Hekaheka majimboni wagombea ubunge wakipambana kuomba kura
Muktasari:
- Uchaguzi mkuu wa Tanzania umepangwa kufanyika Jumatano, Oktoba 29, 2025, wananchi watawachagua viongozi wao kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge na Rais
Dar/Mikoani. Ni heka heka majimboni! Ndivyo unaweza kutamka baada ya kampeni za ubunge kuzinduliwa katika majimbo mbalimbali nchini wiki iliyopita huku kila mgombea akinadi sera zake kuomba kuchaguliwa katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano Oktoba 29, 2025.
Kwa nyakati tofauti katika kampeni zilizoanza Agosti 28 mwaka huu, baadhi ya wagombea wameanza kujinadi kwa wapigakura wakiainisha mipango yao endapo watapewa ridhaa ya kuwaongoza kwa miaka mitano ijayo, wengi wakigusia miundombinu, elimu, afya na ajira.
Mbunge wa Viti Maalumu mkoa wa Arusha aliyemaliza muda wake, Cecilia Paresso (kulia) akimnadi mgombea ubunge wa Jimbo la Karatu, Daniel Awack katika mkutano wa kampeni uliofanyika leo Septemba 7, 2025 Kata ya Mang’ola, mkoani Arusha. Picha na Filbert Rweyemamu.
Mgombea wa Karatu, Daniel Awack (CCM) amejinasibu kuendeleza kasi ya maendeleo, akiahidi kuimarisha huduma za afya kwa kununua gari la kubeba wagonjwa litakalokuwa likisimamiwa na ofisi ya mbunge.
Mgombea ubunge wa Bukoba Mjini, Johnstoni Mtasingwa (CCM) amesema akipewa ridhaa atahakikisha anasimamia miradi yote iliyoanzishwa na itakayoletwa ili Manispaa ya Bukoba iwe kama Ulaya.
Wakati Mtasingwa akiyasema hayo, mgombea ubunge wa Rombo (CCM), Profesa Adolf Mkenda amesema endapo atapewa ridhaa ya kuendelea kulitumikia jimbo hilo kwa miaka mingine mitano, changamoto ya upatikanaji wa majisafi na salama itabaki kuwa historia.
Amesema tayari Serikali imeanza hatua za awali za utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Challa, unaolenga kusambaza huduma hiyo kwa vijiji 33 vya ukanda wa chini wa jimbo hilo huku akisisitiza atahakikisha miradi ya maendeleo iliyoanza haikwami, bali inakamilika kwa wakati.
Mgombea ubunge wa Same Mashariki (CCM), Anna Kilango Malecela mbali na kueleza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, ameahidi kusimamia ujenzi wa Barabara ya Mwembe–Miamba–Ndungu yenye urefu wa kilometa 90.1.
“Niwahakikishie, mkinipa nafasi nitahakikisha tunaendelea kusimamia ujenzi wa miundombinu ya barabara ili kurahisisha usafiri na biashara za wananchi. Pia, shule nyingi zimechakaa na zinahitaji kujengwa upya," amesema.
Mgombea ubunge wa Urambo mkoani Tabora kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Joyce Katobasho amesema endapo atapata ridhaa ya kuongoza jimbo hilo atahakikisha vijana hawalewi pombe tena na kukaa vijiweni bila kazi.
Katobosho amesema ukosefu wa ajira na fursa wilayani humo, ndiyo sababu ya vijana kujikuta wakijikita kwenye ulevi wa pombe na kushinda vijiweni.
George Mwalwiba anayewania ubunge wa Busokelo Wilaya ya Rungwe, akizindua kampeni zake katika Viwanja vya Shule ya Msingi Lwangwa Halmashauri ya Busokelo, ameahidi akichaguliwa, atatekeleza ilani yao ya uchaguzi kwa vitendo kwa kuwaletea wananchi maendeleo kwenye nyanja za kiuchumi, elimu, afya na miundombinu.
Jimbo la Kigoma mjini
Akizungumza kwenye mkutano wake wa kampeni leo Jumatatu Septemba 8, 2025, mgombea ubunge wa ACT - Wazalendo Kigoma Mjini, Zitto Kabwe ametaja mkakati wake wa kulinda masilahi ya wananchi na kugusia suala la uhamiaji.
Amesema amekuwa akiwatetea wananchi wengi wanaosumbuliwa na idara ya uhamiaji kuhusu uraia, hivyo ni wakati sahihi wa kuwasemea bungeni akisema viongozi wa vyama vingine hawajali.
