Exim yaboresha huduma za kibenki Zanzibar
Benki ya Exim Tanzania kupitia mpango wake wa uwajibikaji kwa jamii (CSR) unaojulikana kama Exim Cares, imeendelea kufanya uwekezaji wenye manufaa makubwa katika jamii mbalimbali nchini, ikijikita zaidi katika maeneo yanayogusa maisha ya watu moja kwa moja. Kuanzia afya, elimu, uhifadhi wa mazingira hadi uwezeshaji wa jamii, Exim Cares inaakisi dhamira ya ya benki katika kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini Tanzania.
Visiwani Zanzibar, dhamira hii imejidhihirisha kupitia mfululizo wa utekelezaji wa miradi maalumu inayolenga kuboresha upatikanaji wa huduma muhimu. Miradi hii imejengwa juu ya imani kwamba maendeleo endelevu yanahitaji uwekezaji katika sekta ambazo jamii inazitegemea zaidi.
Kufuatia uzinduzi wa Tawi la Paje uliofanyika hivi karibuni, Benki ya Exim Tanzania imetoa mchango wake kwa jamii kupitia miradi miwili ambayo ni nguzo muhimu za maendeleo: usalama pamoja na elimu. Miradi hiyo ilihusisha utoaji wa samani kwa Kituo kipya cha Polisi cha Paje pamoja na mchango wa madawati 80 kwa Shule ya Msingi Paje.
Kusaidia Usalama wa Umma Katika Jamii Inayokua
Kadiri shughuli za utalii na uchumi zinavyoendelea kukua katika eneo la Paje, uwepo wa taasisi za umma zenye uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi unakuwa nguzo muhimu ya kudumisha utulivu wa kijamii na kuweka mazingira yanayowezesha jamii na biashara kustawi.
Kwa kutambua hitaji hili, Benki ya Exim Tanzania imechangia samani za ofisi kwa Kituo kipya cha Polisi cha Paje ambazo zitasaidia kukiwezesha kituo hicho kutoa huduma bora zaidi kwa wakazi wa Paje na maeneo jirani ambayo yanazidi kushuhudia ongezeko la watu.
Makabidhiano hayo yanaonyesha kwamba Benki inatambua kuwa ustawi wa jamii hauishii kwenye huduma za kifedha pekee, bali pia unahusisha kuimarisha taasisi ambazo wananchi huzitegemea katika maisha yao ya kila siku.
Hivyo, kusaidia taasisi hizo ni sehemu ya kujenga msingi imara wa maendeleo endelevu.
Kuwekeza katika kizazi kijacho
Kama sehemu ya kutekeleza dhamira hii, Benki pia ilitoa mchango wake wa madawati 80 kwa Shule ya Msingi Paje unaolenga kuboresha zaidi mazingira ya kujifunzia darasani.
Matokeo ya msaada huo yanaonekana wazi, kwa kuwa kila dawati linaweza kutumiwa na wanafunzi watatu na hivyo mchango huo unatarajiwa kunufaisha hadi wanafunzi 250 kila mwaka kwa kuwapatia mazingira bora, yenye heshima na faraja zaidi ya kujifunzia na kukua.
Kama ilivyo kwa shule nyingi nchini Tanzania, Shule ya Msingi Paje inakabiliwa na changamoto za miundombinu ambazo huathiri moja kwa moja ubora wa elimu.
Upatikanaji wa madawati hayo utawawezesha wanafunzi kuhudhuria masomo katika mazingira bora zaidi huku ukiwasaidia walimu kufundisha kwa ufanisi katika mazingira yaliyoimarishwa.
Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano wa Exim Bank Tanzania, Stanley Kafu akizungumza kuhusu mchango huo, alisema:
"Katika Benki ya Exim Tanzania, tunaamini kwamba, kuwekeza katika jamii ni msingi wa maendeleo endelevu. Elimu na miundombinu ya jamii ni nguzo muhimu za maendeleo, na tumejizatiti kuunga mkono miradi inayozalisha matokeo yenye maana na athari za kudumu katika maisha ya watu tunaowahudumia" alisema Kafu
Elimu inasalia kuwa moja ya nyenzo muhimu na yenye nguvu zaidi katika kuleta mabadiliko ya kijamii na kiuchumi. Kwa kuwekeza katika mazingira bora ya kujifunzia leo, Benki inasaidia kuibua na kuendeleza fursa kwa vizazi vijavyo kufikia uwezo wao kamili na kuchangia maendeleo endelevu ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Kuhusu ushirikiano wa muda mrefu na Zanzibar
Kwa pamoja, miradi hii inathibitisha ukweli kuhusu mtazamo wa Benki katika kuchochea maendeleo. Ufunguzi wa Tawi la Paje haukuwa tu kuhusu kusogeza huduma za kibenki karibu na wateja zaidi, bali pia kuhusu kujenga ushirikiano wa muda mrefu na watu, na jamii za Zanzibar.
Kupitia msaada kwa Kituo cha Polisi cha Paje na Shule ya Msingi Paje, Benki inaonyesha kwamba uwepo wake katika jamii una maana halisi na athari chanya za kudumu.
Juhudi hizi ni sehemu ya mkakati mpana wa Benki wa Uwajibikaji kwa Jamii unaojikita katika elimu, uwezeshaji wa jamii na maendeleo endelevu nchini Tanzania. Kadiri Zanzibar inavyoendelea kukua na kubadilika, Benki ya Exim Tanzania imejizatiti kuendelea kushirikiana na jamii, taasisi za serikali na wadau wa maendeleo katika kujenga mustakabali mwema ambao fursa za kiuchumi na maendeleo ya kijamii vinaenda sambamba.
Kwa Benki ya Exim, mafanikio hayapimwi kwa ukuaji wa kifedha pekee, bali pia kwa mchango chanya unaotolewa katika maisha ya watu na jamii tunazozihudumia.