni na kura za Rukwa mmezipata. Madiwani wote 28 tunawaomba mumchague. mgombea wetu wa ubunge wa Kwela, Deus Sangu, kijana mzuri, kijana anayesikiliza, tumchague."
Mbunge wa zamani wa Busega, Mkoa wa Simiyu, Dk Raphael Chegeni amesema:"Uchaguzi ndani ya chama umemalizika, madiwani, wabunge na urais umemalizika na waliopatikana ni wa CCM na tarehe 29 twendeni tukawachague."
Dk Chegeni amesema kazi iliyopo mbele ni kuhakikisha CCM inashinda kwa kishindo, hivyo kila mmoja anapaswa kujitoa kuipigania.
Endelea kufuatilia Mwananchi kujua yanayotokea kwenye mikutano yake ya kampeni