"Mtu akikamatwa na uhamiaji nani wa kwanza kupigiwa simu? Nitumeni niende nikawatetee, nimekuwa nikipigania kuifufua bandari yetu, mnahitaji mtu ambaye atakwenda kuhakikisha masilahi ya Kigoma yanazingatiwa na sio mwingine ni mimi," amesema Zitto na kubainisha dhamira yake kuu kuwa ni kurejesha heshima ya Jimbo la Kigoma Mjini na mkoa mzima.
Amesema miradi mingi mkoani humo imedorora kutokana na kukosa usimamizi makini wa wabunge.
Mgombea ubunge wa Dodoma Mjini (CCM), Pascal Chinyele ameahidi kushughulikia changamoto kubwa zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo endapo atapewa ridhaa.
Amesema moja ya vipaumbele vyake ni kuhakikisha tatizo la maji linamalizika ili wananchi wapate huduma hiyo bila usumbufu na barabara za ndani katika jimbo hilo zinawekwa lami ili kurahisisha upatikanaji wa huduma na kupunguza adha kipindi cha mvua.
Saashisa Mafuwe anayegombea Jimbo la Hai kwa tiketi ya CCM, ameahidi akishinda atahakikisha katika mnada wa mifugo uliopo eneo la Mijohoroni, Kata ya Kia, kunajengwa kisasa ili kuwawezesha wafugaji kuuza mifugo yao katika mazingira bora na yenye tija.
Mgombea ubunge wa ACT – Wazalendo Jimbo la Kivule, Peter Madeleka amebainisha mambo matano ya kipaumbele akipewa ridhaa, ikiwamo miundombinu ya barabara na huduma za afya.
Akizungumza akiwa Viwanja vya Ngozoma Majohe, Madeleka amesema barabara nyingi zina hali mbaya lakini hakuna wa kulisemea hilo, ameahidi akipatiwa ridhaa, kitakuwa kipaumbele chake cha kwanza bungeni.
Lakini mgombea kupitia Chaumma, Jimbo la Mbagala, Hadija Mwago amejinadi kushughulia changamoto za elimu, afya na ajira.
Katika mkutano wake uliofanyika Kiwanja cha Kwaserenge Mbagala, Mwago ameahidi kubadilisha sura ya elimu kwa kujenga shule moja katika kila mtaa wa jimbo hilo, hatua aliyosema itasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi na kuhakikisha watoto wanapata elimu bora karibu na makazi yao.
Akizindua kampeni zake kwenye Jimbo la Kibamba, mgombea kwa tiketi ya CCM, Angelah Kairuki amesema amewiwa kugombea nafasi hiyo akilenga kushughulikia changamoto sugu hususani za maji, barabara, afya na ajira kwa vijana zinazowasumbua wakazi wake hususan vijana.
Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni zake uliofanyikia Stendi ya Mbezi Magufuli, jijini Dar es Salaam, Angelah amesema licha ya maendeleo yaliyofikiwa, bado Kibamba haijafikia kiwango kinachotarajiwa, kutokana na uduni wa miundombinu na huduma zisizoendelevu.
Jimboni Monduli mkoani Arusha, Leah Kweka anayewania jimbo hilo kwa tiketi ya Chaumma amesema akipewa nafasi ataweka kipaumbele katika kushughulikia changamoto ya maji, barabara na huduma bora za soko la Jumapili.
Akihutubia mkitano wa kampeni eneo la soko la wafanyabiashara wadogo la Jumapili, wilayani Monduli, Leah amesema tatizo la maji linawafanya watu wengi kushindwa hata kuoga.
“Kuna watu hapa wana siku ya tatu, hawajaoga kisa maji hakuna. Mkinichagua nitakwenda kuzungumzia hili bungeni ili jamii ipate huduma hii muhimu,” amesema mgombea huyo.
Pia, ameahidi kupigania kuboreshwa kwa miundombinu ya soko, kujengwa kwa vyoo na kuhakikisha wafanyabiashara wanapata mazingira bora ya kufanya shughuli zao.
Mgombea ubunge wa Jimbo la Kongwa, Isaya Mngulumi ameomba wananchi wamwamini na kumpa kura za ndiyo ili akakamilishe miradi inayoendelea kujengwa iliyoanzishwa na marehemu Job Ndugai na kufanya maboresho ya miundombinu ya barabara na maji.
Imeandikwa na Imani Makongoro, Habel Chidawali, Tuzo Mapunda, Janeth Joseph, Elizabeth Edward, Mintanga Hunda, Pawa Lufunga, Hamis Mniha, Nasra Abdallah, Florah Temba, Filbert Rweyemamu, Hawa Mathias na Hawa Kimwaga